Mila potofu, umaskini vikwazo matibabu ya fistula

Mila potofu, umaskini vikwazo matibabu ya fistula

Mbeya. Wakati kila ifikapo Mei 23 dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Fistula Duniani, umaskini na mila potofu bado kikwazo kwa waathirika kupata tiba ya maradhi hayo.

Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa kati ya wanawake 2,000 hadi 3,000 wanaobainika kuwa na fistula kila mwaka, ni 1,500 pekee wanaofika kupatiwa matibabu, huku Mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza kwa idadi ya wagonjwa.

Mratibu wa Afua ya Fistula Tanzania kutoka Wizara ya Afya, Fidea Obimbo, alieleza hayo leo, Jumatano Mei 21, 2025, wakati wa mkutano wa wadau ulioandaliwa kwa ajili ya kufanya tathmini ya mikakati ya kupambana na ugonjwa huo na kupunguza athari zake kwa wanawake.

Majadiliano ya mkutano huo ni sehemu ya kuelekea  siku maadhimisho hayo yatakayofanyika Mei 23, 2025 mkoani Mbeya.

Amesema kwa Tanzania tatizo la fistula ni kubwa ambalo huchangiwa na hali ya wajawazito kuchanika wakati wa kujifungua na kusababisha mifumo ya haja ndogo na kubwa kutokea sehemu moja.

Baadhi ya wadau na wataalam wa afya wakiwa kwenye kikao cha tathimini ya mapambano dhidi ya Fistula. Picha na Hawa Mathias

“Tatizo la fistula ni kubwa sana hapa nchini. Takwimu zinaonesha kuwa kila mwaka wanawake kati ya 2,000 hadi 3,000 hubainika kuwa na fistula, lakini ni takriban 1,500 pekee kati yao wanaopata matibabu na kurejea katika hali yao ya kawaida,” amesema Fidea Obimbo.

Amesema kutokana na ukubwa wa changamoto hiyo, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Fistula Foundation, wamekuwa wakikutana kila mwaka kuweka mikakati ya pamoja ya kutokomeza tatizo hilo.

“Kwa kushirikiana na wadau, tumeweka mikakati ya kuhakikisha tunatokomeza kabisa fistula ifikapo mwaka 2030, kama tulivyofanikiwa kupunguza vifo vya uzazi kutoka watu 556 hadi 104,” amesema.

Wakati huohuo, amewataka wananchi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kutumia ipasavyo fursa ya matibabu bure ya fistula yanayotolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Kitengo cha Wazazi  Meta.

Kauli za wadau

Mkurugenzi wa Fistula Foundation, Clement Ndahani amesema tafiti mbalimbali zimebainisha kuwa ugonjwa wa fistula huathiri zaidi familia zinazotoka katika kaya maskini.

Ameeleza kuwa, kama wafadhili wakuu wa huduma za matibabu ya fistula, kwa mwaka 2024 wamefanikiwa kuwafikia wanawake 1,303, huku wakikadiria kuwahudumia wanawake 1,414 ifikapo mwaka 2025.

Huduma hizo ni pamoja na gharama zote za matibabu, ikiwamo upasuaji, ambapo kwa mgonjwa mmoja hutumia kiasi kisichopungua Sh2 milioni.

“Tumeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha huduma hizi zinawafikia makundi yote ya jamii. Lengo letu ni moja kurejesha tabasamu kwa kinamama waliokumbwa na fistula,” amesema Clement.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Dk Godlove Mbwanji amesema umefika wakati kwa wadau kushirikiana kikamilifu na Serikali ili kutokomeza kabisa ugonjwa wa fistula nchini.

 “Mjamzito hatakiwi kuwa na tatizo lolote baada ya kujifungua. Ni jukumu letu kuhakikisha mazingira ya uzazi salama na huduma za haraka zinapatikana kwa wote.

“Mama anapojifungua mtoto hatakiwi kuwa na tatizo lolote, tunajua ni muhimu sana kumlinda mama dhidi ya fistula ili kuwa na uzazi endelevu kwa kizazi kijacho na Taifa letu,” amesema Dk Mbwanji.

Kwa upande wake Jane Aloyce amesema kimsingi ujio wa huduma hizo ni kimbilio, kwani idadi kubwa kimama wenye changamoto hujifungia majumbani kwa kuona aibu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *