‘Katazo matumizi fedha za kigeni, limeimarisha thamani ya Shilingi’

‘Katazo matumizi fedha za kigeni, limeimarisha thamani ya Shilingi’

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema utekelezaji wa kanuni za matumizi ya fedha za kigeni umesaidia kuimarisha thamani ya Shilingi ya Tanzania na kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni sokoni.

Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa BoT, Emmanuel Akaro ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumanne, Mei 20, 2025.

Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni, zilizotungwa chini ya Sheria ya BoT, Sura ya 197, zilichapishwa Machi 28, 2025 zikiwahusu watu binafsi na wafanyabiashara wote nchini.

Kwa mujibu wa Akaro miamala ya kila siku ya fedha za kigeni imeongezeka kwa kiwango kikubwa.

Amesema mafanikio hayo yanatokana na utekelezaji wa kanuni hizo mpya ambazo zimeongeza ukwasi na kuleta utulivu sokoni.

 “Thamani ya shilingi imeimarika,” alibainisha.

Kwa mujibu wa BoT, viwango vya ubadilishaji fedha za kigeni Mei 20, mwaka huu Dola moja ya Marekani  ilikuwa inauzwa kwa  wastani wa Sh2,685 ikiwa ni pungufu kutoka Sh2,703 hadi Sh2,730 iliyokuwa ikitumika kama gharama za kubadili Dola moja iliyokuwa ikitumika Oktoba 25 mwaka jana.

Akifafanua kwa nini Serikali imepiga marufuku matumizi ya dola za Marekani katika miamala ya ndani, amesema imechukua hatua madhubuti kudhibiti matumizi ya dola ndani ya nchi, ili kulinda thamani ya fedha za ndani na kukuza uchumi.

Katazo hilo liliwekwa katika malipo ya bidhaa, huduma na kodi za nyumba ndani ya Tanzania na badala yake zitumike fedha za ndani pekee.

“Tunafanya hivi kwa sababu watu wanapotafuta dola kwa matumizi ya ndani, huongeza mahitaji na kudhoofisha Shilingi,” alieleza. “Ndiyo maana hata ada na faini za Serikali zinapaswa kutozwa kwa Shilingi.”

Ingawa watu binafsi na wafanyabiashara bado wanaruhusiwa kuwa na akaunti za dola au kufanya miamala na watalii wa kigeni, lengo la BoT ni kuhakikisha Shilingi ya Tanzania inabaki kuwa sarafu kuu ya miamala ya ndani.

Kuhusu soko la fedha la mtaani, Akaro amesema BoT imeongeza juhudi za kulidhibiti ambapo hapo awali lilichangia kushuka kwa thamani ya Shilingi.

Kuhusu mauzo ya dhahabu kuongeza akiba ya dola, amebainisha kuwa biashara ya dhahabu inayozidi kukua inachangia pia ongezeko la upatikanaji wa dola.

“Kwa sasa tunanunua tani 4 hadi 4.5 za dhahabu kwa mwezi,” amesema.

Juni 2024, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba wakati akisoma hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2024/2025 alitangaza marufuku ya malipo ya huduma kwa kutumia fedha za kigeni kuanzia Julai Mosi 2024, huku akieleza mwongozo wa suala hilo utatolewa baadaye.

Dk Mwigulu alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizokabiliwa na upungufu wa fedha za kigeni katika mwaka 2023/24 na baadhi ya Watanzania wanakuza tatizo hilo kwa kudai au kufanya malipo ya bidhaa na huduma zinazotolewa ndani ya nchi kwa kutumia fedha za kigeni.

“Kitendo cha kuuza bidhaa au huduma za ndani kwa kutumia fedha za kigeni ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006, ambacho kinabainisha kwamba Shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali pekee kwa malipo ya ndani ya nchi,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *