‘Mtiti’ majimbo ya Dodoma, kwa Kibajaji watatu watajwa

‘Mtiti’ majimbo ya Dodoma, kwa Kibajaji watatu watajwa

Bajaji waliyosafirishiwa wananchi wa Jimbo la Mtera (Mvumi) miaka 15 iliyopita bado iko barabarani, lakini watu wanne wanatarajia kuipanda.

Lengo ni kutaka kushindana nayo katika mbio za kuliwania jimbo hilo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Lakini inaelezwa wenye kutegua kitendawili hiki ni wajumbe ambao wamebeba maono yake, licha ya ukweli kuwa safari bado ni ndefu.

Wakati kwa Kibajaji hali iko hivyo, inaelezwa vita nyingine ipo kwenye majimbo ya Mpwapwa, Dodoma Mjini na Kondoa mjini ambako joto ni kali na hakuna anayetabiriwa kushinda kutokana na nguvu ya ushawishi kutoka kwa watangaza nia.

Jimbo la Mpwapwa ambalo mbunge wake ni George Malima naye anapitia wakati mgumu kwa sababu kura za jimbo hilo zinaweza kugawanyika kwa ukanda kulingana na minong’ono kuwa tayari kuna makada wanaodaiwa kuwa na ushawishi kupita kwa wapigakura na kujionyesha kwenye matukio na mikusanyiko ya watu.

“Wengine hakuna shida sana, lakini kuna kada mmoja (jina tunalihifadhi) akiingia, kweli tutavutana, maana itabidi tupige kura za ukanda, vinginevyo itakuwa ni shughuli nzito, wengine wanasindikiza,” anasema mmoja wa wenyeviti wa kata aliyedumu kwa muda mrefu.

Hata hivyo Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Joel Kihombo anasema utabiri wa jimbo hilo kwa sasa ni mgumu, tusubiri muda ufike. Katika Jimbo la Kondoa Mjini vita ni kati ya Mbunge, Ally Makoa na Mbunge wa Viti Maalumu Mariam Ditopile, ambaye anatajwa pia huenda akajitosa kuwania.

Ditopile alishatangaza siku nyingi kwamba analitaka jimbo hilo na licha ya kuwa ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, alichagua kufanya kazi za uwakilishi kwenye wilaya hiyo yenye majimbo mawili na hapo amejiunga na madiwani kupitia halmashauri ya Kondoa mji.

Makoa amekuwa akionekana kwenye matukio mengi ya kisiasa na ya kijamii katika siku za hivi karibuni.

Jimbo pekee ambalo limetupwa kama sandakalawe, licha ya kuwa tayari kuna taarifa kuwa mmoja wa vigogo wa CCM naye analinyemelea ni la Dodoma Mjini. Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi ililigawa na kuzaliwa jimbo jipya la Mtumba.

Mtiti Jimbo la Mvumi

Jimbo hilo linaundwa na kata 22 zilizopo katika tarafa tatu za Mvumi, Makang’wa na Mpwayungu, lakini kundi kubwa la wagombea wanatajwa kuliwania, huku wengine wakienda kwa kipindi cha tatu bila mafanikio.

Kwa sasa, Livingstone Lusinde (Kibajaji) ndiye analiongoza jimbo hilo kwa miaka 15 tangu alipolitwaa kutoka kwenye mikono ya John Malecela na kwa wakati wote huo Kibajaji amekuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Ni vita ya wanaume tisa na mwanamke mmoja, ndivyo inavyoonekana huku wawili kati ya hao wakitarajiwa kuwa na mchuano mkali zaidi kama majina yao yatapitishwa kwenye vikao vya chama na kuteuliwa kuwa wagombea.

Kwa kuwa waliotangaza nia wote wanatoka CCM, watatakiwa kufuata utaratibu wa kuomba na kusubiri majina yao yapite kwenye chekecheke la mchujo wa wagombea watatu ndipo waingie kwenye upigaji wa kura tofauti na kipindi cha nyuma ambacho wagombea walikuwa wakipelekwa kwa idadi ya wote waliochukua fomu.

