Mpanda kicheko, umeme gridi ya Taifa kuwafikia Juni

Mpanda kicheko, umeme gridi ya Taifa kuwafikia Juni

Tabora. Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Kusafirisha na Kusambaza Umeme (ETDCO), Raymond Mbilinyi amesema mpaka kufikia mwisho mwa Juni mwaka huu, umeme kutoka kwenye gridi ya Taifa utakuwa umefika wilayani Mpanda, Mkoa wa Katavi.

Akizungumza akiwa mkoani Tabora leo Jumanne Mei 20, 2025 wakati wa ziara ya ukaguzi wa mradi huo, Mbilinyi amesema maendeleo ya mradi yanaridhisha na bodi ya wakurugenzi imeridhishwa na usimamizi wake.

Amesemamradi utasafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 kutoka mkoani Tabora hadi Mkoa wa Katavi.

 “Tumeridhishwa na maendeleo ya mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Katavi, kwa sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 96” amesema Mbilinyi.

Awali akizungumzia mradi huo, Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Sadock Mugendi aliieleza bodi hiyo kuwa ujenzi wa mradi huo unaendelea vizuri na sasa upo hatua za mwisho za ukaguzi wa laini.

Amewahakikishia wajumbe hao wa bodi kuwa mpaka kufikia mwishoni mwa Juni 2025, mradi utakuwa umekamilika kwa asilimia 100 na kufikisha umeme Mkoani Katavi.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) Kanda ya Magharibi, Mhandisi Richard Swai amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Tabora na Katavi.

Mhandisi huyo amewataka wananchi wa mikoa hiyo kujiandaa kupokea umeme wa gridi ya Taifa, ambao utachochea shughuli za kiuchumi na maendeleo kupitia sekta mbalimbali kama kilimo, viwanda, usindikaji na uongezaji thamani wa mazao.

Akizungumzia hali ya upatikanaji wa umeme mkoani Tabora, Julius Shite, mkazi wa Tabora amesema kukamilika kwa mradi huo kutawapatia ahueni kubwa.

“Kama tulivyosikia, Tabora na Wilaya ya Mpanda sasa tunakwenda kupata umeme wa uhakika, kilio cha kukatikakatika sasa basi, niipongeze Tanesco kwa jitihada hizi kubwa,” amesema Shite.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *