Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo-Bara, Isihaka Mchinjita amemtangaza Wakili Peter Madeleka kuwa mwanachama mpya aliyejiunga na chama hicho akitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Madeleka tayari amekabidhiwa kadi ya uanachama wa chama hicho pamoja na katiba ikiwa ni ishara ya kuwa mwanachama wa chama hicho.
Tukio hilo limefanyika jijini Dar es Salaam leo Mei 20, 2025 makao makuu ya chama hicho, Magomeni, huku Isihaka akimtaja Wakili Madeleka kama mpigania haki kwa wananchi wote.
Wakili huyo akizungumza baada ya kutambulishwa rasmi mbele ya vyombo vya habari, amesema uamuzi wake wa kujiunga na chama hicho umetokana na dhamira ya kutaka kuimarisha nguvu ya upinzani na kuleta matumaini kwa Watanzania kufikia malengo yao ya kisiasa na maendeleo ya kweli.

“Mapambano ya kudai demokrasia na utawala unaoheshimu haki za binadamu ni sawa na vita vingine inayohitaji mbinu tofauti na juhudi za pamoja,” amesema Madeleka.
Amesema Chama cha Mapinduzi (CCM) tayari kimeeleza dhamira yake ya kufanya uchaguzi wa uwazi, haki na huru kutokana na mageuzi ya kisiasa ambayo kimekuwa kikiyafanya kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Wakili huyo amekihama Chadema, chama ambacho kimetangaza kutoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 endapo hakutakuwa na mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi huku kikinadi kampeni yake ya “No Reforms, No Election”, na kusisitiza kuwa lengo kuu la kila mwanasiasa ni kushika madaraka ili kutekeleza sera zake.
Madeleka amesema anatarajia kugombea ubunge katika moja ya majimbo nchini, huku akiamini uchaguzi utakuwa huru na wa haki.
Amesema moja ya changamoto kubwa nchini ni ukosefu wa taasisi imara za kisiasa, kutokana na hulka ya dola ya kupinga upinzani.
“Ndiyo maana nipo ACT Wazalendo kuchangia katika kuimarisha nguvu ya upinzani na kuleta matumaini kwa wananchi. Mapambano haya ya kisiasa yanahitaji mbinu nyingi. Huwezi kuweka matumaini yote kwa chama kimoja au njia moja,” amesema.
Amesema baadhi ya vyama vitaamua kushiriki uchaguzi huku vingine vikisusia na zote ni njia halali, lakini anaamini ushiriki wa ACT Wazalendo utaleta mafanikio makubwa kwa Taifa.

“Kwa kuzingatia hatua mbalimbali zilizochukuliwa na makundi ya kijamii kushinikiza uchaguzi huru na kwa kuwa CCM imetangaza mageuzi, ni muhimu kushiriki uchaguzi huu ili kuthibitisha iwapo kweli kuna mabadiliko au la,” amesema Madekeka.
Mchinjita, ndiye alimpokea rasmi Wakili Madeleka na kumkabidhi kadi ya heshima inayohusishwa na hayati Maalim Seif Sharif Hamad, huku akimtaja kuwa ni mwanaharakati shupavu na mtetezi wa haki za binadamu.
“Wote tunatambua uwezo wa Wakili Madeleka, ni maarufu, shujaa wa haki za kiraia na amekuwa akihimiza demokrasia kwa muda mrefu. Ni miongoni mwa wadau waliokuwa bega kwa bega na chama hiki kwa kipindi kirefu,” amesema Mchinjita.
Amesema Madeleka alikuwa sauti ya wananchi katika kipindi cha utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne, akiitetea jamii katika masuala nyeti ikiwa ni pamoja na kesi za ugaidi zilizohusisha baadhi ya masheikh waliokamatwa na kushikiliwa kwa muda mrefu.
Mchinjita pia alitolea mfano wa mchango wa Madeleka katika kesi iliyomhusisha aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Paul Gekul.
Aidha, ACT Wazalendo imewataka wananchi na wanaharakati wote wenye dhamira ya kulitumikia Taifa kujiunga na chama hicho.