Wananchi ‘wamhamishia’ Dk Tulia Jimbo la Uyole, kumchukulia fomu

Wananchi ‘wamhamishia’ Dk Tulia Jimbo la Uyole, kumchukulia fomu

Mbeya. Wakati vuguvugu la kisiasa likiendelea kupamba moto nchini, wananchi wa Bonde la Uyole wamemuomba Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson kuchukua fomu ya kugombea jimbo jipya la Uyole katika uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mei 12, 2025 Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kutangaza kugawanya majimbo mapya manane, likiwepo jimbo jipya la Uyole mkoani Mbeya.

Pamoja na kuombwa kugombea na makundi mbalimbali, tayari wananchi hao wamechanga fedha kwa ajili ya kumchukulia fomu ya kuwania nafasi hiyo.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Mei 22, 2025, baadhi ya wananchi wametaja sababu za kumtaka Dk Tulia kugombea ni kutaka kuharakishwa kwa maendeleo, huku wakitaja mambo kadhaa ambayo yametekelezwa chini ya ubunge wake.

Miongoni mwayo ni uekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020, iliyoelekeza kujengwa kwa mradi wa kimkakati wa barabara ya njia nne yenye urefu wa kilometa 29 kutoka Nsalaga mpaka Songwe.

Mwingine ni ujenzi wa mradi wa kimkakati wa maji kutoka chanzo cha Mto Kiwira utakaokuwa mwarobaini wa adha ya maji kwa wananchi wa Mkoa wa Mbeya na Songwe.

Akizungumzia uamuzi huo, Amina Hussein mfanyabiashara katika Kituo cha Mabasi cha Usangu Kata ya Uyole, amesema kwa kipindi kirefu maendeleo yamechelewa na kitendo cha kugawa majimbo kumekuwa mkombozi kwao.

“Sasa sisi wananchi tunamtaka Dk Tulia, tunamchukulia fomu kabisa kwa sababu tayari hela tunayo, kilichobaki ni yeye kugombea ubunge tu kwenye jimbo hili jipya la Uyole, tuna mhakikishia kumpa kura za heshima wakati ukifika,” amesema mwananchi huyo.

Dereva bodaboda, Peter Joel amesema ni wakati sasa wa siasa kuwekwa pembeni wananchi wanataka maendeleo ya kweli.

“Na maendeleo haya tutayapata kupitia mwakilishi tunayemuoana anafaa kwenye jimbo letu ambaye ni Dk Tulia,” amesema Joel.

Mwenyekiti wa Bodaboda Jiji la Mbeya, Aliko Fwanda amesema kundi hilo litampigania Dk Tulia iwe mvua liwe jua mpaka kieleweke.

Awali, Diwani Kata ya Uyole, Daniel Njango aliliambia Mwananchi Digital kwamba kesho watafanya mapokezi ya mbunge huyo katika viwanja vya Shule ya Msingi Hasanga.

Amesema mapokezi hayo yatashuhudiwa na viongozi mbalimbali wa CCM sambamba na wa Serikali na makundi ya vijana ambao watamuomba Dk Tulia akubali ombi lao la kumchukulia fomu ili agombee kwenye jimbo hilo jipya la Uyole.

“Sio kwa bahati mbaya au maamuzi yangu, bali ni misimamo ya wananchi wenyewe ndiyo wanaomuomba Spika Tulia agombee baada ya kuridhishwa na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi CCM kwa 2020,” amesema.

Daniel amesema kikubwa kilicho wavutia ni pamoja na kutekeleza ahadi zake ambazo zimekwenda kutatua changamoto na kuleta suruhisho la wananchi kwa miaka mitano ya nafasi yake.

“Kesho Mei 23,2025,ndio siku rasmi ya  kusikia kauli ya  Dk, Tulia  kutoa mwelekeo wake  atagombea Jimbo gani ili kurejesha matumaini kwa  wananchi wenye kiu naye ,”amesema.

Kauli ya UVCCM

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Wilaya ya Mbeya, Clement Mwandemba amesema matarajio ya wananchi ni kumtaka mbunge huyo kugombea Jimbo la Uyole.

“Tuna imani sana na huyu Mama ndio maana mnaona makundi mbalimbali yanamtaka kugombea kipande cha Uyole, lengo lao ni kuhitaji maendeleo,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *