Bandari bubu janga kwa afya za Watanzania -2

Bandari bubu janga kwa afya za Watanzania -2

Dar/Mikoani. Serikali inaendelea kukuna kichwa kutokana na ongezeko la magonjwa yasiyokuambukiza nchini, huku sababu mbalimbali zikitajwa ikiwamo mtindo wa maisha na vyakula.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wameonya juu ya tishio jipya la matumizi ya vyakula visivyo na ubora vinavyopitishwa kinyemela katika bandari zisizo rasmi (bandari bubu).

Takwimu za Wizara ya Afya kupitia Mfumo wa Taarifa za Utoaji wa Huduma za Afya (Mtuha) zinaonyesha idadi ya wagonjwa wapya wa saratani inaongezeka kila mwaka kutoka wagonjwa 33,484 mwaka 2019 mpaka 49,215 mwaka 2023.

Mbali ya hayo, takwimu za wanaohudhuria vituo vya afya kutokana na shinikizo la damu limeongezeka kutoka 1,112,704 mwaka 2019 hadi 1,482,911 mwaka 2023.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa zaidi ya miezi miwili umebaini kuwa bandari bubu zilizopo kinyume cha Sheria ya Bandari Namba 17 ya mwaka 2004 ni kinara wa kupitisha bidhaa ambazo ubora wake haujathibitishwa kitaalamu.

Katika uchunguzi huo uliofanywa katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Lindi, bidhaa zinazoingizwa kinyemela kwa wingi ni sukari, vipodozi na mafuta ya kupikia vikitoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Akizungumzia ubora wa bidhaa za vyakula hasa zinazoingia kinyemela na athari zake, daktari wa binadamu, Zainabu Abdul anasema nyingi husababisha magonjwa ya moyo, saratani na kiharusi kwa sababu hazijafanyiwa uchunguzi wa ubora.

“Mafuta yanayoingizwa kiholela hayana uthibitisho wa usalama wa kiafya. Mara nyingi yanakuwa yamechakachuliwa au yamekwisha muda wake wa matumizi, hali inayoongeza uwezekano wa sumu za ukungu (aflatoxins) ambazo husababisha saratani ya ini,” anasema.

Dk Zainabu anasema mafuta ya kupikia yasiyo na ubora mara nyingi huwa na viwango vya juu vya asidi mafuta zenye madhara (trans fats), ambavyo huchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la magonjwa ya moyo na kiharusi.

“Pia matumizi ya mafuta haya kwa muda mrefu yanaweza kusababisha unene uliokithiri, kisukari aina ya pili na matatizo ya usagaji wa chakula,” anasema.

Kuhusu athari za vipodozi kiafya, daktari wa binadamu, Edgar Rutaigwa anasema vingi vinavyoingia nchini kwa njia ya magendo huwa na viambato hatari katika afya na ngozi.

“Vipodozi hivi vinaweza kusababisha kuwashwa ngozi, vipele, ngozi kuwa nyembamba kupita kiasi na hata saratani ya ngozi. Pia, zebaki inapoingia mwilini inaweza kuharibu figo na kusababisha matatizo ya mfumo wa neva,” anasema.

Dk Rutaigwa anaonya kuwa vipodozi vyenye viambato vyenye kemikali kali vinaweza kuvuruga mfumo wa homoni na kusababisha matatizo ya uzazi kwa wanawake na wanaume.

TBS yataja mikakati

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dk Ashura Katunzi amesema wanaendelea kupambana na bidhaa zisizo na ubora sokoni ambazo nyingi huingia kwa njia ya magendo.

“Mwaka wa fedha uliopita tulitoa bidhaa ambazo hazina ubora sokoni zenye thamani ya Sh1.6 bilioni na kuziteketeza. Wakati huo tukihakikisha biashara inaendelea,” amesema Dk Ashura.

Kuhusu mikakati ya kuzuia bidhaa hizo Dk Ashura amesema: “Ili kuzuia uingizwaji wa bidhaa hizo tunaendelea kuboresha mifumo ya Tehama.

“Tupo katika hatua ya kuona bidhaa zinazoingia ndani ya nchi ubora wake katika tovuti yetu na mitandao yetu tunaweka pale ambazo hazitakiwi kutumika kabisa.”

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2024/2025 alisema ili kupambana na bidhaa feki na za magendo kutakuwa na ufuatiliaji wa mara kwa mara wa stempu za kodi za kieletroniki.

