Makalla amkingia kifua Shigongo ujenzi wa barabara

Makalla amkingia kifua Shigongo ujenzi wa barabara

Mwanza. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amewataka wakazi wa Wilaya ya Buchosa kutomhukumu Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo kutokana na ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Sengerema hadi Nyehunge kutoanza hadi sasa.

Makalla amesema Shigongo hana kosa kwa sababu yeye wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, alishiriki mchakato wa kumuondoa mkandarasi aliyekuwa akijenga barabara hiyo kutokana na mwenendo wake kusuasua.

Hata hivyo, Makalla amesema mkandarasi mwingine atakayetekeleza mradi huo ameshapatikana na Jumatatu Mei 19, 2025, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega walikuwa Sengerema kukagua miradi ya maendeleo, likiwemo suala hilo.

Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo.

Katika ziara hiyo, Ulega aliwahakikishia wakazi wa Sengerema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kumkabidhi mkandarasi mradi wa barabara ya Sengerema-Nyehunge tayari kwa kuanza kazi.

Makalla ameyasema hayo leo Jumatano Mei 21, 2025  kwa nyakati tofauti alipokuwa akiwasalimia wananchi wa Bokokwa na Nyehunge wilayani Sengerema mkoani Mwanza katika mwendelezo wa ziara yake ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Ufafanuzi wa Makalla ulichagizwa na swalli Peter Nyangara anayeishi Bokokwa, aliyemuuliza mwenezi huyo kuhusu ujenzi wa barabara hiyo  yenye urefu wa kilomita 54.

Akisoma ujumbe huo baada ya kusimama Bokokwa, Makalla amesema, “Peter anaomba kuuliza mradi wa ujenzi barabara ya lami kutoka Sengerema hadi Nyehunge mbona hautekelezwi? Tunaomba majibu,” alisoma ujumbe huo kwa umma.

Baada ya kuusoma, Makalla alitoa ufafanuzi kuwa ujenzi wa barabara hiyo utatekelezwa, akiahidi kuwa atakuwa balozi wa kuhakikisha mchakato huo unafanikiwa ili kuondokana na adha ya vumbi.

“Naomba Eric asihukumiwe kuhusu barabara ya Sengerema – Buchosa, nimeshiriki kumfuta kazi mkandarasi kwa mujibu wa sheria. Nimelisema hili la barabara maana isije kuwa fimbo ya wanasiasa wengine, naijua vizuri Serikali haikutaka kuchukua mtu atakayelipua ujenzi wa barabara au kuchelewesha mradi huu,” amesema.

Amesema walifanya uamuzi mgumu kwa masilahi ya wananchi wa Sengerema na Buchosa.

Kwa mujibu wa Makalla, akiwa Mkuu wa Mkoa Mwanza, kwa nyakati tofauti alikuwa akifuatwa na wabunge, Hamis Tabasamu (Sengerema) na Shigongo waliokuwa wakimwelezea kuhusu mwenendo wa mkandarasi wa awali kwamba hawaridhishwi naye.

Akizungumzia hilo, Shigongo amesema jimbo limefunguka katika sekta mbalimbali ikiwemo maji na elimu na sasa tayari kuna chuo cha ufundi katika halmashauri hiyo.

“Zipo changamoto, ikiwemo ya umeme kutofika kwenye baadhi ya vitongoji, hatujamaliza ila CCM inazifahamu na itazitatua, naomba msiwe na wasiwasi tembeeni kifua mbele,” amesema Shigongo.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja amemmweleza Makalla kuwa mkoa huo utaendelea kuwa ngome ya chama hicho kutokana na kazi nzuri inayofanywa na serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *