Spurs yatwaa Ubingwa wa Europa League ikiichapa Man United

Spurs yatwaa Ubingwa wa Europa League ikiichapa Man United

Bilbao, Hispania. Pamoja na kufanya vibaya katika mashindano ya ndani ya Ligi Kuu England, Tottenham Hotspurs imeondoa ukame wa mataji baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi Manchester United katika mchezo wa fainali wa Europa League.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye dimba la San Mamés, Bilbao nchini Hispania ilishuhudiwa Man United ikipoteza mchezo wa kwanza katika mashindano hayo tangu ilipoanza kushiriki msimu huu.

Bao pekee la mchezo huo lilifungwa na Brennan Johnson dakika ya 42 kipindi cha kwanza na kudumu mpaka kipenga cha mwisho cha mwamuzi Felix Zwayer raia wa Ujerumani.

Baada ya kupata ushindi huo, Tottenham imeandika rekodi ya kuifunga Man United mara nne mfululizo katika mashindano yote msimu huu ikifanya hivyo mara mbili Ligi Kuu England, mara moja katika Kombe la Karabao na Europa League.

Ubingwa huo ni wa tatu kwa Spurs katika historia yake ikitwaa mara ya kwanza1971/72 na ya pili 1983/84 wakati huo mashindano hayo yakiitwa Kombe la UEFA.

Ni rasmi Spurs itacheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao licha ya kuwa nafasi za chini Ligi Kuu England.

Katika msimu ujao wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), England itatoa jumla ya timu sita zitakazo shiriki katika mashindano hayo ambapo Spurs itaungana na zile tano bora kwenye msimamo wa Ligi hiyo.

Msimamo wa Ligi Kuu ya England ikiwa imesalia mechi moja kwa kila timu unaonyesha Manchester United ipo nafasi ya 16 ikiwa na pointi 39 na Spurs ipo nafasi ya 17 ikiwa na pointi 38.

Manchester United sasa imepoteza fainali ya michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo baada ya ile iliyocheza mwaka 2021 dhidi ya Villarreal ambapo ilipoteza kwa mikwaju ya penalti 11-10.

Mara ya mwisho United ilichukua taji la Europa Leagu msimu wa 2016-2017 ikiifunga Ajax Amsterdam mabao 2-0.

Spurs ilifuzu hatua ya fainali kwa kuitupa nje Bodo/Glimt ya Norway kwa ushindi wa mabao 5-1 ambapo mechi ya kwanza nyumbani ilipata ushindi wa mabao 3-1 na mechi ya marudiano ugenini ikapata ushindi wa mabao 2-0.

Manchester United ilipenya na kuingia hatua ya fainali kwa ushindi mnono ikiifunga Athletic Bilbao mabao 7-1 kwani katika mechi ya kwanza ugenini iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 na iliporudi nyumbanio ikapata ushindi wa mabao 4-0.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *