Dar es Salaam. Hekaheka na shamrashamra zimeanza kwa wanachama wa Chama Cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), tayari kupokea wanachama wapya zaidi ya 3,000 waliokihama Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Miongoni mwa wanachama hao ni wale waliokuwa viongozi wa ngazi mbalimbali Chadema.
Wanachama hao wanapokewa katika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, ikiwa siku mbili zimepita tangu kufungua pazia kwa kuwapokea wanachama 14 kutoka Chadema baadhi yao wakiwa waliokuwa wanaunda Sekretarieti ya uongozi wa Chadema uliomaliza muda wake.

Wanachama 14 waliopokewa na kutunukiwa nyadhifa za juu katika chama hicho kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chaumma ni Salum Mwalimu nafasi ya Katibu Mkuu, Benson Kigaila, Naibu Katibu Mkuu Bara wakati Devotha Minja akiwa Kaimu Makamu wa chama hicho Tanzania Bara.

Leo ukija katika viunga vya Ubungo Plaza na kuingia ndani ya ukumbi wenyewe utastaajabu kwani kumetawala nyimbo za kusifu ukombozi, huku wanachama wakiwa wengi lakini wote wamevalia fulana nyekundu zenye nembo ya mkono uliokunjwa ngumi.

Mpaka sasa wakati hayo yakiendelea ukumbini hapo ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, Kigaila ndiye pekee aliyewasili.