Kikwete alivyobadili upepo ushindi wa Profesa Janabi

Kikwete alivyobadili upepo ushindi wa Profesa Janabi

Dar es Salaam. Ushindi wa Profesa Mohamed Janabi katika kinyang’anyiro cha nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika, si tu umeandika historia mpya kwa Tanzania, bali pia umefungua ukurasa mpya wa mafanikio ya taifa katika majukwaa ya kimataifa.

Katika ushindi huu wa kishindo, yapo mafumbo ya uongozi, diplomasia na mshikamano wa kitaifa yaliyofanikisha ndoto hiyo na kulifanya jina la Profesa Janabi kung’ara Afrika.

Kupitia uongozi wa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kama mwenyekiti wa kamati ya kampeni na msukumo wa Rais Samia Suluhu Hassan, kampeni hii si tu ilifanikiwa, bali iliweka msingi wa mafanikio ya baadaye ya Tanzania katika ulingo wa uongozi kimataifa.

Baadhi ya waliokuwa mstari wa mbele katika kampeni hii, wamefanya mahojiano na Mwananchi na kueleza mikakati mbalimbali ya ushindi iliyotumika wakati wa kampeni hiyo iliyomwezesha Profesa Janabi kuibuka mshindi kwa kishindo.

Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaalamu ya Mawaziri wa Umoja wa Afrika kutoka Liberia, Dk Louise Mopleh Kpoto, amesema Janabi ameshinda kwa kishindo baada ya nchi 32 kumchagua kati ya 46. Ili ashinde alitakiwa kupata kura 24.

Uchaguzi huo uliitishwa mara ya pili baada ya kifo cha aliyekuwa mteule wa nafasi hiyo, Dk Faustine Ndugulile, pia wa Tanzania, aliyekuwa amechaguliwa kushika nafasi hiyo Agosti 27, 2024, na kufariki dunia Novemba 27, 2025, wakati akipatiwa matibabu nchini India.

Jana Jumatatu, Mei 19, 2025, Rais Samia alisema: “Kwa dhati kabisa nimshukuru Rais mstaafu (Kikwete) nilipomwita na kumwomba awe meneja wa kampeni za Profesa Janabi, akakubali…kwenye Jakaya hakuna kushindwa, alitumia weledi wake wa diplomasia, muda wake, busara kuongoza timu ya kampeni.”

Alichosema Waziri wa Afya

Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo waliopita nchi kadhaa kumnadi mgombea huyo, amesema walitumia fursa ya Rais Samia katika kukuza diplomasia ya kimataifa na kukubalika kwake duniani kufanikisha hilo.

Pia amesema walitumia falsafa ya 4R, kwa kuwa kulikuwa na maeneo waliyolazimika kukubaliana, mengine walikubali kujenga ustahimilivu na mahala pengine walikubali kupoteza kura kwa sababu za kimkakati.

“Tulitumia faida ya ilani ya uchaguzi pamoja na vipaumbele vya awali vya uchaguzi uliopita, ambavyo viliiwezesha timu yetu ya kitaalamu kuibua vipaumbele vinavyogusa nchi nyingi kwa kuzingatia mazingira ya sasa.

“Timu ya kampeni ilikuwa na umahiri wa hali ya juu, ikiwa na uzoefu mkubwa wa kimkakati na kimbinu. Hata hivyo, kilicholeta mafanikio makubwa zaidi ni uongozi thabiti wa mwenyekiti wa timu ya kampeni, Rais mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete,” amesema Waziri Jenista.

Kuhusu mafanikio anayojivunia, amesema ni pamoja na wizara yake kufanikisha juhudi zilizoiwezesha nchi kuendelea kuimarika katika utambuzi wa kimataifa.

“Kumbuka, haikuwa kazi rahisi, tulishinda mwaka jana na tumeshinda tena mwaka huu kwa kura nyingi zaidi.

“Nimefurahi sana kwamba tumefanikisha, kwa mara nyingine tena, kuiwezesha nchi yetu kuongoza katika nafasi za juu za diplomasia ya afya,” amesema.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo akiwa pamoja na mawaziri wa afya, Mhagama (Muungano) na Nassor Mazuri (Zanzibar), waliongoza ujumbe uliokuwa na jukumu la kuimarisha uungwaji mkono kutoka kwa nchi za Afrika. 

Kombo amesema juhudi zao ziliratibiwa na Kikwete, aliyefanya kikao cha kimkakati kwa njia ya mtandao mara ili kuratibu mikakati ya mwisho ya ushawishi.

