
Iringa. Mkoa wa Iringa umekumbwa na ongezeko kubwa la bei ya nyanya, hali inayowaelemea wananchi na wafanyabiashara ambapo awali, wananchi wanasema kuwa walinunua nyanya kwa bei nafuu, lakini sasa bei imepanda maradufu.
Bei ya tenga moja la nyanya lililokuwa linauzwa kati ya Sh20,000 hadi Sh25,000 sasa linauzwa kati ya Sh48,000 hadi Sh50,000.
Wakulima wameeleza kuwa pamoja na miezi kama hii nyanya huwa zinapanda bei, lakini mwaka huu hali imezidi kuwa mbaya, kwani mwaka jana zilipanda hadi kufikia Sh20,000 mpaka Sh30,000 kwa tenga moja.
Wananchi wa Iringa wanalalamikia hali hii, wakisema kuwa awali fungu moja la nyanya lenye nyanya tano mpaka 10 liliuzwa kuanzia Sh200 hadi Sh300, lakini sasa bei imepanda hadi kuanzia Sh500 kwa fungu lenye nyanya tatu mpaka nne zenye ukubwa tofauti.
”Hizi nyanya zimekuwa kama dhahabu siku hizi. Wiki iliyopita nilinunua kilo moja kwa Sh200, leo ni Sh500. Hali ni ngumu sana, hasa sisi wa kipato cha chini,” amesema Neema Malimbula mkazi wa mkoani humo.
”Hata chakula cha kawaida sasa kinakuwa gharama. Mama ntilie anasema bei ya nyanya imepanda, hivyo na gharama ya wali maharage inapanda pia. Tunateseka sisi wananchi wa kawaida,” amesema Jackson Mbinda mkazi wa halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Sababu za kupanda kwa bei
Wafanyabiashara wameeleza kuwa kupanda kwa bei kunatokana na uzalishaji mdogo wa nyanya baada ya wakulima wengi kukata tamaa kutokana na hasara walizopata mwaka uliopita.
Lakini pia mfanyabiashara wa nyanya kutoka soko kuu la Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Emmanuel Tishu amesema kuwa sababu nyingine ya bei kupanda ni kutokana na mvua nyingi zilizonyesha, baadhi ya sehemu ambako nyanya ndio hutokea ikiwemo Morogoro na Arusha.
”Kiukweli bei ya nyanya kwa sasa hivi inatuumiza wafanyabiashara na wateja wetu lakini wenzetu wakulima bei hii ni kicheko kwao,” amesema Tishu.
Katika hatua nyingine mfanyabiashara Joshua Mnyika kutoka Soko la Mlandege halmashauri ya Manispaa ya Iringa ameeleza kuwa baadhi ya maeneo mkoani Iringa ambayo hulima nyanya ikiwemo Ilula na Kalenga wamekosa nyanya baada ya mvua zilizonyesha kuharibu zao hilo, hivyo nao wamejikuta wakifuata mzigo huo katika masoko ya mijini baada ya kutoka mikoa mbalimbali.
”Bei ya nyanya kwa sasa inatokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni mfano mikoa kama Arusha na Morogoro wafanyabiashara tulikuwa tunaagiza nyanya huko lakini sasa hivi wanatuambia zimesombwa na maji,” amesema Mnyika na kuongeza kuwa,
”Kutokana na hali hii Wafanyabiashara tumejikuta tukishindwa kulikimbia soko hivyo tunapambana na hali halisi,”
Walichosema wakulima
Wakulima wa nyanya mkoani Iringa wamesema kuwa wanafurahia kupanda kwa bei hiyo, wakisema kuwa imefuta kilio cha bei ndogo walichokipata mwaka jana na miezi ya hivi karibuni.
Mkulima wa nyanya kutoka Kalenga Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Ramadhani Ibrahim amesema kuwa kupanda kwa bei ya zao hilo ni fursa kwa wakulima na wao wanaendelea kuzalisha kwa wingi ili wamudu mahitaji ya soko.
”Soko la nyanya kwa sasa tumelifurahia kwa kiasi kikubwa maana miezi iliyopita tulikuwa tunalima kwa hasara lakini sasa hivi si haba,” amesema Ibrahim.
Changamoto za usafirishaji
Asia Mbata mmoja wa wafanyabiashara wa nyanya kutoka mkoani Iringa ambaye hufuata nyanya kutoka sehemu tofautitofauti nchini ameeleza kuwa mvua zimeharibu miundombinu ya barabara, na kufanya iwe vigumu kusafirisha bidhaa kutoka mashambani hadi sokoni.
”Tunajua kuwa wakulima wengi wa nyanya wanapatikana vijijini ambako sehemu nyingi barabara zake ni za vumbi hivyo baada ya mvua barabara hizo imekuwa ni changamoto kupitika,” amesema Mbata.
Wadudu waharibifu watajwa
Baadhi ya wakulima kutokea mkoani Iringa pia wamesema kuwa katika kilimo cha nyanya wanachokifanya kinakabiliwa na changamoto ya wadudu waharibifu kama tomato leaf miner (Tuta absoluta) ambao wameathiri uzalishaji wa nyanya.
Mwananchi Digital imezungumza na Ofisa kilimo wa Wilaya ya Iringa, Daniel Mlay ambaye amesema kuwa ni kweli bei ya bidhaa hiyo imekuwa tofauti na ya hivi karibuni ambapo imefikia ni Sh48,000 hadi Sh50,000 kutoka Sh20 000 mpaka Sh25,000 kwa tenga moja.
Mlay ameeleza kuwa kupanda kwa bei ya nyanya katika mkoa huo kunatokana na kuongezeka kwa mahitaji ya zao hilo katika masoko mbalimbali, hasa yale ya nje ya mkoa.
Pia amesema kuwa hali hiyo imechangiwa na uzalishaji mdogo wa nyanya kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, hususani mvua zisizotabirika ambazo zimeathiri mavuno ya wakulima.
”Kupanda kwa bei ya nyanya kumechangiwa na kuongezeka kwa mahitaji ya soko, hasa nje ya mkoa, huku uzalishaji ukiwa mdogo kutokana na mvua zisizotabirika,” amesema Mlay.
Ameongeza kuwa wakulima wengi walikumbwa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa, ambapo mvua zilikuwa tofauti na matarajio yao, hali iliyosababisha mavuno kuwa chini ya kiwango kilichotarajiwa.
”Mvua za mwaka huu zimekuwa tofauti na matarajio ya wakulima wengi, hivyo kusababisha wakulima kuvuna mazao tofauti na walivyotarajia,” amesema Mlay.
Aidha, Mlay amewashauri wakulima kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo na kutumia mbinu bora za kilimo ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa, na kuhakikisha uzalishaji wa mazao unakuwa wa uhakika.
”Ni muhimu kwa wakulima kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo na kutumia mbinu bora za kilimo ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa,” amesema Mlay.
Akizungumzia kuhusu changamoto ya wadudu waharibifu kama tomato leaf miner (Tuta absoluta) ambao wameathiri uzalishaji wa nyanya amewashauri Wakulima kuwa jirani na maofisa kilimo ili kusaidia mawasiliano ya haraka endapo itatokea changamoto ya ugonjwa.
Katika hatua nyingine Mlay amekiri kuwa uzalishaji wa zao hilo la nyanya kwa mwaka huu bado ni wa wastani ukilinganisha na miaka mingine iliyopita.