Mwanza. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kulizindua rasmi Daraja la JP Magufuli (Kigongo-Busisi) jijini Mwanza, Juni 19, 2025.
Waziri Ulega ameyasema hayo jana Jumatatu, Mei 19, 2025 katika mkutano wa hadhara wilayani Sengerema mkoani Mwanza ambao ulikuwa wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Amewataka wananchi wa Mwanza kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa daraja hilo lenye urefu wa kilomita tatu na barabara zake unganishi zenye urefu wa kilomita 1.66 na linalotarajiwa kuwa refu kuliko yote katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.
Ulega amesema kukamilika kwa daraja hilo ni mafanikio ya maono na jitihada kubwa zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan na mtangulizi wake, hayati John Magufuli.
“Namna pekee ya kuonyesha furaha yetu na shukurani zetu kwa mafanikio hayo ni kwenu wananchi wa Sengerema, Mkoa wa Mwanza, Geita, mikoa yote ya kanda ya ziwa na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi huo,” amesema waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Mkuranga.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi katika tukio hilo.
“Jitayarisheni kwa wingi kumpokea kiongozi wetu mkuu atakapokuja kulifungua daraja hili Juni 19, 2025,” amesema Majaliwa.

Muonekano wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo-Busisi).
Ziara ya Majaliwa mkoani Mwanza ni ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo Ulega alitumia mkutano wa Sengerema kumweleza (Majaliwa) juu ya kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha huduma za usafiri na uchukuzi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa ujumla.
“Watu waliokuwa wanasafiri kwa zaidi ya saa mbili watakwenda kusafiri kwa wastani wa dakika tatu hadi tano, tunamshukuru Rais kwa maono na maelekezo yake,” amesema.
Amesema zaidi ya Sh700 bilioni zimetumika katika ujenzi wa daraja hilo linalounganisha mji wa Kigongo na Busisi katika Ziwa Victoria ambalo ni la tatu kwa ukubwa duniani.
Aidha, Waziri Ulega amewahakikishia wakazi wa Wilaya ya Sengerema kuhusu ujenzi wa barabara Segerema – Nyehunge (yenye kilomita 54.5) na Kamanga – Sengerema (kilomita 32) kwa kiwango cha lami. “Serikali ipo katika hatua za mwisho za kumkabidhi mkandarasi kazi ya ujenzi huo.”