Bima ya lazima kwa wageni yazalisha Sh16 bilioni Zanzibar

Bima ya lazima kwa wageni yazalisha Sh16 bilioni Zanzibar

Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema imekusanya Sh16.177 bilioni kwa miezi mitano kupitia malipo ya bima ya lazima ya Dola za Marekani 44 (Sh118,404) kwa kila mgeni anayeingia Zanzibar.

SMZ ilianzisha sera maalumu ya kutoza wageni wanaoingia nchini,na utekelezaji wake ulianza rasmi Oktoba mosi, 2024.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi, Mei 22, 2025 na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Juma Makungu Juma, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohamed Ali Suleiman, aliyehoji kuhusu kiasi cha fedha kilichokusanywa tangu kuanzishwa kwa sera hiyo pamoja na matumizi yake.

Katika swali lake la msingi, Dk Mohamed amesema kiwango hicho cha Dola 44 kimekuwa kikubwa na kuibua malalamiko makubwa kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

“Kwa kuwa lengo la EAC ni kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kijamii na kisiasa miongoni mwa nchi wanachama kwa lengo la kuboresha ustawi wa wananchi, naomba kujua ni kiwango gani Serikali inatambua changamoto hiyo kwa wananchi wa EAC wanaoingia Zanzibar,” amesema Dk Mohamed.

Aidha, Dk Suleiman alitaka kufahamu tathmini ya uingiaji wa wananchi kutoka nchi za EAC kwa kipindi cha Oktoba 2024 hadi Februari 2025.

Makungu, akijibu swali hilo, amesema kuwa Serikali imetambua changamoto hiyo na tayari imechukua hatua za haraka kwa kushirikiana na wadau wake, kwa kufanya maboresho ya mfumo wa tozo.

Amesema moja ya hatua hizo ni kupunguza viwango vya tozo kwa wananchi kutoka nchi wanachama wa EAC na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wanaoingia Zanzibar, ili kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuhamasisha utalii.

“Tumepunguza kiwango cha tozo kutoka Dola 44 (Sh118,781) hadi Dola 22 (Sh59,390). Lengo la kutoza kiwango hicho tofauti na wageni wanaotoka nchi nyingine ni kuendelea kuwa na ushirikiano mzuri katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa,” amesema Makungu.

Kuhusu tathmini ya uingiaji wa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha Oktoba 2024 hadi Februari 2025, na waliolazimika kukata kinga ya bima ya lazima Oktoba mwaka jana walikuwa wageni 2,372.

“Novemba mwaka huohuo, wageni walikuwa 2,609, Desemba wageni 6,743, Januari mwaka huu wageni 2,494 na Februari wageni 2,389,” amesema.

Hata hivyo, Makungu amefafanua kuwa Serikali haina makubaliano ya moja kwa moja na EAC kuhusu uanzishwaji wa bima ya lazima kwa wageni wanaoingia Zanzibar.

Amesema badala yake, hatua hiyo ni sehemu ya sera ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, iliyolenga kuanzisha bima ya lazima kwa wageni wote wanaoingia visiwani humo.

Katika kujibu hoja kuhusu matumizi ya fedha zilizokusanywa kupitia bima ya lazima kwa wageni, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya, amesema kuwa mapato hayo yameelekezwa kwenye huduma mbalimbali zilizokusudiwa, zikiwemo gharama za matibabu kwa wageni, usafirishaji wa miili ya wageni waliopoteza maisha, pamoja na kusaidia wageni waliokumbwa na changamoto kubadilisha tiketi zao.

Hata hivyo, Dk Mkuya ameeleza kuwa kwa sasa hawezi kueleza kwa usahihi ni kiasi gani cha fedha kimetumika, kwani jambo hilo linahitaji uchambuzi wa kina. Ameahidi kuwa taarifa kamili juu ya matumizi hayo itatolewa baadaye.

Aidha, amekiri kuwepo kwa changamoto katika ukusanyaji wa bima hizo kutokana na ukweli kuwa mfumo huo bado ni mpya, huku baadhi ya watu wakiendelea kutouelewa au kuukubali.

“Hata sisi watumishi wa Serikali, wakiwemo mawaziri, tumekutana na changamoto pale tunapotakiwa kuonesha vitambulisho kwenye viwanja vya ndege au bandarini.

“Wapo wanaojibu kwa dharau, ‘Hunijui mimi ni nani?’ Lakini vijana wanaosimamia hawana sababu ya kujua wewe ni nani, wao wanataka kujiridhisha kwa mujibu wa utaratibu,” amesema Waziri Mkuya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *