
Zanzibar. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amefanya mabadiliko ya uongozi kwa kuwateua wakurugenzi wapya wa halmashauri na manispaa 11 katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Taarifa iliyotolewa leo Mei 20, 2025 na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Said imeeleza kuwa uteuzi huo unalenga kuimarisha ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Katika uteuzi huo, Dk Mwinyi amemteua Hasna Attai Masoud kuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa ya Mjini Unguja, akichukua nafasi hiyo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Afya na Mazingira katika Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPRA).
Moh’d Simba Hassan ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Manispaa Magharibi “A”, Unguja ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Ofisa Utawala Mwandamizi wa Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS. Sabra Issa Machano ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Manispaa Magharibi “B”, Unguja.
Wengine ni Adam Abdulla Makame ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Manispaa Kaskazini “A”, Unguja, Juma Mohamed Juma Mmanga ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Jiji la Kaskazini “B”, Unguja. Dk Mwanaisha Alli Said ameteuliwa Mkurugenzi wa Baraza la Mji, Wilaya ya Kati, Unguja.
Naye Mussa Haji Mussa ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kusini, Unguja, Shuwena Hamad Ali ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Baraza la Mji, Wilaya ya Wete, Pemba na Hamad Khatib Saleh ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Micheweni, Pemba.
Pia, Shida Kombo Mohammed ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa ya Chake Chake, Pemba na Muumin Abeid Salum ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Baraza la Mji, Wilaya ya Mkoani, Pemba.
Mhandisi Zena amesema uteuzi huo unaanza rasmi leo, Mei 20, 2025.