‘Ujenzi uwanja wa ndege Pemba, kuimarisha utalii wa kimataifa’

‘Ujenzi uwanja wa ndege Pemba, kuimarisha utalii wa kimataifa’

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  (SMZ) imeanza rasmi ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba, mradi unaotajwa kuwa chachu ya maendeleo kwa kisiwa hicho ukielezwa utafungua zaidi fursa za kiuchumi, kitalii na kijamii.

Baada ya kukamilika, uwanja huo utawezesha ndege kubwa kutua moja kwa moja kisiwani humo, tofauti na hali ya sasa ambapo abiria hulazimika kutua kwanza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume uliopo Unguja, kisha kusafiri kwa ndege ndogo au boti kuelekea Pemba.

Akizungumza leo Mei 20, 2025, katika kikao cha Baraza la Wawakilishi, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Nadir Abdulatif amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo ulianza rasmi Novemba 2024.

Kwa mujibu wa Abdulatif uwanja huo mpya ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga na kukuza shughuli za kiuchumi kisiwani Pemba, ikiwemo utalii wa kimataifa ambao kwa muda mrefu umekuwa ukikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa usafiri wa moja kwa moja.

“Mradi huu utaleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya usafiri wa anga kisiwani Pemba na kuwa kichocheo cha maendeleo ya sekta nyingine kama utalii, biashara na uwekezaji.

“Mkandarasi anakamilisha ujenzi wa kambi yake ili aanze kuleta vifaa vya ujenzi vitakavyotumika katika kazi za ujenzi wa uwanja,” amesema.

Amesema msimamizi wa ujenzi ni kampuni ya Dar al Handasah Consultants (Shair And Partners).

Abdulatif amesema hayo wakati akijibu swali la mwakilishi nafasi za wanawake, Chumu Kombo Khamis aliyetaka kujua mpango wa Serikali kuendeleza ujenzi wa viwanja vya ndege kisiwani Pemba.

Akijibu swali hilo, Abdulatif amesema mkataba wa ujenzi wa uwanja huo  ulisainiwa Januari 4, 2023 baina ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na Kampuni ya Propav Infrastructures, Ikulu Unguja ukishuhudiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Amesema lengo la Serikali ni kuimarisha uwanja wa ndege wa Pemba kwa kuongeza urefu wa barabara ya kutua na kurukia ndege, kujenga jengo jipya la abiria na miundombinu husika itakayowezesha uwanja huo kutua ndege aina ya Code C (Boeing 737-800) na zinazolingana na hiyo.

Ujenzi wa mradi wa uwanja wa ndege wa Pemba unajengwa kwa fedha za mkopo kutoka United Kingdom Export Finance (UKEF) kwa gharama ya Euro milioni 170 (Sh516.73 bilioni).

Hata hivyo, ujenzi huo ulisuasua kuanza kutokana na kampuni mbili ambazo zilikuwa na ubia kuingia mgogoro mpaka kupelekana mahakamani. Kampuni hizo ni Propav ya nchini Brazil na Mecco ya Tanzania.

Januari 10, 2024 Mahakama Kuu ya Zanzibar ilitoa amri za muda kusimamisha maendeleo ya mradi kusubiri utatuzi wa mgogoro wa kisheria kati ya kampuni hizo mbili.

Hata hivyo, amesema  baadaye kampuni hizo mbili zilifikia muafaka na kukubaliana  nje ya Mahakama uwanja huo ujengwe na Propav ya nchini Brazil kama walivyokuwa wamefanya makubaliano Aprili 18, 2024.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *