NIKWAMBIE MAMA: Viongozi wabovu sasa iwe mwisho

NIKWAMBIE MAMA: Viongozi wabovu sasa iwe mwisho

Mfalme Juha alikuwa bingwa wa kutatua matatizo kwa njia za mkato. Mara anapolitatua linarudi likiwa limetengeneza madhara ya tatizo (side effects) mabaya kuliko tatizo lenyewe. Lakini hakuwa na njia mbadala kwa sababu yeye mwenyewe alikuwa hamnazo, halafu alikuwa ndiye kila kitu katika utawala wake. Nani mwingine angeweza kuiongoza nchi iliyoitwa “Kichaa”?

Sikatai kwamba Mfalme anaweza kutoa maamuzi magumu kwa makusudi ili aone mapokezi ya upande wa pili. Suleiman aliamuru mtoto aliyegombaniwa na mama wawili akatwe katikati, na kila mama achukue kipande.

Lakini alikuwa ametega ili aone mapokezi ya hukumu yake kutoka kwa kinamama hao. Mwisho wa siku alimgundua mama halisi wa mtoto na kumkabidhi mwanaye.

Lakini Juha alizidisha. Yeye ndiye aliyechunguza matatizo ya wananchi wake, akaenda kuziwakilisha kwake mwenyewe na kuzifanyia kazi.

Palipokuwa na tofauti yeye ndiye aliyezivumbua na yeye mwenyewe kuzirekebisha.

Alipoletewa mashitaka akageuka kuwa hakimu! Kifupi alikuwa sawa na mpiga kona aliyekwenda kufunga bao la kichwa kabla mpira haujaguswa na yeyote!

Alianza na upelelezi kukusanya matatizo ya wananchi wake mtaani. Akagundua kuwa masikini walio wengi hawakwisha kulalamikia hali ngumu ya maisha nchini mwake. Mzee alitoa kubwa moja ambayo hadi leo hakuna nchi yoyote iliyojaribu kufuata.

Aliamuru kufutwa kwa tofauti ya bei katika manunuzi. Akatangaza bei ya Shilingi Moja kwa kila kitu kimoja. Alizingatia kuwa masikini angeweza kumudu kununua kwa Shilingi Moja.

Nchi ikawa na wazimu kuliko ilivyoitwa. Nyumba iliuzwa Shilingi Moja, na nyanya ikauzwa bei hiyohiyo. Watu wenye mitaji kutoka nje waliingia kwa wingi na kuhamisha rasilimali kubwa ya Kichaa. Ungekuwa Shilingi kumi tu basi ungeweza kuwa na mtaa wako. Maisha yalinukia uturi kwa matajiri, japo kwa masikini hali ilikuwa ileile.

Masikini hawakujishughulisha sana na hilo. Wao kila siku walikuwa wakishitakiana kwa mambo madogo kama kuangaliana vibaya, kupigana vikumbo na kadhalika. Mmoja aliyefuga mbwa koko aliburuzwa barazani (hakukuwa na Mahakama) kwa Mfalme kushitakiwa.

Ilitokea baada ya mbwa wake kumgegeda mguu mpita njia. Mfuga mbwa kwa jinsi alivyokuwa chizi akauliza: “Bwana wewe aliyekuluma ni nani; mimi au mbwa?” Alipojibiwa ni mbwa akashangaa kwa yeye kuitwa barazani.

Ati Mfalme naye akaona sawa. Akaamuru samansi na kisha hati (RB) ya kukamatwa mbwa. Mbwa akashitakiwa lakini sikumbuki alipewa adhabu gani, lakini kwa Mfalme alivyo angeweza kumuamuru kugharimia matibabu ya mhanga.

Mfalme huyuhuyu aliletewa kesi na mtu mwingine: “Wanangu walienda kuiba ndizi kwa bibi kizee huyu. Lakini walipoparamia dirishani nyumba ikabomoka, wakafa wote. Huyu bibi ni mwanga kabisa; ilikuwaje akajenga nyumba iliyobomoka kabla watoto hawajaiba?” Mfalme naye ati akatikisa bichwa lake kwa huzuni na kumuuliza mshtakiwa “Kwa nini umeua watoto?”

Huyu bibi alijitetea kuwa alilipa fedha kwa ujenzi wa nyumba bora (ya udongo). Kama ni tatizo basi lilisababishwa na fundi mjenzi.

Fundi naye akaruka na kudai kuwa aulizwe mchanganya udongo. Mchanganya udongo akamrushia zengwe mtia maji. Mtia maji ndiye aliyemaliza ubishi: akakubali kuwa alifanya kosa. Wakati akitia maji kwenye udongo alipita mtu mnene kama meli ya mafuta, hivyo katika mshtuko wake akazidisha maji kwenye udongo.

Kwa sifa na mbwembwe kama kawaida yake, Mfalme akaagiza kukamatwa kwa huyo mtu mnene. Unakuwaje mnene hata kuchukua nafasi isiyo ya kwako duniani?

Bonge likaletwa na si ajabu baraza ilihamia uwanjani siku hiyo. Katika kulihoji wakagundua kuwa lilihamia nchi ya Kichaa baada ya sera ya “Kitu Kimoja Shilingi Moja”.

Yeye hakuelewa uwekezaji wala biashara. Alifanya kazi yenye mshahara mdogo usiopungua Shilingi Moja kwa siku. Kwa hiyo kila siku alikuwa na uhakika wa kula mbuzi mzima! Na alikula kweli.

Mtu anayedhani kuwa Afrika imefanana na nchi ya Kichaa anakosea sana. Kule mambo yalikuwa wazi, na chizi mkubwa alikuwa mmoja tu; Mfalme. Mshtaki ni yeye, Mpelelezi wa kesi yeye, Mwendesha Mashtaka yeye, Hakimu yeye na Mtawala yeye. Afrika mambo yanakwenda kizani kama vile lilivyoitwa “Bara la Kiza.” Kundi dogo linashika majukumu ya Mfalme Juha na kuwaburuza wengi.

Kundi hili ndilo linalofaidika na sera ya kuuza kwa Shilingi Moja na kutia fedha mfukoni mwao.

Linafanya mikataba kwa siri, linauza nchi na wanyama kwa siri, linauza gesi na dhahabu kwa siri na hata akaunti zao pia ni siri.

Enzi za Mfalme Shaka Zulu, mtumishi mwaminifu zaidi wa Mfalme alizikwa pamoja na bosi wake aliyekufa. Lakini enzi hizi mambo yamezidi kuharibika.

Waziri mbadhirifu wa Afrika anastaafishwa uwaziri baada ya kuiba matrilioni ya fedha. Inafanana na kumtanguliza mtumishi mwaminifu kaburini kabla Mfalme hajafa ili siri ibaki kuwa sirini “Asiyejua maana usimwambie”.

Uchaguzi ndio huo ushapiga hodi. Ni lazima mtu mmoja mmoja ayatafakari mambo ya akina Juha na Shaka. Kama kukosea tumeshakosea vya kutosha, na sasa imetosha. Nikuulize: wewe unaona raha mtu asiye na hatia anapoumizwa? Kama sivyo, basi acha kuchagua viongozi wabovu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *