Majaji katika mahakama ya kimataifa ya ICC, mwezi Septemba mwaka huu wataanza kusikiliza kesi inayomkabili mbabe wa kivita nchini Uganda, Joseph Kony bila ya yeye mwenyewe kuwepo mahakamani, wakitupilia mbali rufaa iliyokatwa na upande wa utetezi.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Uamuzi huu wa majaji wa rufaa ulikuwa wa kwanza katika historia ya mahakama hiyo, ambapo sasa Septemba 9 mwaka huu wataketi kuamua ikiwa kuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha mashtaka dhidi ya Kony.
Kony anashtakiwa kwa makosa 39 ya uhalifu wa kivita na dhulma dhidi ya binadamu, vitendo anavyodaiwa kuvitekeleza kati ya mwezi Julai mwaka 2002 na Disemba 2005 kaskazini mwa nchi ya Uganda.
Kony ambaye alikuwa kijana wa kanisa na baadae kujiita nabii, aliunda na kuongoza kundi hatari zaidi la waasi lililofahalika kama Lords Resistance Army kwenye miaka ya 1980.

Kundi lake lilikuwa linapigana na wanajeshi wa serikali ya rais Yoweri Museveni, ambapo watu laki 1 waliuawa na watoto zaidi ya elfu 60 walitekwa nyara na kutumikishwa kama wapiganaji wa kundi hilo.
Makosa mengine ambayo Kony anakabiliwa nayo ni pamoja na mauaji, kutesa watu, utumwa wa kiongono na ubakaji.
Mwaka 2021, mahakama hiyo ilimuhukumu Dominic Ongwen, mwanajeshi mtoto ambaye baadae alikuja kuwa kamanda wa juu wa LRA, kifungo cha miaka 25 jela kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.