Wanaotajwa hadi sasa katika jimbo hilo ni Lusinde (Kibajaji) ambaye anatetea nafasi yake, Edson Sweti (mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Chamwino), Mwanga Chibago, Dk Michael Msendekwa ambaye ni Mhadhiri wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo na Stephen Lusinde.

Wengine ni aliyewahi kuwa Rais wa Serikali ya wanafunzi Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Lubeleje, John Lubote, Amos Kusaja (mkurugenzi mstaafu wa Bunda), Stephen Ulaya (mkurugenzi mstaafu wa Monduli) na mwanamama pekee, Happynes Mgongo.

Mwanga Chibago, Dk Michael Msendekwa, Lubote, Stephen Lusinde na Livingstone Lusinde walikutana kwenye uchaguzi wa 2020 katika kura za maoni ambapo Lusinde (Kibajaji) aliwaacha kwa mbali wenzake baada ya kupata kura 571, akifuatiwa kwa mbali na Dk Msendekwa aliyepata kura 122, huku Mwaga Chibago akiambulia kura 37.

Hata hivyo, hali inatarajiwa kuwa tofauti ikiwa Lusinde na Mwanga watapenya wote katika tundu la watu watatu, mpambano utakuwa mkali zaidi kwani wanatajwa kuwa wanakubalika kwa sehemu kubwa, licha ya kuwa wanatoka eneo moja lakini Mwanga ameikamata zaidi tarafa ya Mpwayungu ambayo inatajwa kuwa na wapigakura wengi.

Mbunge huyo ambaye alijipatia umaarufu wa jina hilo kutoka gazeti la Mwananchi mwaka 2010, anasema bado anahitajika na kwamba anaamini kuwa atashinda kwa kura nyingi zaidi kuliko watu wanavyodhani.

“Gazeti la Mwananchi mliniibua wakati ule, lazima niwaambie ukweli kwamba sina hofu wala mashaka katika kushinda jimbo la Mtera, nasema hayo kutokana na kelele za watu wengi wanaotaka niendelee baada ya kuona mchango wangu,” anasema Lusinde.

Akizungumzia nguvu ya wagombea wenzake, anasema hawezi kuwabeza, isipokuwa idadi ya wapigakura wanaomuunga mkono ndiyo mtaji wake.

Mwanga Chibago ndiye anayetajwa kwa sasa kwamba atatoa ushindani mkali kama ataingia kwenye tatu bora na Lusinde, kwani anatajwa kuwa miongoni mwa wagombea ambao licha ya kushindwa katika kura za maoni uchaguzi uliopita, aliendelea kubaki na jamii na maisha yake kwa sehemu kubwa yapo kijijini.

Mtihani wa mchujo

Wataalamu wa masuala ya siasa wanasema mtindo wa kuwa na majina matatu unampa nafasi kubwa Lusinde kupita tena, kwani kama itatokea kurudisha majina kwa kuangalia ukanda, huenda akaingia na watu wenye nguvu ndogo.

Matonya Chilindo kutoka tarafa ya Makang’wa anasema bado wanamuona Lusinde kama kioo chao, kwani wanamlinganisha na wabunge wengine waliokuwa kabla yake kwamba anafaa zaidi ya hao.

“Mimi ni mjumbe kutoka kwenye tawi, kura nitapiga, lakini ukweli Lusinde tutasonga naye na hata wanaotoka kwenye tarafa yangu ningewashauri wagombee udiwani, lakini huku wanachelewa, kama hatakuwa huyo bora twende na Mwanga Chibago, maana naye amekuwa karibu na sisi wakati wengine tunawaona wakati wa uchaguzi tu,” anasema Chilindo.

Mmoja wa viongozi wa CCM Mkoa wa Dodoma anasema wote wanaogombea wanapaswa kujipima na kutambua kuwa lazima jina la Lusinde litakuwepo, hivyo waingie wakiamini wanakwenda kushindana na aliyeko madarakani.

“Lusinde ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, unakataje jina lake na anatetea kiti, tukimkata ina maana hata kwenye chama tumebeba mtu dhaifu, kwa hiyo watambue atakuwepo ingawa mimi siingii kikao cha uamuzi lakini huo ndiyo ukweli, waambieni wakajipime presha kwanza,” anasema mjumbe huyo kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *