Mauzo kuni yapungua kwa asilimia 96.8, mkaa bado moto

Mauzo kuni yapungua kwa asilimia 96.8, mkaa bado moto

Dar es Salaam. Unaweza kusema ni hatua ya kwanza imepigwa na Tanzania katika kutokomeza matumizi ya nishati chafu hasa baada ya mauzo ya kuni kupungua kwa asilimia 96.8, ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza.

Ripoti hii ya uchumi wa kanda inaonyesha kuwa, katika robo ya mwaka iliyoishia Desemba 2024 mauzo ya kuni yalifikia Sh187.9 milioni ikiwa ni pungufu kutoka Sh5.81 bilioni yaliyokuwapo katika kipindi kilichotangulia.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio yaliyoonekana matumizi ya mkaa bado yanazidi kupanda ndani ya kipindi hicho. Mauzo ya mkaa yalifikia Sh7.7 bilioni katika robo ya mwaka ulioishia Desemba 2024 kutoka Sh5.81 bilioni iliyokuwapo mwaka uliotangulia.

Hili linaonekana wakati ambao Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii inaeleza kuwa katika kukabiliana na uharibifu wa rasilimali za misitu na nyuki nchini, mwaka 2024/2025 walifanya doria 405 za kiintelijensia na doria 17,510 za kawaida katika maeneo ya hifadhi za misitu na nyuki.

Kupitia doria hizo, watuhumiwa 3,459 walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali za kisheria.

“Pia doria hizo zimewezesha kukamatwa na kutaifishwa kwa magunia ya mkaa 36,625 yaliyovunwa bila kufuata utaratibu, mbao 40,621 zenye mita za ujazo 2,671, kuni zenye mita za ujazo 285 na magogo 1,267 yenye mita za ujazo 226.6,” alisema Waziri Pindi Chana alipokuwa akiwasilisha bajeti yake wiki hii Bungeni jijini Dodoma.

Pamoja na hayo, baadhi ya wadau wanasema jitihada zaidi zinahitajika ili kuhakikisha watu wengi wanaachana na mkaa na kwenda kwenye gesi.

“Achana na hii gesi ya mitungi ni gharama, namna rahisi ni kuhakikisha wale walio karibu na bomba la gesi asilia wanaunganishwa na watumie kama wanavyonunua umeme, vinginevyo watu watakuwa wanapewa mitungi wakimaliza wanaweka ndani kwa sababu hela za kujaza hawana,” amesema Belinda Semangale ambaye ni mkazi wa Ubungo.

Wakati yeye akiyasema hayo, Yusuph Msangi ambaye ni muuzaji wa gesi eneo la Tabata amesema ni vyema kuhakikisha urahisi unawekwa hasa kwa kupunguza tozo na kodi zinazofanya gharama za gesi kuwa juu, ili watu wengi waweze kumudu.

“Tuweke urahisi, watu wapewe motisha waanze kutengeneza mitungi ya gesi hapa nchini, vifaa vyote vya gesi hata majiko vinavyokuja kutoka nje visitozwe kodi, hili likifanyika bei itashuka, wateja wataongezeka na watu wataona hakuna ulazima wa kuendelea kutumia mkaa,” amesema Msangi.

Amesema kwa sasa watu bado wanaona mkaa ni rahisi kwa sababu wanaweza kupata kwa Sh1500 au Sh2,000 lakini gesi hadi mtu awe na kuanzia Sh25,000 ndiyo aweze kupata.

“Hii Sh25,000 unaweza kuiona ni ndogo lakini mtu anayelipwa Sh7,000 kwa siku anahitaji siku nne kuipata ikiwa kamili na hapo ni kama hana matumizi mengine, ikiwa ana familia ni ngumu sana kumshawishi kutumia gesi bila kuwa na mkaa kama njia ya ziada akitaka kupita vitu vigumu kama maharage,” amesema Msangi.

Kampeni ya kutomeza matumizi ya nishati chafu inafanyika duniani kote huku Tanzania ikiazimia  kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wake wanaachana na matumizi ya nishati chafu ifikapo mwaka 2034.

Wakati azma hii ikiwekwa, Mei 9 mwaka huu akiwa ofisini kwake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alisema Serikali imedhamiria kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kutoka asilimia 21 hadi asilimia 75 ifikapo mwaka 2030.

Amesema ili kufanikisha hilo, wameishirikisha sekta binafsi ili iweze kusaidia katika utekelezaji huku Serikali ikiendelea kuboresha, kuimarisha, kurahisisha na kuwezesha upatikanaji wa umeme na nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu.

“Hatua hii inalenga kupunguza athari za kiafya, mabadiliko ya tabianchi na kuboresha maisha ya wananchi,” alisema Dk Biteko alipotembelewa na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Youichi Mikami.

Kiuchumi imekaaje

Akizungumzia suala hili, Mtaalamu wa Uchumi, Dk Lutengano Mwinuka amesema badala ya kuweka nguvu zaidi katika kumaliza matumizi ya mkaa na kuni ni vyema itafutwe namna ambayo itaanza kupunguza kwanza kiasi cha matumizi yake.

Namna hiyo itawawezesha watu kutumia nishati kidogo kufanya shughuli walizokuwa wakizifanya awali kwa kiwango kidogo cha nishati hususan mkaa.

“Mfano kuna majiko banifu matumizi ya mkaa yanakuwa kidogo hii inaweza kuwa njia ya kwanza ya kupunguza matumizi ya mkaa ikiwa itatumika ipasavyo,” amesema Dk Mwinuka.

Amesema mbali na hilo ni wakati sasa wa kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ikiwemo mkaa usiotokana na rasilimali za misitu bali unaotengenezwa kwa kutumia mabaki ya vitu mbalimbali ikiwemo mazao.

Amesema mkaa mbadala unaweza kusaidia kuokoa misitu hasa kwa watu wanaosihi vijijini ambao wanaweza kuifikia kwa urahisi.

Lakini ili kuhakikisha watu wengi zaidi wanahamia katika matumizi ya gesi ambayo inatajwa kuwa na uchafuzi kidogo wa mazingira, anashauri kutazamwa upya kwa mifumo ya kikodi ili kufanya gesi, majiko na vifaa vingine kupatikana kwa gharama nafuu.

“Watu wanaangalia unafuu, mtu anaona achemshe maharage kwa gesi au mkaa, mtu anabaki katika mazoea kwa kuona gesi ni gharama na hawezi tumia kuchemsha maharage. Tunaweza kutazama gharama za nishati zetu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *