
Dar es Salaam. Wakazi waishio mikoa ya Pwani mwa Tanzania, wametakiwa kuchukua tahadhari kujikinga na ongezeko la hatari ya kuenea kwa magonjwa yanayoenezwa na mbu na njia ya hewa.
Magonjwa hayo ni pamoja na Uviko19, influenza na yanayoenezwa na mbu kama vile homa ya dengue, malaria na mengine ya aina hiyo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Mei 21, 2025, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe amesema ili kujikinga na madhara yatokanayo na magonjwa hayo, wananchi wote wachukue tahadhari.
“Natoa rai kwa wananchi wote kuzingatia kanuni za afya ili kujikinga na kuwalinda wengine dhidi ya maambukizi ya magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa, hasa wale wanaoishi maeneo ya ukanda wa Pwani ikiwemo Dar es Salaam ambao umeathirika zaidi,” amesema Dk Grace.
Amesema ni muhimu kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya, pamoja na kuvaa barakoa pale inapohitajika.
Kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vipukusi mara kwa mara pamoja na kudumisha usafi wa mwili binafsi na wa mazingira yanayowazunguka.
Ameshauri ni vema yeyote anaposikia dalili kufika katika kituo cha afya, “Magonjwa haya yanayosababishwa na virusi yana dalili zinazoshabihiana hivyo ni vigumu kuyabaini bila kupata vipimo vya maabara.
“Hivyo, nawasihi kuwahi katika vituo vya kutolea huduma mara mnapopata dalili zozote za homa, maumivu ya kichwa, macho, misuli, viungo, au vipele mwilini au dalili za magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa kama vile kikohozi, mafua, kuwashwa koo au kupumua kwa shida ili kupata vipimo na matibabu stahiki,” amesema.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya ina uwezo, utaalamu na mifumo madhubuti ya kufuatilia, kutambua na kudhibiti magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa pamoja na magonjwa mengine ya mlipuko.
“Tutaendelea kutoa taarifa sahihi kwa wakati kwa lengo la kuwalinda na kuhakikisha usalama wa afya za Watanzania wote,” amesema Dk Grace.
Mkurugenzi wa huduma za dharura na maafa, Dk Erasto Sylvanus amesema dalili si ugonjwa wa Uviko-19 hivyo watu wanatakiwa kupima pale wanapogundua dalili.
“Uviko-19 tangu ulipoanza ulikua mkali, ilipofika Mei, 2023 ulitangazwa siyo tishio kimataifa sababu wengi walishachanja na virusi walishapoteza nguvu, uliendelea kuwepo bila madhara kwa binadamu kulazwa na vifo.
“Tumeendelea kuwaona wagonjwa hao kila mwaka na vipindi vya Februari, Juni, Septemba mpaka Desemba huwa wanakuwa wagonjwa wengi, siyo mpya na wagonjwa wameendelea kuwepo.
“Kipindi hiki wanapata pia na wanaopimwa tumekuta wana Uviko-19. Ugonjwa haujaja tena ila bado upo, watu wajikinge,” amesema Dk Erasto.
“Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi, muhimu kuangamiza mazalia ya mbu, kuondoa maji yaliyotuama karibu na makazi, ikiwemo madimbwi, ndoo, chupa, matairi ya zamani na vifaa vingine vinavyoweza kuhifadhi maji,” amesema.
Muhimu kutumia vyandarua vyenye dawa na kupulizia viuatilifu ndani ya nyumba mara kwa mara ili kuua mbu waliopo ndani.
“Tunashauri katika kipindi hiki watu wavae nguo ndefu zinazofunika mwili hasa wakati wa jioni na alfajiri, sambamba na kufunga madirisha na milango au kutumia wavu ili kuzuia mbu kuingia ndani ya nyumba,” amesema.
Dalili za dengue
Hata hivyo, wataalamu wanasema dalili ya ugonjwa wa dengue ni homa ya ghafla, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu.
Dalili hizi huanza kujitokeza siku ya tatu hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa virusi vya homa hii.
Wakati mwingine dalili za homa ya dengue inaweza kufanana sana na dalili za ugonjwa wa malaria.
Mara nyingine huambatana na kutokwa na damu sehemu za fizi, mdomoni, puani, machoni, pia kwenye njia ya haja kubwa au ndogo.
Mtafiti wa tabia za mbu kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), Dk Nicholaus Govela amesema wapo wanaougua bila kuonyesha dalili na wanaendelea kuambukiza, “mara nyingi watu hawa huwa hawaendi hospitali lakini wanakuwa na virusi mwilini.”
Dk Govela amesema zipo aina nne za virusi vinavyoambukiza dengue vikiwamo den 1, den2, den 3 na den 4.
Hata hivyo, amesema mpaka sasa wanasayansi hawajaweza kubaini ni virusi vya aina gani vinasababisha homa hiyo kwa Tanzania, licha ya utafiti kuendelea kufanyika.
Inavyoenezwa
Virusi vya homa ya dengue vinaenezwa kutoka kwa mbu kwenda kwa binadamu baada ya binadamu kung’atwa na mbu mwenye maambukizi wa aina ya Aedes.
Viluwiluwi vya mbu hawa huweza kuishi katika mazingira ya ndani ya nyumba mpaka kuwa mbu kamili na kusambaza ugonjwa huu kwa binadamu. Mbu hawa huwa na tabia ya kuuma wakati wa mchana.
Mbu hawa hupendelea kuzaliana kwenye maji yaliyotuama karibu na makazi ya watu au hata ndani ya nyumba.
Hutaga kwenye madimbwi ya maji hasa sehemu yenye mafuriko, kwenye mapango ya miti, sehemu zenye mashimo au mapango yaliyotengenezwa na binadamu.
Pia hutaga mayai yao kwenye mapipa, vyungu na makopo ya maua, kwenye chupa na makopo yaliyotupwa ovyo, matairi ya gari, vifuu vya nazi, matambara katika viambaza vya nyumba na sehemu zozote zile zenye upenyo hasa katika lundo la uchafu uliopo katika viambaza vya nyumba.