Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema taifa, aliingia kwenye chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akiwa na mpango tayari. Bila shaka alishakuwa na taarifa kichwani ya uwepo wa watu waliofika kumtembelea.
Alivaa fulani yenye kola (form six), rangi nyeupe na bluu (rangi za Chadema). Kifuani upande wa kulia, kuna maandishi ya jina lake, “Mh Lissu”, kushoto nembo rasmi ya Chadema, tumboni imeandikwa “No Reforms, No Election”. Ni Mei 19, 2025.
Lissu baada ya kuingia chumba cha mahakama, anasalimiana na viongozi mbalimbali wa Chadema, pamoja na watu wengine mashuhuri waliofika mahakamani. Alichanua tabasamu kuonesha yupo imara, kwa hiyo wafuasi wake wasiwe na hofu.

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akisalimiana na Jaji mstaafu wa Kenya, David Maraga.
Kesi inayomkabili Lissu ni uhaini. Matamshi yake ya kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu 2025, ndiyo yamemwingiza matatizoni. Chadema wapo kwenye azimio lao la “No Reforms, No Election”, yaani bila mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi, hakutakuwa na uchaguzi.
Watu kwenye matatizo hufariji na kuongeza nishati. Hata pale aliye matatizoni anaposhuka chini au kuishiwa nguvu, anapoona watu, nishati hupata chaji mpya. Lissu alipoona watu mahakamani, alijiona salama, na kama kiongozi, aliona wajibu wa kuwatia moyo wafuasi wake.
Mwandishi mashuhuri wa Uingereza, William Shakespeare, aliandika: “A friend ni the court is better than a penny in purse.” Alimaanisha kuwa rafiki anayeambatana nawe mahakamani ni bora kuliko fedha kwenye pochi.
Maneno hayo ya Shakespeare, yatakupa mantiki ya uimara wa Lissu mahakamani Kisutu. Ni sababu ya kumtaja mmoja baada ya mwingine kwa jina na kumshukuru, kumpongeza, vilevile kumtia moyo. Alichofanya Lissu ndiyo kile ambacho huitwa siasa za mahakama (court politics). Kutumia fursa za ushindani wa kisheria kufanya siasa kwenye chemba na viunga vya mahakama. Lissu aliingia mahakamani kushindana kisiasa kuliko kisheria.
Ni kawaida kwa wanasiasa kufanya siasa za mahakama. Kenya, hufanya mara kwa mara. Venezuela, kuna wakati njia zote za ufanyaji siasa kwa vyama vya upinzani zilifungwa, mahakama zikageuzwa majukwaa ya kisiasa.

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akisalimiana na John Heche ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bara.
Siasa za mahakama ni maonesho ya ushindani wa muda mfupi. Watu wengine hutazama kama filamu ya mashindano, na hufuatilia kwa shauku ya nani atashinda. Katu, siasa za mahakama hazijawahi kutoa matokeo ya moja kwa moja.
Kiongozi wa upinzani Kenya, Raila Odinga, amefanya sana mashindano ya kisiasa kwenye vyumba vya mahakama. Ameshinda mara nyingi, pia ameangushwa mara kwa mara. Matokeo ya kimahakama hayajawahi kujenga athari ya kisiasa moja kwa moja.
Raila hajawahi kushinda kiti cha urais kwa sababu alichanga karata nzuri kwenye siasa za mahakama. Hajawahi kuonekana kupoteza mvuto, kwa kuwa alishindwa mahakamani. Ni sinema ya maonesho isiyo na matokeo ya moja kwa moja.
Rais Nicolas Maduro, ameendelea kukaa madarakani Venezuela, licha ya wapinzani wake kutia fora kwa siasa za mahakama. Haina maana wanasiasa wasiitumie fursa ya kufanya siasa mahakamani, bali wajitahidi kuzingatia maeneo yenye mtaji halisi.
Mazingira yameonesha kuwa majukwaa ya kisiasa na usukaji mtandao wa vyama kushuka chini, hadi mashina na matawi, ni mtaji muhimu wa kujenga chama na wanasiasa. Matokeo kwenye uchaguzi huakisi ujenzi wa aina hiyo.

Polisi wakiwa katika majukumu ya kuimarisha ulinzi katika eneo la Mahakama ya Hakimu Kisutu.
Huu ni mwaka wa uchaguzi. Chama cha siasa hupaswa kwenda kwa wananchi. Chadema, kupitia No Reforms, No Election, wapo kwenye utata mkubwa wa kushiriki uchaguzi. Hadi sasa, kanuni zimeshawatoa nje ya mchezo kwa sababu chama hicho hakikusaini fomu ya maadili ya uchaguzi kutoka Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).
Wapo watu wanaamini Lissu anaongeza umaarufu na ufuasi kwa kuwepo kwake mahabusu na tamthiliya zake za kimahakama. Swali ni moja, umaarufu huo una faida gani ikiwa chama chake hakitashiriki uchaguzi na yeye mwenyewe hatagombea?
Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020, Chadema walifanya siasa za mahakama kwa ubora wa hali ya juu. Ghafla, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam, iligeuka jukwaa la maonesho ya kisiasa kati ya CCM na Chadema, ambao waliungwa mkono waziwazi na ACT-Wazalendo pamoja na NCCR-Mageuzi.
Viongozi wa juu wa Chadema, wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti, Freeman Mbowe, walikuwa wakikabiliwa na kesi ya uchochezi na kusababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.
Washitakiwa wengine walikuwa John Mnyika, Katibu Mkuu, Salum Mwalimu, alikuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Halima Mdee, Mwenyekiti Baraza la Wanawake (Bawacha), Esther Matiko, Mwenyekiti Chadema Kanda ya Serengeti na mbunge wa Tarime Mjini.
Peter Msigwa, aliyekuwa Mwenyekiti Chadema Kanda ya Nyasa na Mbunge wa Iringa Mjini, Ester Bulaya, alikuwa Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Bunda Mjini, vilevile John Heche, alikuwa Mbunge wa Tarime Vijijini na Mjumbe wa Kamati Kuu. Heche, kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti Chadema, Tanzania Bara.
Katika orodha ya washitakiwa, alikuwepo pia aliyekuwa Katibu Mkuu Chadema, Vincent Mashinji, ambaye alihamia CCM mwaka 2020. Wote kwa pamoja, walikutwa na hatia katika makosa 12 kati ya 13 waliyoshitakiwa, hivyo kuhukumiwa kulipa faini jumla ya Sh350 milioni au kwenda jela miezi mitano kila mmoja.
Sasa, Chadema walianza kuchangisha michango ya kuwalipia faini viongozi wao. Ndani ya saa 8 walifikisha Sh108 milioni. Zilipotimu saa 16 tangu kuanza michango, taarifa za Chadema zilitaja makusanyo kufikia Sh234 milioni. Kasi ya uchangishaji ikawa kubwa na uitikio ni wa juu.
Kasi kubwa ya ukusanyaji michango kwa ajili ya kuwalipia faini viongozi wa Chadema, ilionesha ni kiasi gani chama hicho kilikuwa na ufuasi mpana na ulio hai, vilevile hukumu dhidi yao ilivyogusa watu wengi. Ilidhihirika kuwa viongozi wa Chadema wapo upande wa kushoto kwenye vifua vya wengi, kwani marafiki wa mahakamani ni bora kuliko pesa ndani ya pochi.
Pamoja na karata hizo za mahakamani, Uchaguzi Mkuu 2020, haukuwa na matokeo bora kwa Chadema. Siasa haziendeshwi kama tamthiliya. Bali maarifa yenye uwanda mpana. Mageuzi ya kisiasa yataletwa na siasa za wananchi kuliko za kimahakama. Mbowe alishinda sana siasa za mahakama, lakini chama hakikupata dola.
Kesi ya ugaidi na kunyimwa dhamana kwa kesi ya uchochezi, kisha mapambano ya kimahakama kutoka Mahakama ya Kisutu hadi Mahakama Kuu; Mbowe aliifanya Chadema kushinda mahakamani, lakini siyo uchaguzi. Lissu anarejea njia ileile.