Simba nzima yaifuata Berkane Zanzibar

Simba nzima yaifuata Berkane Zanzibar

Simba imewasili visiwani Zanzibar tayari kwa maandalizi ya mechi yake ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane, Jumapili Mei 25, 2025.

Nyota wote wanaounda kikosi cha Simba wamejumuishwa kwenye safari hiyo wakiwemo Hussein Kazi, Aishi Manula na  Omary Omary ambao hawakuwemo kwenye msafara wa timu hiyo ulioenda Morocco kwa mchezo uliopita.

Baada ya kutua Zanzibar, Simba itafanya mazoezi kwa siku nne na Jumapili kuanzia saa 10:00 jioni itakuwa uwanjani kukabiliana na Berkane ambapo inahitajika kupata ushindi wa tofauti ya mabao matatu ili itwae ubingwa wa mashindano hayo.

Simba inalazimika kupata matokeo hayo kwa vile ilipoteza mchezo wa kwanza ambao ulichezwa kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane, Morocco kwa mabao 2-0.

Wakati Simba ikitua visiwani Zanzibar leo, wapinzani wao RS Berkane wanatarajiwa kuwasili kesho ambapo wataingia Zanzibar na ndege ya moja kwa moja kutoka Morocco ambayo itawasubiri hadi pale watakapomaliza mchezo.

Huu ni mchezo wa pili wa Simba katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu kuchezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar ambapo wa kwanza ulikuwa ni wa nusu fainali dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini ambao ilishinda bao 1-0.

Mchezo huo umelazimika kuchezwa New Amaan Complex kutokana na maagizo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ya kuamua fainali kutochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa vile ukarabati wake hujakamilika.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa mabadiliko hayo ya uwanja hayawapi hofu ya kutimiza lengo lao la kutwaa ubingwa.

“Hatuna budi kukubaliana na maamuzi ya wenye mpira wao. Sasa lazima tuonyeshe tofauti ya sisi Simba SC na vilabu vingine katika kuheshimu mamlaka. Tayari mabadiliko yamefanyika hatuna budi kuheshimu mabadiliko hayo.

“Ziko fikra nyingi za watu kwamba pengine ni figisu. Zote hizo zinabaki kuwa ni dhana lakini msingi wa CAF kufanya uamuzi huo ni kutokuwa na uhakika na ubora wa Benjamin Mkapa. Hawataki kuchukua risk (tahadhari) ya kupeleka mechi Benjamin Mkapa halafu yakatokea yaliyotokea katika mechi ya robo fainali,” amenukuliwa Ahmed Ally.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *