Mashabiki Man United, Spurs walitibua Hispania kabla ya fainali

Mashabiki Man United, Spurs walitibua Hispania kabla ya fainali

Bilbao, Hispania. Saa chache kabla ya pambano la fainali ya Kombe la Europa League baina ya Manchester United na Tottenham Hotspur, jiji la Bilbao limeingia katika sintofahamu baada ya mashabiki wa timu hizo mbili kutuhumiwa kusababisha vurugu na kufanya uharibifu wa miundombinu ya mji huo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini Hispania, mashabiki wapatao 80,000 kutoka England wamefurika jijini Bilbao, wakati Uwanja wa San Mames una uwezo wa kuchukua mashabiki 52,114 tu, huku kila timu ikipatiwa tiketi 15,000 pekee.

Licha ya Polisi 2,000 kuwepo kwa ajili ya kuhakikisha usalama, hali imekuwa ngumu kudhibiti umati mkubwa wa mashabiki waliotawanyika mitaani na baadhi wakijihusisha na vitendo vya uharibifu.

Gazeti la El Correo limeripoti kuwa mashabiki wa Spurs wameharibu taa mbili za barabarani na kuzitumia kama ishara ya ushindi kwa kuzinyoosha juu mithili ya kombe. Mashabiki wengine wanadaiwa kupanda kwenye nguzo za taa na kuchukua samani zilizopamba mji huo.

Mbali na uharibifu huo, mashabiki wa Manchester United nao hawakubaki nyuma, ambapo baadhi yao wanadaiwa kumshambulia mwenzao na kusababisha Polisi wanane kuingilia kati kuzuia ugomvi huo usiendelee.

Taarifa zaidi zinasema kuwa mashabiki wa Spurs walionekana kuwa na fujo zaidi ambapo waliripotiwa kuwamwagia bia na kuwapiga mashabiki wa Manchester United katika mji wa San Sebastian, hali iliyoibua hofu kwa wakazi na wageni wa jiji hilo.

Bingwa wa Europa msimu huu atapokea zawadi ya fedha taslimu kiasi cha Euro 8.6 milioni (Sh25.3 bilioni) pamoja na nafasi ya moja kwa moja kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Fainali hiyo ya Europa League inatarajiwa kuchezwa leo saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, huku kila timu ikisaka ushindi ili kufuta machungu ya msimu mbaya katika Ligi Kuu ya England. Hadi sasa, Manchester United inashika nafasi ya 16 kwa alama 39, huku Spurs wakiwa nafasi ya 17 na alama 38.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *