
Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto umejikita katika kumaliza ukatili ukijumuisha kubakwa na kupewa mimba kwa kuzini na maharimu au ndugu na jamaa wa karibu ikiwemo baba wa kuwazaa.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis ameyasema hayo leo Jumanne, Mei 20, 2025 wakati akijibu swali Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Fatma Toufiq.
Mbunge huyo amehoji Serikali inatoa tamko gani kuhusu wasichana waliopata mimba kutokana na kubakwa na wanaopewa mimba na baba zao na ndugu wa karibu.
Akijibu swali hilo, Mwanaidi amesema ubakaji ni kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sheria ya Mtoto pamoja na sheria nyingine zinazopinga ukatili kwa watoto.
Amesema Serikali kupitia wizara tunayoisimamia inakemea tabia ya ubakaji na ulawiti wa watoto.
“Pamoja na matamko na hatua za kisheria ambazo zimekuwa zikichukuliwa, Serikali imeendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto Awamu ya Pili wa mwaka 2024/2025 hadi 2028/2029,” amesema.
Mwanaidi amesema mpango huo umejikita katika kumaliza ukatili ukijumuisha kubakwa na kupewa mimba kwa kuzini na maharimu au ndugu na jamaa wa karibu ikiwemo baba wa kuwazaa.
Katika swali la nyongeza, Fatma amesema baadhi waathirika wamekuwa wakijaribu kutoa mimba baada ya kupewa mimba na maharimu yao na hivyo kugharimu maisha yao na kuhoji Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na jambo hilo.
“Je Serikali inawasaidiaje wahanga wa ukatili wa kupewa mimba na maharimu wao na familia zao zimekuwa zikiwatenga,”amehoji.
Akijibu swali hilo, Mwanaidi amesema Serikali inatoa kauli kali kwa wale wote wanaopata mimba na kuzitoa kwa sababu utoaji mimba ni kosa la jinai.
“Serikali itaendelea kutoa elimu ikiwemo maofisa wa jamii, kuwaelimisha wahanga wote waliopata na changamoto za kupata mimba ili waweze kuondokana na msongo wa mawazo na kupata huduma stahiki,” amesema.
Amesema Serikali imeendelea kutoa huduma kupitia nyumba salama kwa wasichana ambao wametelekezwa na familia zao.
Mwanaidi amesema wameendelea kutoa huduma za afya na huduma za msaada wa kisheria zimekuwa zikitolewa kwa waathirika wa ukatili huo ili kuhakikisha wanakaa salama na kuondokana na msongo.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Maryam Azan Mwinyi amesema watoto wengi wanaopata mimba za utotoni ni wale wa mitaani na kuhoji Serikali ina mkakati gani wa kuwalinda watoto hao.
Akijibu swali hilo, Mwanaidi amesema Serikali ina mkakati wa kuwafuata mtaani, kuwahoji na baada ya kuwahoji wanawakutanisha na wazazi wao ili waendelee na maisha.
“Na Serikali inaposhindwa basi Serikali ina vituo vyetu vya kulelea watoto, vipo Dodoma na Dar es Salaam ambapo watoto wanalelewa na kupata stahiki za elimu hadi wanapokua na wametimiza miaka 18 na kuendelea na maisha yao,” amesema.