Kansela wa Ujerumani kukutana na Trump licha ya tofauti zao

Kansela Merz aliwasili mjini Washington kambako atakutana kwa mara kwanza na Rais wa Marekani Donald Trump akiwa katika wadhfa wa kansela wa Ujerumani.

Katika mkutano wa ana kwa ana wakati wa chakula cha mchana, kansela wa Ujerumani analenga kuuimarisha uhusiano wa kibinafsi kati yake na Trump. Kwa kuzingatia mvutano katika mahusiano ya Ujerumani na Marekani tangu Trump aingie madarakani, ziara ya kansela wa Ujerumani inaangaliwa kwa tahadhari kuona kama Merz na Trump wataweza kudumisha uhusiano mzuri wa kibinafsi kati yao na iwapo watafanikiwa kuleta mwanzo mpya wa ushirikiano katika masuala yanayohusu sera ya kigeni.

Berlin | Kansela Friedrich Merz
Kansela wa Ujerumani Friedrich MerzPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Masuala mengine muhimu yatakayojadiliwa na viongozi hao ni pamoja na mustakabali wa jumuiya ya kijeshi ya NATO, vita vya Ukraine na mzozo wa ushuru wa forodha. Mkutano na waandishi wa habari katika Ofisi ya Rais Trump umepangwa kufanyika baadaye leo.

Ni wiki chache tu zilizopita ambapo kansela wa Ujerumani Friedrich Merz alionyesha kutokukubaliana na matukio katika Ofisi ya Rais Trump mwezi Machi, wakati rais huyo wa Marekani alipomdhihaki hadharani Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy na kumlaumu kwa vita vya Urusi dhidi ya nchi yake.

Soma pia: Kansela Merz asema vita vya Ukraine vitaendelea

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz anatumai ataepuka mashambulio ya maneno ya rais wa Marekani huku kukiwa na mzozo kuhusu Ukraine, ushuru wa forodha na uungaji mkono wa serikali ya Trump kwa chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD, kinachojiita chama Mbadala kwa Ujerumani.

Tangu kurejea kwake madarakani mwezi Januari, Trump amewatenga washirika wake kwa kufuata sera yake kali ya Marekani Kwanza.

Kuhusu Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Trump ametishia kuacha kuiunga mkono jumuiya hiyo iwapo nchi washirika hazitaongeza fedha kwenye bajeti zao kwa ajili ya matumizi ya kijeshi. Pia amesema Marekani itakata msaada wake kwa Ukraine hatua itakayozifanya nchi hizo ziwe dhaifu mbele ya Urusi.

Ujerumani Berlin 2025 | Zelensky alipomtembelea Friedrich Merz
Kushoto: Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky. Kulia: Kansela wa Ujerumani Friedrich MerzPicha: Pou/ROPI/picture alliance

Katika ziara yake mjini Washington kansela mpya wa Ujerumani, Friedrich Merz, anataka kuishawishi Marekani iunge mkono juhudi za nchi za Magharibi za kutoa msaada kwa Ukraine.

Soma pia: NATO kuidhinisha malengo ya ununuzi wa zana za kijeshi

Anataka pia kutuliza mvutano wa kibiashara ambao unahatarisha uchumi wa Ujerumani ambayo ndio nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya na wakati huo huo anatazamia kuipamba nchi yake ambayo inakosolewa kwa muda mrefu kutokana na kukunja mkono katika matumizi ya kijeshi.

Vyanzo: AFP/DPA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *