
Bingwa wa Europa League msimu huu atapatikana leo kwa mechi ya fainali baina ya Tottenham Hotspur na Manchester United itakayochezwa kwenye Uwanja wa Sam Mames, Bilbao, Hispania kuanzia saa 4:00 usiku.
Timu hizo zinakutana huku zote zikiwa katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa Ligi Kuu England (EPL) msimu huu ingawa zote zimenusurika kushuka daraja.
Manchester United inashika nafasi ya 16 kwenye msimamo wa EPL ikiwa na pointi 39 wakati Tottenham Hotspur inashika nafasi ya 17 ikiwa na pointi 38.
Baada ya kukwama kupata taji katika mashindano yote ambayo timu hizo zimeshiriki msimu huu, hii ni fursa muhimu kwa kila moja kumaliza msimu vyema kwa kutwaa taji na ile ambayo itapoteza itakuwa imekamilisha msimu wa ovyo zaidi na hapana shaka hatima ya meneja wa benchi la ufundi la timu itakayopoteza itakuw mashakani.
Uwanja wa San Mames ambao fainali hiyo itachezwa leo, unaingiza idadi ya mashabiki 53,289 na unamilikiwa na klabu ya Athletic Bilbao inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania ‘La liga’.
Pamoja na kufanya vibaya katika mashindano ya ndani hata Ligi Kuu England, Manchester United na Spurs zote zimeingia kibabe katika hatua ya fainali ya mashindano hayo kwa kupata ushindi wa idadi kubwa ya mabao kwenye hatua ya nusu fainali huku zikipata ushindi nyumbani na ugenini.
Spurs ilifuzu hatua ya fainali kwa kuitupa nje Bodo/Glimt ya Norway kwa ushindi wa mabao 5-1 ambapo mechi ya kwanza nyumbani ilipata ushindi wa mabao 3-1 na mechi ya marudiano ugenini ikapata ushindi wa mabao 2-0.
Manchester United ilipenya na kuingia hatua ya fainali kwa ushindi mnono wa mabao 7-1 ambapo katika mechi ya kwanza ugenini iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 na iliporudi nyumbanio ikapata ushindi wa mabao 4-0.
Ladha ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Europa League ipo kwa Manchester United kwani walitwaa taji hilo katika msimu wa 2016/2017 ikiichapa Ajax kwa mabao 2-0 kwenye fainali.
Tangu mashindano hayo yalipoanza kuitwa Europa League, Spurs haijawahi kutwaa taji wala kufika fainali ingawa kipindi hicho yalipokuwa yakiitwa Kombe la UEFA, iliwahi kutwaa mara mbili tofauti ambazo ni 1971–1972 na 1983–1984.
Kocha wa Spurs, Ange Postecoglou anaamini ushindi katika fainali ya leo utakuwa na maana kubwa kwake na timu.
“Ni vigumu kuainisha changamoto za miaka michache iliyopita. Kwa mtazamo wangu, nilikuja katika klabu nikiwa na malengo ya wazi.
“Nimejaribu kadiri niwezavyo kushikamana na mchakato huo wa kuifikisha klabu katika nafasi ambayo inaweza kutwaa mataji na wakati huo huo, kukipa nguvu kikosi na kubadili mfumo wa uchezaji.
“Imekuwa kazi ya haki na changamoto nyingi njiani. Kwa mchezo mkubwa kama huu [hapa], kuna fursa ya kutimiza angalau kazi kuu niliyopewa ambayo ilikuwa kuleta mataji kwa klabu,” amesema Postecoglou.
Kocha wa Manchester United, Ruben Amorim amesema kuwa kutwaa taji la mashindano hayo angalau kutapooza maumivu ya msimu mbovu ambao wamekuwa nao.
“Msimu huu umekuwa mgumu sana kwa kila mtu. Matokeo, mabadiliko ya wafanyakazi; unaweza kuhisi katika klabu yetu. Tunashughulikia hilo, tunabadilisha jinsi tunavyocheza. Tunapoandaa mchezo katika Ligi ya Europa, mazingira ni tofauti kidogo; basi unaweza kuhisi msisimko.
“Hakuna kitakachobadilisha msimu wetu, lakini kila mtu anajua kushinda taji la Europa kunaweza kutusaidia kuwa na hisia ambayo inaweza kutusaidia kujenga maisha yajayo. Tuna mambo makubwa zaidi ya kushughulikia ili kurudisha klabu hii kileleni; [taji hili] linaweza kusaidia, na kutupa nguvu ya kufanya kile tunachopaswa kufanya,” amesema Amorim.
Felix Zwayer ndiye amepangwa kuchezesha mechi hiyo ambaye atasaidiwa na Wajerumani wenzake Robert Kempter na Christian Dietz huku refa wa akiba akiwa ni Maurizio Mariani.