“Takwa hili litaenda sambamba na ukaguzi utakaokuwa ukifanyika mara kwa mara ili kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa zinawekwa stempu za kielektroniki na kulipiwa kodi stahiki.

Bidhaa nyingine ndogo ndogo ambazo zimesafirishwa kwa njia ya boti.

“Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani dhidi ya biashara ya bidhaa feki sokoni, kuboresha usimamizi wa ukusanyaji wa ushuru wa bidhaa na kuzuia upotevu wa mapato ya Serikali,” alisema Dk Mwigulu.

Athari kwa wananchi

Wakazi wawili kutoka maeneo tofauti ya Tanzania, mmoja kutoka Mbweni jijini Dar es Salaam na mwingine kutoka Lindi, wanasema walijikuta wakipambana na matatizo ya kiafya baada ya kutumia mafuta ya kula yasiyo na ubora, hali inayoibua wasiwasi kuhusu usalama wa bidhaa hiyo sokoni.

Mariam Mshamu, mama wa watoto watatu mkazi wa Mbweni, jijini Dar es Salaam, anasema alianza kutumia mafuta hayo baada ya kuyapata kwa bei nafuu sokoni, akidhani ni fursa ya kuokoa pesa.

“Nilinunua lita tano kwa Sh14,000 tu (uhalisia huuzwa kati ya Sh24,000 hadi Sh30,000), nikiwa na matumaini kwamba ningetumia kwa muda mrefu. Siku chache baada ya kuanza kuyatumia, nilianza kuhisi kichefuchefu na maumivu ya tumbo yasiyoisha,” anasimulia.

Mariam anasema baada ya vipimo iligundulika alikula sumu kutoka kwenye chakula, ambayo walihusisha moja kwa moja na mafuta aliyotumia.

“Nilishangaa waliponiambia kuwa mafuta niliyotumia hayakuwa salama. Waliagiza nipeleke kwa ajili ya uchunguzi wa maabara,” anasimulia.

Bidhaa ambazo hazikutambulika kwa haraka ambazo zimeshushwa kwenye bandari bubu ya Kilwa Kivinje na kisha kuhifadhiwa kwenye nyumba zilizopo katika mwambao wa bahari.

Kwa upande wake, Suleiman Bushiri, mkazi wa Kilwa Kisiwani, mkoani Lindi ambaye ni muuza chipsi anasema alipata madhara pamoja na wateja wake baada ya kutumia mafuta aliyoyapata kwa magendo mwaka 2023.

“Nilipata mafuta kutoka kwa wauzaji wa jumla yaliyoletwa kwenye hizi bandari za uchochoroni, walidai wanauza kwa bei ya ofa. Siku ya pili tu baada ya kuyatumia, wateja watatu walilalamika kuhisi vibaya baada ya kula chipsi zangu,” anasimulia.

Bushiri anasema baadaye alianza kupata matatizo ya ngozi na kuvimba mdomo, hali iliyomlazimu kufunga biashara kwa wiki nzima.

“Nilikwenda hospitali, wakaniambia ni athari za kemikali isiyo salama. Nilihisi yatakuwa ni yale mafuta, sikuyatumia tena na nimekuwa balozi mzuri wa kukataa bidhaa hizi za magendo,” anasema.

Suala la kiusalama

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Seleman Jafo alipoulizwa kuhusu changamoto ya bandari bubu amesema jambo hilo ni mtambuka si tu athari za kibiashara bali ni usalama wa nchi kutokana na watu kukimbilia kununua bidhaa zinazoingia kimagendo ambazo hazijathibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

“Biashara hiyo inahusisha masuala ya usalama wa nchi, hivyo kuna haja ya kukaa kikao cha pamoja kujadiliana namna ya kukabiliana na tatizo hilo, kwani linatishia usalama wa wananchi kwa kuingizwa vitu kinyemelea ambavyo vinaweza kuwadhuru kiafya,” amesema.

Ofisa Habari Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Leonard Magomba anasema kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wanafanya kazi ya kudhibiti biashara ya magendo.

“Awali hakukuwa na udhibiti wa masuala ya kiusalama kwa hiyo wengi wao walikuwa wanatumia mwanya huo kupitisha biashara zao za magendo,” anasema.

Imeandikwa kwa ufadhili wa Gates Foundatio

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *