Sudan: Watu14 wameuawa katika shambulio la bomu Darfur

Takriban watu 14 wameuawa siku ya Jumatano, Juni 4, katika shambulio la bomu kwenye kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Darfur, magharibi mwa Sudani, shirika la kutoa misaada limesema, likiwalaumu wanamgambo wa RSF.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

“Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vimeshambulia soko na nyumba katika kambi ya Abu Shouk kwa mizinga mikubwa,” na kuua watu 14 na kujeruhi wengine kadhaa, kulingana na shirika moja la eneo hilo, moja ya makundi mengi ya kujitolea yanayotoa msaada kwa watu tangu kuanza kwa vita mnamo Aprili 2023 kati ya RSF na jeshi.

Kambi hii, ambayo inawapa hifadhi makumi ya maelfu ya watu waliokimbia vita, iko kwenye viunga vya Al-Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini, ambao umezingirwa na RSF kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Mji huu unakabiliwa na njaa, kama maeneo mengine ya nchi, kulingana na Umoja wa Mataifa, ambao unaelezea mzozo wa Sudani kama “janga mbaya zaidi la kibinadamu duniani.”

Al-Fasher ni mji mkuu wa mwisho wa mkoa katika jimbo la Darfur lililo nje ya udhibiti wa jeshi.

Vita hivyo ni kati ya jeshi linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan, kiongozi mkuu wa nchi hiyo tangu mapinduzi ya 2021, na RSF, inayoongozwa na makamu wake wa zamani, Jenerali Mohamed Hamdane Daglo.

Pia huko Darfur, ndege ya mizigo imeshambuliwa siku ya Jumatano muda mfupi baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Nyala, mji mkuu wa Darfur Kusini, ambao unadhibitiwa na RSF, kulingana na mashahidi.

Mashahidi wengine wameripoti kusikia milipuko katika maeneo kadhaa ya jiji kwa takriban saa moja.

Katika ripoti iliyochapishwa siku ya Jumatano, shirika lisilo la kiserikali la Human Rights Watch (HRW) limeshutumu mashambulizi ya anga ya “kiholela” ya wanajeshi wa Jenerali Burhane dhidi ya vitongoji vya makazi na maduka huko Nyala kati ya mwezi Novemba 2024 na Februari 2025, na kuripoti vifo vingi vya raia.

Vita nchini Sudani vimeua makumi ya maelfu ya watu, watu milioni 13 kuyahama makazi yao, na kuitumbukiza nchi hiyo katika baa la njaa.

Nchi sasa imegawanyika: jeshi linadhibiti kaskazini, mashariki na katikati mwa nchi, wakati RSF inashikilia sehemu za kusini na karibu zote za Darfur.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *