Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema hali ya kisiasa nchini ni tulivu.
Kauli ya Wasira kuhusu hali ya kisiasa nchini inatokana na kile alichosema kwamba alimsikia mwanazuoni mmoja akidai kuwa hali ya siasa Tanzania ni mbaya.
“Nimemsikia mwanazuoni, sijui mwandishi wa habari, akisema hali ya siasa Tanzania ni mbaya sana. Nilimuelewa yeye kwa sababu ana chama chake na hali ya chama chake ni mbaya sana,” amesema.
Amesema mwanazuoni huyo anachanganya hali mbaya ya chama chake na Tanzania kwa ujumla. “Hali ya kisiasa Tanzania ni stable (tulivu),” amesema Wasira kupitia mahojiano maalum na BBC jana usiku Mei 21, 2025.
Akijibu malalamiko kuhusu vyombo vya dola kunyamazisha upinzani, Wasira amesema hana ushahidi juu ya vyombo hivyo kunyamazisha wakosoaji, ingawa matukio yaliyotokea nchini yanachunguzwa na Jeshi la Polisi.
Miongoni mwa matukio aliyoyataja Wasira ambayo Jeshi la Polisi linayafanyia uchunguzi ni kujeruhiwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Dk Charles Kitima na kupotea kwa mwanaharakati Nyangali Mdude.
“Ukisema vyombo vya dola vinanyamazisha, napata tabu kukubaliana kwa sababu sina ushahidi wa vyombo hivyo kunyamazisha na kumnyamazisha nani? Maana wapinzani wa CCM wapo ndani ya vyama.
“Hoja nyingine inayozungumzwa ni kuhusu Tundu Lissu, Tundu Lissu hakunyamazishwa na vyombo vya dola bali alijikoki mwenyewe,” amesema Wasira.
Sakata la Martha Karua
Akizungumzia hatua ya wanaharakati kuingia nchini kufuatilia kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Lissu, Wasira amesema aliyewaponza wengine ni Martha, akidai kuwa aliingia nchini na kwenda mahakamani akieleza kuwa alifika kwa kofia mbili.
“Moja, amekuja nchini kama observer (muangalizi) kama mwanasheria, wakili na raia wa Afrika Mashariki. Hayo yote tulisema ni sawa, lakini akasema vilevile amekuja kama mwanasiasa wa Kenya mwenye chama chake kinachoitwa People’s Liberation Party.
“Kwa hiyo, akasema palepale Kisutu kwamba Serikali inaiogopa Chadema na akataka Serikali imuachie Lissu bila masharti. Vilevile, akasema kwamba Chadema iruhusiwe kugombea uchaguzi,” amesema Wasira.

Mwanaharakati wa nchini Kenya, Martha Karua.
Hata hivyo, amesema Karua kama aliingia nchini kwa lengo la kuwa mwangalizi wa sheria, “ukienda mahali kokote kufuatilia, huendi na judgement (hukumu) kazi ya kufuatilia ni kusikiliza na kutazama mwenendo. Sasa yeye alishakuwa judgemental (mtoa hukumu) ameshatoa uamuzi, ameshajua nani mbaya na suluhisho ni lipi.”
Kiongozi huyo wa CCM amesema Karua aliposema hivyo, walimjibu na akaondoka kitendo ambacho walikitafsiri kuwa alivuruga mfumo.
Hivyo, amesema kumruhusu aendelee kurudi nchini, shabaha yake si kuwa mwangalizi bali kuanzisha ghasia na kutaka kuwagawa Watanzania.
Wasira amesema mwanaharakati huyo wa Kenya, pamoja na kufika nchini, aliwachongea wengine.
Akieleza kama hatua ya kuzuiliwa wanaharakati hao kutaathiri malengo ya mkataba wa jumuiya ya Afrika Mashariki, Wasira amesema nchi yoyote ina haki ya kumkubali mtu yeyote kuingia au kutoingia na Serikali itakuwa na sababu.
“Nchi yoyote ina haki ya kukubali aidha uingie pale au usiingie na Serikali inazo sababu, kwamba amekuja mtu ana nia mbaya na Serikali ikasema kwa nia yako mbaya usiingie, huwezi kusema inaathiri Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema makamu huyo mwenyekiti.
Wasira amesema itakumbukwa hivi karibuni Lissu na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman walizuiwa kuingia Angola, lakini huwezi kusema Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imeharibika.
Karua ajibu
Kupitia mtandao wake wa X, Karua amemjibu Wasira, akimtaka atoe maelezo ya ukweli, si ya kubahatisha.
“Wewe ni mwanasiasa kama mimi na unaelewa kuwa siasa si kosa wala haramu. Bora hamkunifukuza peke yangu, mkavamia wengine ambao si wanasiasa. Kutoa maoni yangu siyo hatia kulingana na Katiba na sheria za Tanzania, Observer, (mwangalizi) mabalozi wa nchi za Ulaya ni wawakilishi wa kisiasa mbona hawakufukuzwa? Au hatia ni kuwa mwanasiasa? ameandika akihoji Karua.