AU yaelezea wasiwasi kuhusu madhara ya marufuku ya Trump

Katika taarifa, AU imesema hatua hizo zitadhuru uhusiano miongoni mwa watu, mipango ya kubadilishana fursa za kielimu, ushirikiano wa kibiashara, na uhusiano mpana wa kidiplomasia uliojengwa pamoja na Marekani kwa miongo mingi. AU imetoa wito kwa serikali ya Marekani kutumia “mbinu ya mashauriano na kufanya mazungumzo yenye kujenga na nchi husika.”

Rais wa Marekani Donald Trump alitia saini marufuku ya kusafiri inayozilenga nchi 12 ambazo ni Somalia, Chad, Jamhuri ya Kongo, Equatorial Guinea, Eritrea, Libya, Sudan, Yemen, Afghanistan, Myanmar, Haiti na Iran. Trump amesema hatua hiyo inahitajika ili kuilinda nchi dhidi ya kile alichokiita “magaidi wa kigeni” na vitisho vingine vya usalama.

Pia aliweka marufuku kwa sehemu dhidi ya raia kutoka nchi zingine saba: Burundi, Cuba, Laos, Sierra Leone, Togo, Turkmenistan na Venezuela.

Amri hiyo ni sehemu ya msako wa uhamiaji aliouzindua Trump mwaka huu mwanzoni mwa muhula wake wa pili. Hatua hizo zimehusisha kuwahamishia El Salvador mamia ya raia wa Venezuela wanaoshukiwa kuwa sehemu ya magenge ya uhalifu, pamoja na juhudi za kuwanyima viza wanafunzi wa kigenina kuwafukuza nchini baadhi yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *