
Waasi wa M23 waliwauwa watu 21 bila hatia yoyote mwezi Februari katika jiji la Goma, wanalodhibiti, kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Human Rights Watch kupitia ripoti yake iliyotolewa Juni tarehe 3, inaeleza kuwa, waasi wa M 23 walitekeleza mauaji hayo kati ya Februari 22 hadi 23, baada ya kudhibiti Goma tangu mwezi Januari.
Aidha, Shirika hilo linasema kuna uwezekano mkubwa kuwa, huenda watu wengi ambao ni raia wa kawaida wamekuwa wakiuawa huko Goma chini ya M23.
Katika tukio moja, Human Rights Watch inasema, tarehe 22 mwezi Februari, waasi hao waliwauwa watu saba, karibu na kambi ya jeshi la serikali ya Katindo.
Mtafiti wa Shirika hilo kutoka ukanda wa Maziwa Makuu Clementine de Montjoye, amesema mauaji hayo yamesababisha wakaazi wa Goma kuendelea kuishi kwa woga.
Montjoye, amesema kwenye ripoti hiyo kuwa, mauaji hayo yameagizwa na wakuu wa M23 ili kuwatisha wakaazi wa Goma ili kuendelea kuwadhibiti na kuonekana kukubalika kwa namna yeyote ile.
Hata hivyo, msemaji wa M 23 Lawrence Kanyuka, amekanusha ripoti za wapiganaji wa kundi hilo kuhusika na ukiukwaji wa haki za binadamu yakiwemo mauaji ya raia wa kawaida, katika maeneo wanayodhibiti, kama ilivyoelezwa pia na ripoti ya Shirika la Kimataifa la Amnesty International.