Ripoti: Watu 23 walibakwa kila siku mwaka 2024, sita wakilawitiwa

Ripoti: Watu 23 walibakwa kila siku mwaka 2024, sita wakilawitiwa

Dar es Salaam. Takwimu zinaonyesha kuwa watu 23 walibakwa kila siku nchini katika mwaka 2024, huku wengine sita wakilawitiwa, ripoti ya hali ya uhalifu na makosa ya usalama Barabarani 2024 inaeleza.

Ripoti hii ya Jeshi la Polisi iliyotolewa Mei mwaka huu inaeleza kuwa matukio ya kubaka na ulawiti yalisababishwa na utandawazi, imani za kishirikina, tamaa za kimwili, mmomonyoko wa maadili, ulevi na visasi.

Ikiwa imechapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inataja jumla ya watu waliofanyiwa ubakaji katika mwaka 2024 walikuwa 8,541 ikiwa ni pungufu ya matukio 150 ukilinganisha na yale yaliyokuwapo mwaka 2023.

Katika upande wa ulawiti, matukio yaliyorekodiwa yalikuwa 2,083 ikiwa ni pungufu ya matukio 450 ikilinganishwa na yaliyorekodiwa mwaka uliotangulia.

“Kama Jeshi la Polisi tutaendelea kuelimisha jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika usimamizi wa sheria hususan Sheria ya Makosa ya Kimtandao ya Mwaka 2015,” limesema Jeshi la Polisi katika mikakati yake ya kukabiliana na matukio haya.

Pia njia nyingine itakayotumika ni kuelimisha jamii kuzingatia na kufuata maadili ya Kitanzania, kushirikisha taasisi za kidini, wazee wa kimila na wadau mbalimbali katika kuhamasisha jamii ili kuachana na imani potofu za kishirikina.

“Pia Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, kutenga muda maalumu mashuleni wa kutoa elimu ya ulinzi wa fikra kwa watoto ili waweze kutambua viashiria vya watu wenye nia mbaya mfano kampeni ya ‘’tuwaambie kabla hawajaharibiwa’’,” imeelezwa.

Pia wamejipanga kuendelea kukusanya taarifa za kiintelijensia ili kubaini mtu, watu au kikundi, taasisi zinazochochea na kufadhili wahalifu wa makosa haya na upotoshaji wa maadili ya Kitanzania na kuchukua hatua za kisheria.

Wakati hayo yakielezwa, suala la malezi limetajwa kuwa moja ya kuendelea kuwapo kwa matukio haya.

“Wazazi siku hizi wanajali sana kazi, hawapati muda wa kuzungumza na watoto wao, hii ni mbaya, hata kama mtoto anakutana na changamoto inakuwa ni ngumu kupatiwa usaidizi wa haraka,” amesema Joseph John mkazi wa Ubungo.

Maneno yake yanaungwa mkono na Frolentina Maganga mkazi wa Ubungo ambaye anasema mbali na wazazi kujitenga katika malezi, utandawazi ni moja ya kitu kinachopaswa kuangaliwa vizuri ili kuhakikisha watoto hawaangamii.

“Hizi simu tunazowapa watoto siku hizi wakiwa wadogo zina mambo mengi, kama wazazi wengine hawapati hata nafasi ya kukagua mtoto alitafuta nini kwenye simu kwa sababu inaonekana, utajuaje mwanao anatumia simu uliyompa kwa usahihi,” anasema Faustina na kuongeza

“Si kila kitu kinapaswa kuigwa hasa kwenye kizazi hiki cha Kiafrika ambacho wazazi hawana uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya teknolojia.

Wote wawili kwa pamoja, walitaka sheria kali zitumike kuhukumu wanaofanya vitendo hivyo ikiwemo kuondoa mwanya wa ulipaji faini ili watu wakwepe vifungo, kwani huo unaweza kutumika kama mwanya wa wahalifu kutokea.

Maeneo yanayoongoza

Kwa mujibu wa takwimu, Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar ndiyo unaongoza kwa kusajili matukio mengi ya ubakaji ambapo kwa mwaka 2024 ilirekodi matukio 511, ikifuatiwa na Kinondoni, Dar es Salaam iliyokuwa na matukio 496, Dodoma (462), Tanga (457) na Morogoro matukio 444.

Katika upande wa ulawiti, Kinondoni ilirekodi matukio 230 ikifuatiwa na mjini Magharibi iliyokuwa na matukio 157, Arusha (181), Dodoma (145) Kilimanjaro (119) na Tanga (117).

Shida iko wapo

Akizungumzia suala hili, Wakili Dominic Ndunguru amesema moja ya jambo ambalo linafanya kesi hizi kuendelea kuripotiwa kwa wingi ni kutoshughulikiwa kikamilifu mahakamani, kutokana na watu kuamua kumalizana kindugu.

Hiyo ni kutokana na watekelezaji wa matukio haya kuwa ndugu wa karibu wa waathirika, hivyo wanapotaka kuendelea na jitihada ili kumaliza kesi hizi huleta mgongano ndani ya jamii.

“Hali hii mara nyingi hufanya kesi kuishia nyumbani, wanalipana fidia labda ya ng’ombe, Sh500,000 na wanakubali kusameheana na hii ipo hata kwa watu wanaopata mimba, tukio likitokea wanaona tukimfunga nani atalea, au aliyempa mimba ana familia nani ataitunza wanaamua kulipishana faini,” amesema wakili.

Tunatokaje?

Ndunguru amesema njia sahihi inayoweza kutumika kumaliza tatizo hili ni kuwatenganisha waathirika na jamii inayowazunguka, ili kuwapa nguvu ya kudai haki yao.

Amesema hilo linawezekana kwa waathirika kupelekwa katika nyumba salama kama ilivyokuwa kwa waliokimbia ukeketaji au ndoa za utotoni, ili kuwapa uhakika wa maisha yao kuendelea baada ya matukio hayo.

“Huko kwenye nyumba salama wapewe pia usaidizi wa kisaikolojia ili kuhakikisha wanakuwa salama si kimwili tu bali na kiakili,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *