Mali: JNIM yaongeza operesheni zake kote nchini

Kufuatia shambulio katika kambi ya Boulikessi (katikati ya Mali) ambalo lilisababisha vifo vya watu kadhaa siku ya Jumapili, Juni 1, Kundi linalodai kutetea Uislamu na Waislamu limelenga maeneo manne huko Timbuktu siku ya Jumatatu asubuhi.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Muda mfupi baada ya saa 4:00 asubuhi kwa saa za Mali, wakazi kadhaa wa Timbuktu wameiambia RFI walisikia mlipuko uliofuatwa na urushianaji risasi. Chini ya saa mbili baadaye, JNIM ilidai kuhusika na shambulio la kujitoa mhanga kwenye kambi ya kijeshi ya jiji hilo, na kufuatiwa na milio ya risasi kwenye uwanja wa ndege, na kukamata vituo viwili vya ukaguzi katika lango la kaskazini na mashariki mwa jiji hilo. Haya ni mashambulizi manee yaliyotekelezwa kwa wakati mmoja. JNIM iliripoti hakuna majeruhi. Kulingana na shuhuda kadhaa, wanajihadi walifanikiwa kuingia kwenye kambi ya kijeshi. Wanafunzi wanaosomea kwenye shule zilizo karibu na eneo la tukio walihamishwa mara moja, kulingana na mashahidi kadhaa.

Katika taarifa, gavana wa Timbuktu amethibitisha haraka “majaribio ya kujipenyeza kwenye kambi ya kijeshi” na “mabomu yaliyorushwa kwenye uwanja wa ndege.” “Hakuna uharibifu mkubwa,” gavana amehakikisha. Kwa upande wake, jeshi la Mali limedai “kuzuia” “jaribio la watu weye silaha waliotaka kuvamia uwanja wa ndege.” “Magaidi wametimuliwa haraka kwa uingiliaji kati haraka wa jeshi,” taarifa ya makao makuu ya jeshi imesema, ikitaja”magaidi kumi na watatu waliouawa” na vifaa vya jeshi kukamatwa. Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa vya habari, kundi hili la wapiganaji wakujitoa mhanga wa JNIM lilikuwa limeundwa na watu sita au saba, ambao walifanikiwa kuua askari kadhaa na kusababisha uharibifu mkubwa kabla ya kuuawa. Hakuna idadi kamili ya vifo ambayo ilieweza kuthibitishwa.

Gavana na jeshi wamesema kwamba shughuli za msako zilifanywa baadaye. Milio ya risasi ya hapa na pale imeripotiwa tena kwa RFI na wakaazi mchana. “Timbuktu ni mji ambao hakuna shughuli yoyote inayoripotiwa,” mmoja wao amesema. “Duka zimefungwa na tunakaa ndani.”

Zaidi ya watu 75 hadi 90 wamefariki huko Boulikessi

Jana, Jumapili, kambi ya kijeshi ya Boulikessi katika eneo la Douentza (katikati) ilishambuliwa na JNIM. Picha zilizotolewa na wanajihadi hao zinaonyesha miili mingi ya wanajeshi wa Mali waliouawa katika mapigano. Vyanzo kadhaa vya ndani, ikiwa ni pamoja na vyanzo vya usalama vya Mali, vinaripoti vifo vya zaidi ya watu 75 hadi zaidi ya 90. Wengi wao walikuwa wanajeshi wa Mali, lakini pia wasaidizi wa kundi la wanamgambo la Wagner kutoka Urusi. Wanajihadi hao pia walitoa video zinazoonyesha wanajeshi kadhaa wa Mali wakiwa wamekamatwa. Katika taarifa yake, jeshi la Mali limekiri kutokea kwa shambulio baya lililotokea huko Boulikessi, bila kutaja idadi ya waliouawa.

JNIM pia ilidai kuhusika na shambulio la bomu la kutegwa ardhini dhidi ya gari la kijeshi lililokuwa likitumiwa na Wagner kati ya Anefis na Kidal, na mauaji ya wanajeshi wawili wa Mali huko Konna, katikati mwa nchi, siku ya Jumatatu Juni 2. Siku kumi zilizopita, kambi ya Dioura, katikati mwa nchi, ilishambuliwa na wanajihadi wa JNIM, na wanajeshi zaidi ya arobaini waliuawa.

Mashambulizi mengine madogo pia yaliripotiwa katika mikoa ya Ségou na Koulikouro katika siku za hivi karibuni. Wanajihadi wa JNIM wanazidisha operesheni zao nchini humo na wanaonekana kudhamiria kuongeza shinikizo kwa jeshi la Mali na wasaidizi wake wa Wagner kutoka Urusi. Siku ya Jumapili, katika taarifa yake kuhusu shambulio la Boulikessi, Makao maku ya jeshi ilitoa wito kwa raia wa Mali “kusalia na umoja katika mshikamano na maombi” ili “kuunga mkono” vikosi vya usalama vinavyotetea “uhuru wa taifa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *