Rais Nandi-Ndaitwah awafunda wanawake, awapa mbinu za kiuongozi

Rais Nandi-Ndaitwah awafunda wanawake, awapa mbinu za kiuongozi

Dar es Salaam. Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah amesema majaribu na kukatishwa tamaa ni sehemu ya masahibu yanayomkumba mwanamke yeyote anayepata nafasi ya kuwa kiongozi.

Jambo baya zaidi, amesema majaribu hayo hayatoki kwa wanaume pekee, bali jamii kwa ujumla, wakiwemo wanawake wenzake.

Amelisisitiza hilo, akihusisha na maendeleo ya teknolojia, akisema mitandao ya kijamii inatumika zaidi kuwatoa kwenye njia viongozi, hasa wanawake.

Rais Nandi-Ndaitwah amebainisha hayo leo, Jumatano, Mei 21, 2025, wakati akitoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa wanawake, ikiwa ni moja ya majukumu katika ziara yake ya kiserikali ya siku mbili.

Kiongozi huyo wa Namibia aliwasili nchini jana, Mei 20, 2025, akiambatana na mumewe, Epaphras Ndaitwah, na hii ndiyo ziara yake ya kwanza tangu alipoapishwa kuwa Rais wa nchi hiyo, Machi 21, 2025.

Katika mhadhara uliofanyika UDSM, Rais Nandi-Ndaitwah amewahamasisha wanawake kutokata tamaa, bali kujizatiti kwenye jambo wanalolifanya na kutarajia changamoto mbele yao, lakini zisiwavunje moyo.

“Niwaambie viongozi wanawake, mnapokuwa kwenye nyadhifa mnatakiwa kusimama wenyewe kwa sababu mtakutana na majaribio lukuki ya kuwatoa kwenye njia,” amesema.

Majaribio hayo, amesema, hayatatoka kwa wanaume pekee, bali hata wanawake na jamii kwa ujumla, hivyo ni wajibu wa viongozi wanawake kutekeleza wajibu wao huku wakiwa imara.

Katika mhadhara huo, amesema hali ni mbaya zaidi katika kipindi hiki chenye mitandao ya kijamii, ambayo aghalabu huitumia kuwachafua viongozi.

Hata hivyo, amesema yote hayo yanalenga kuwatoa viongozi hao, hasa wanawake, kwenye njia na mwenendo wa utendaji sahihi, hivyo wanapaswa kujiimarisha.

Rais Nandi-Ndaitwah ameeleza hayo akisisitiza ili kufikia lengo lolote ni muhimu kujizatiti na kukubali kukabiliana na mazingira, kadhalika changamoto zozote zitakazokukumba.

Katika hilo, amerejea historia yake ya kisiasa, akidokeza kwamba aliingia katika harakati hizo akiwa kijana, na kwa sababu alijizatiti, hakuyumba licha ya changamoto zilizomkabili.

Miongoni mwa changamoto alizozitaja ni kufungwa jela miaka mitatu akiwa na umri wa chini ya miaka 18, lakini alipotoka aliendeleza harakati na hatimaye sasa ni Rais wa Namibia.

Akiwa mahakamani, amesema ilivutia sana kwa sababu wakili aliyekuwa anamwakilisha alisema mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 18 hapaswi kutokea mahakamani.

Hata hivyo, amesema jaji alikataa na kusema inatokana na aina ya kesi sheria hiyo inaweza kuzingatia, hivyo kesi iliendelea hadi kufungwa miaka mitatu kisha akatoka.

Amesema safari yake hiyo, ilikumbwa na mitihani mingine lukuki, ikiwemo kulazimika kuondoka nchini mwake na kuishi mataifa mengine, ikiwemo Tanzania kwa miaka kadhaa akiwa na umri mdogo.

Amesimulia alipokuwa nchini kwa miaka takriban sita, alilazimika kujifunza Kiswahili kwa kuwa wengi kati ya aliokuwa anaongea nao walimtaka azungumze lugha hiyo ili wamwelewe.

“Dk Salim Ahmed Salim, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, alisema nisipoweza kuzungumza kwa Kiswahili ndani ya miezi sita itabidi nirudi kwetu. Nikamwambia Kate Kamba anifundishe hadi ukafika wakati nikawa najua na nikabaki Dar es Salaam,” amesema.

Yote hayo, amesema, alifanikiwa kwa sababu alijizatiti na hakutaka kuyumba katika safari yake ya kisiasa, ndiyo maana amefanikiwa na kuwa kiongozi katika nafasi mbalimbali nchini mwake na hatimaye Rais.

“Ukiwa na juhudi na ukijua unachotaka kufanya, utakifanya. Kama wanawake tusikubali kuondolewa kwenye njia na haitaisha hadi pale utakapoondolewa katika hii dunia,” amesema.

Amesema watu wanaweza kusema maneno mabaya, lakini viongozi wanawake hawapaswi kuyasikiliza, isipokuwa wajizatiti na kusimamia wanacholenga.

“Katika ulimwengu wa teknolojia, mitandao ya kijamii kuna habari mbalimbali mbaya zitaandikwa dhidi yako, lakini unapaswa kupuuza,” amesema.

Ameuhusisha mhadhara huo na historia ya kuinuka kwa wanawake, akisema ilianzia enzi za mkutano wa Beijing mwaka 1995, ambao baadaye ukatoka na maazimio na kuyashusha yatekelezwe na kila nchi.

“Hatima yako inapaswa kuandaliwa kwa namna unavyojiongoza wewe na wengine,” amesema.

Hata hivyo, amesema vijana wa sasa wana fursa nzuri kwa sababu watakuwa viongozi katika wakati ambao walipata fursa ya kusoma elimu stahiki.

“Kwa hiyo, mna bahati hampo kama sisi enzi hizo tulilokuwa tunapata elimu ya kibantu,” amesema.

Na kwa sababu hiyo, amesema: “Wanawake wana uwezo sawa wa kuongoza nchi zetu, bara letu na dunia kwa ujumla, tuwape nafasi.”

Hata hivyo, Rais Nandi-Ndaitwah amesema kwa kadri wanawake wanavyowezeshwa imebainika watoto wa kiume wameanza kuachwa nyuma.

“Namibia kwa sasa hatuna mke wa Rais anayefanya harakati za kuwainua wanawake, bali tuna mume wa Rais anayetakiwa kujielekeza kwa vijana wa kiume, hii ni changamoto kwa sababu wamebaki nyuma,” amesema.

Awali, akizungumza wakati wa mhadhara huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Tanzania chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere ilisimama kuwa kinara wa harakati za uhuru.

Katika elimu, amesema Tanzania inajivunia kuwa mshirika wa kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Namibia, na mmoja wa wanazuoni kutoka nchini ndiye aliyesimamia hilo.

Amesema Tanzania inavutiwa na hatua ya Namibia kukisambaza na kukikumbatia Kiswahili na kuifanya kuwa moja ya lugha inayofundishwa.

“Tumeanza safari ya kuhakikisha tunakuwa na usawa wa kijinsia katika sekta nzima ya elimu, ikiwemo ya juu. Tunatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kwa kuzingatia usawa,” amesema.

Akimwelezea Rais Nandi-Ndaitwah, Makamu Mkuu wa Chuo, Mipango na Utawala UDSM, Profesa Bernadetha Kilian amesema urais wake umefanya awe miongoni mwa wanawake 28 waliowahi kushika wadhifa huo duniani.

Amesema historia yake inavutia na kutoa elimu kwa Waafrika kwa ujumla, na kwamba amelelewa katika familia iliyothamini elimu licha ya kuwa chini ya mikono ya ukoloni.

Amesema kiongozi huyo aliondoka nchini mwake akiwa kijana na akaamua kwenda kupambania uhuru, na alijiunga na chama cha Swapo akiwa na umri wa miaka 14.

“Mwalimu Nyerere alikuwa akimuita kwa jina la Mama Swapo, na kwamba alihudhuria mikutano mbalimbali ya wakuu wa nchi na alijifunza kutoka kwa Mwalimu Nyerere,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *