Washington. Ziara ya Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa nchini Marekani imegeuka shubiri baada ya mwenyeji wake Rais, Donald Trump kuibua vielelezo na ushahidi wa matukio ya mauaji ya wakulima weupe (Afrikaners) waishio Afrika Kusini.
Hata hivyo, Rais Ramaphosa pamoja kuonyesha kushtushwa na vielelezo hivyo vya video na picha zilizochapishwa kwenye magazeti, amemuomba Trump kumsaidia kupambana na makundi yanayodaiwa kuchochea chuki dhidi ya Afrikaners na mauaji hayo.
Rais Ramaphosa alifanya ziara katika Ikulu ya Marekani jana Jumatano Mei 21, 2025, yenye lengo la kufanya mazungumzo yatakayorejesha uhusiano baina ya mataifa hayo ambao umetetereka tangu Trump aingie Ikulu, Januari 20 mwaka huu.
Baada ya kupokewa nchini humo na kufanya mazungumzo, kama ilivyo kawaida kwa Trump kuwapeleka wageni wake katika Ofisi ya Oval ambako hupata fursa ya kuanika sehemu ya mazungumzo yao mbele ya vyombo vya habari.
Mambo yalianza kawaida kwa Trump kumkaribisha mgeni wake na kumtambulisha mbele ya waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali ambapo alianza kutoa picha ya hali ya uhusiano kati ya Marekani na Afrika Kusini.
Huku akidai kuwa na marafiki lukuki wanaoishi nchini Afrika Kusini, Rais Trump amesema Ramaphosa alimpigia simu akimuomba kutembelea nchi hiyo kwa lengo la kufanya mazungumzo.
“Sijui alipata wapi namba yangu lakini nilishangaa tu ananipigia akasema anataka kuja Marekani kuniona, nakushukuru sana Ramaphosa kwa kuja kunitembelea,” amesema Trump.
Ramaphosa akizungumzia lengo la ziara yake nchini humo, ametaja kauli za Trump kuhusu kuiwekea vikwazo Afrika Kusini na kukomesha ushirikiano katika baadhi ya maeneo hususan biashara, huku akisisitiza kuwa ziara hiyo inalenga kuweka mambo sawa.
“Tunaamini kwamba tunaweza kurejesha mahusiano yaliyokuwepo kupitia mazungumzo yetu. Pia tunahitaji tuzungumzie masuala ya jinsi tunavyoweza kuhamasisha uwekezaji zaidi kwa kila upande,” amesema Ramaphosa.
Ramaphosa ambaye katika ziara hiyo ameambatana na mawaziri, wafanyabiashara na wachezaji nguli za gofu nchini Afrika Kusini amesema Marekani inamiliki kampuni zaidi ya 600 nchini mwake, huku Afrika Kusini ikimiliki kampuni 22 tu nchini Marekani.

Bilionea, Elon Musk ambaye amekuwa akiituhumu Afrika Kusini kwa kuchochea chuki dhidi ya wakulima weupe (Afrikaners) akifuatilia mjadala wa Rais Donald Trump na Rais Cyril Ramaphosa. Picha na Mtandao.
Mauaji ya Wazungu yaibuka
Baada ya mazungumzo hayo, Rais Trump akaibua sakata la kuwepo madai ya mauaji ya ‘Afrikaners’ wanaoishi nchini Afrika Kusini huku akimtaka Ramaphosa kujibu madai ya uwepo wa mauaji hayo.
“Tuna makala, habari na maelfu ya ushahidi kuonyesha kwamba kuna mauaji ya Wazungu nchini Afrika Kusini. Naomba hiyo TV iwashwe tuone sehemu ya hayo matukio ya chuko, tafadhali punguza mwanga hapo ionekane vizuri,” amesema Trump.
Baada ya taa kuzimwa, kipande cha video kinachomuonyesha kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF), Julius Malema kilionyeshwa akizungumza bungeni kuhusiana na jinsi ambavyo Wazungu wanaoishi nchini Afrika Kusini wanapaswa kuuawa.
(Bunge hili linapaswa kufahamu kwamba watu wetu wataitwaa ardhi (ya Wazungu) iwe kwa kutaka ama kutotaka, Mheshimiwa Spika, hatujawahi kuogopa kuua na mageuzi yanafanyika hata kwa kuua, Kill the boer (wazungu wauawe),” anasikika Malema akitamka kauli hiyo.
Baadaye, Trump aliagiza kiwekwe kipande kingine cha video kikionyesha msururu wa magari ya Wazungu (Afrikaners) wakienda kuhudhuria maziko ya watu anaodai waliuawa (bila kutaja idadi) kikatili nchini Afrika Kusini.
“Mnachokiona hapo ni msururu wa magari ya Wazungu wakulima weupe ambao wamebeba misalaba wakienda kuhudhuria mazishi ya watu waliouawa. Na kila mmoja mnayemuona hapo amebeba kitu cheupe ambacho ni msalaba.”
“Sijawahi kuona jambo la kushtua kama hili, watu wote hao wameuawa,” amesema Trump.
Huku akikanusha kuwa hana taarifa ya kuwepo mauaji na mazishi ya watu hao wanaoonekana kwenye video hizo, Ramaphosa alimuuliza swali Trump iwapo ana taarifa za yalipofanyikia mazishi hayo ambapo Trump alimjibu kwa ufupi tu kuwa yametokea Afrika Kusini.
“We need to find out (tunapaswa kulifuatilia),” alijibu Ramaphosa kisha kimya cha dakika zaidi ya tatu kikapita marais hao wakitazamana na kunong’oneza watu waliokuwa pembeni yao.
Mshangao zaidi ulimshika Ramaphosa baada ya Trump kuletewa vielelezo vya makala za mauaji zilizochapishwa kwenye magazeti, zikionyesha picha za Wazungu waliouawa kwa kushushiwa vipigo na kuchomwa moto.
“Ukiangalia video unaona kabisa kwamba hawa ni watu wameuawa na viongozi wanasema wataua na kupora ardhi yao. Hizi ni habari za watu ambao wameuawa siku siyo nyingi, sijui ni kwa jinsi gani tutashughulikia suala hili,” amesema Trump.
Ramaphosa akamjibu Trump kuwa video hizo zinazomuonyesha Malema akihamasisha mauaji ya Wazungu na uporaji wa ardhi siyo sera wala msimamo wa nchi, huku akisema Afrika Kusini ni nchi yenye mfumo wa vyama vingi hivyo kila mtu anaongea analojisikia.
“Kuna wakati baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani vimekuwa vinafanya mambo ambayo ni kinyume na sera za nchi. Wanazungumza wanayojisikia kwa sababu ni haki inayolindwa kikatiba lakini haimaanishi kuwa huo ndiyo msimamo wa nchi,” amesema Ramaphosa.
“Hata takwimu za matukio ya mauaji nchini Afrika Kusini siyo yanayohusisha Wazungu bali watu weusi,” amesema.
Ramaphosa ameiomba Marekani kumsaidia kupambana na matukio ya uhalifu yakiwemo yanayodaiwa kuhusisha mauaji ya wakulima wa Kizungu nchini Afrika Kusini, huku Trump akisema matukio hayo yatasababisha maelfu ya Wazungu waishio nchini humo kukimbilia Marekani na kuahidi kulishughulikia.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.