Kampeni hiyo iliendeleza msimamo wa Rais Samia wa kumtetea kiongozi wa afya kutoka Afrika mwenye maono na dhamira ya kweli. 

Amesema tangu kuzinduliwa kwa kampeni hiyo Desemba 2024, Balozi za Tanzania kote Afrika ziliwahusisha wadau, zikasisitiza umahiri wa Profesa Janabi na zikahamasisha uungwaji mkono kwa ahadi yake ya uongozi wa mabadiliko.

“Uongozi wa Profesa Janabi utafanikisha matokeo chanya katika sekta ya afya barani Afrika,” Rais Samia alisisitiza Aprili 7, 2025.

“Zaidi ya diplomasia, historia ya kazi ya Janabi inaeleza mengi. Kuanzia kuwa mshauri wakati wa mlipuko wa Ebola kati ya mwaka 2014–2016 hadi kufanikisha uwekezaji wa dola 363 milioni za Marekani kutoka Jamhuri ya Korea kwa ajili ya mifumo ya afya,” amesema Waziri Kombo.

Kampeni nchi kwa nchi

Hoyce Temu, ambaye kwa sasa ni Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu katika Mashirika ya Kimataifa Geneva, Uswisi alikuwa mjumbe wa kamati ya kampeni hiyo, akiwa miongoni mwa waliofanikisha.

Balozi Hoyce uzoefu wake kwenye kampeni nyingine, kama ile ya Dk Tulia Ackson kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), ulimpa msingi mzuri wa kushiriki kikamilifu kwenye mchakato huu.

Alianza kushiriki mara tu jina la Profesa Janabi lilipotajwa kama mgombea, ingawa hatua za awali za kampeni zilibaki za kimya kimkakati ili kuepuka ushindani wa mapema.

“Mikakati mbalimbali ilitumika kuvutia nchi wanachama wa WHO. Mkakati mkubwa uliokuwa na mafanikio makubwa ulikuwa juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alitumia ushawishi wake wa kidiplomasia kwa vitendo na kuonyesha sura nzuri ya Tanzania katika nyanja za maendeleo ya jamii, afya, elimu, mazingira na uchumi,” amesema.

Balozi Hoyce amesema kupitia vipaumbele vya Maendeleo Endelevu (SDGs) vinavyojulikana kama “5Ps”, Tanzania ilionekana kuwa mstari wa mbele, jambo lililomsaidia Profesa Janabi kupata uungwaji mkono wa kimataifa.

Ameungana na wajumbe wengine, kusema Kikwete alitumia uzoefu wake kama Waziri wa Mambo ya Nje na baadaye Rais wa Tanzania, kuendesha kampeni ya uso kwa uso na viongozi wa nchi zaidi ya 20, akiambatana na wajumbe wa kampeni.

Amesema Rais huyo mstaafu alitumia historia ya mahusiano ya kidiplomasia ya muda mrefu kati ya Tanzania na mataifa mengine, kuonyesha ushawishi wa nchi na mgombea wake.

“Kwa mfano, nchini Guinea, Kikwete alizungumzia historia ya uhusiano wa Rais Nyerere na nchi hiyo, jambo ambalo lilizua hisia chanya miongoni mwa viongozi wa mataifa hayo.

Kwa upande wake, Balozi Suleiman Haji Suleiman, Kaimu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, yeye amesema kama ambavyo alikuwa mjumbe kwenye timu ya kampeni ya Dk Ndugulile ndivyo alikuwa kwa Profesa Janabi.

Amesema alianza kampeni mara tu Rais Samia alipotangaza Profesa Janabi atakuwa mgombea wa nafasi ya WHO. Kwa hiyo kuanzia Novemba 2024: “Tulianza rasmi kazi ya kumnadi mgombea wetu.”

“Mikakati ya kumtangaza au kumnadi mgombea wetu hadi kufikia kupata ushindi mkubwa ni pamoja na kufanya mikutano ya uwili, baina yangu na mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao na kuwa mjumbe katika ya kuonana na wakuu wa nchi na Serikali zaidi ya 20 Afrika,” amesema Balozi Suleiman.

Amesema mafanikio ya kujivunia ni kuona Tanzania sasa inang’ara zaidi kimataifa na inatoa Watanzania wengi katika nafasi mbalimbali za kazi katika eneo hilo la Kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *