Roma, Italia. Kocha wa zamani wa Liverpool, Jurgen Klopp ametajwa kuwa anaweza kujiunga na AS Roma mwishoni mwa msimu huu, huku wakala wake akikanusha.

Klopp ni mmoja kati ya makocha wenye mafanikio makubwa kwenye kikosi cha Liverpool akiwa aliiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la FA, Ngao ya Jamii na Klabu Bingwa Dunia kwa kipindi alichokaa kwenye klabu hiyo.
Mara baada ya kuachana na timu hiyo aliyodumu nayo kwa miaka tisa, Klopp alisema anataka muda mwingi wa kupumzika na familia yake.
Taarifa iliyosambaa kuanzia juzi Jumatatu, imesema kuwa mwishoni mwa msimu huu kocha huyo raia wa Ujerumani atajiunga na Roma ya nchini humo.

Kwa mujibu wa gazeti la La Stampa, limesema kuwa kocha huyo amekubali kujiunga na timu hiyo ya zamani ambayo iliwahi kufundishwa na Jose Mourinho, ili kuchukua nafasi ya mkongwe Claudio Ranieri ambaye atastaafu mwishoni mwa msimu huu.
Taarifa hiyo ilisema kuwa Klopp tayari ameshafanya mazungumzo na mkurugenzi wa michezo wa timu hiyo Florent Ghisolfi, na wameshakubaliana kila kitu muhimu.

Taarifa hiyo imesema kuwa Mjerumani huyo ameutaka uongozi wa timu hiyo kufanya usajili wa mastaa sita wakubwa jambo ambalo limekubaliwa.
Wakati tetesi hizi zikisema hivyo, Wakala wake Marc Kosicke, amesema jambo hilo siyo la kweli.
“Klopp kuifundisha Roma?” jambo hilo siyo la kweli.”
“Kama kungekuwa na jambo hilo wala nisingeshindwa kusema ukweli, lakini nataka kuwahakikishia kuwa hakuna hicho kitu,” alisema.