UDSM kuja na teknolojia kuzalisha protini kwa mabaki ya mkonge

UDSM kuja na teknolojia kuzalisha protini kwa mabaki ya mkonge

Dodoma. Bodi ya mkonge kwa kushirikiana na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM, Tari Mlingano, NM – AIST) wapo mbioni kukamilisha utafiti ili kuangalia uwezekano wa kuzalisha protini kutokana na mabaki ya mkonge.

Protin hizo zitatumika kutengeneza chakula cha mifugo na shughuli nyingine, Bunge limeelezwa leo.

Hayo yamo katika taarifa ya hotuba ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliyoisoma leo Jumatano Mei 21, 2025 ambayo imebeba vipaumbele sita na mikakati 30 kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Amesema uzalishaji wa mkonge umeongezeka hadi kufikia tani 61,215.55 ikilinganishwa na tani 56,732.7 kwa mwaka 2023/24 sawa na asilimia 76.5 ya lengo la kuzalisha tani 80,000.

Amesema mikakati maalumu ya kuinua zao hilo muhimu katika uchumi wa nchi imewekwa na sasa hali inakwenda vizuri baada ya mwitikio wa wakulima.

“Bodi ya Mkonge imeanzisha Kituo Atamizi cha BBT Mkonge mkoani Tanga ili kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalumu kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa kutumia singa za mkonge,” amesema Bashe.

Amesema katika kuongeza thamani ya zao la mkonge, mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha uzalishaji wa nzi chuma (Blacksoldier flies) kwa kutumia mabaki ya mkonge, amepatikana na taratibu za kuanza ujenzi zinaendelea.

Kwa mujibu wa Waziri, Wizara kupitia Bodi ya Mkonge Tanzania ilipanga kununua mashine ya kuchakata mkonge, kukarabati miundombinu ya shamba la Kibaranga – Tanga na kuwezesha umiliki wa ardhi ya kilimo yenye ukubwa wa hekta 6,000.

Nyingine ni kuratibu usambazaji wa miche ya mkonge  milioni 3 na kutoa mafunzo kuhusu uzalishaji wa zao hilo kwa wadau 100,000 na maofisa ugani 500, ambao watakuwa msaada mkubwa katika maeneo yanayofaa kwa kilimo cha zao hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *