Dar es Salaam. Mambo yameanza kuchangamka ndani ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), baada ya viongozi watatu wa kitaifa kujiuzulu nafasi zao, wakitaja sababu ni kukipa chama hicho fursa ya kuwapata viongozi wengine watakaoendeleza gurudumu mbele.
Waliotangaza kujiuzulu ni Katibu Mkuu wa chama hicho Mohammed Masoud Rashid, Naibu Katibu Mkuu Bara, Rahman Rungwe na Makamu Mwenyekiti Bara, Kayungo Mohammed.

Katibu wa Chauma, Mohammed Masoud akitangaza kujiuzulu nafasi hiyo mbele ya Halmashauri Kuu ya chama hicho.
Hata hivyo, uamuzi wa kujiengua kwao unahusishwa na kuwapisha viongozi wapya watakaotokana na wanachama wapya watakaopokelewa leo wakiwamo waliojivua uanachama wa Chadema.
Akitoka taarifa ya kujiuzulu kwake mbele ya wajumbe wa halmashauri kuu ya Chaumma leo, Jumatatu Mei 19, 2025 Katibu Mkuu wa chama hicho, Mohammed Masoud Rashid amesema ameachia ngazi kwa manufaa ya chama chake.
“Kwa sababu tunakiongoza chama na kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 53 nimeamua kujiuzulu ukatibu mkuu kwa madhumuni ya kukifanya chama changu na halmashauri kuu kazi yake kubwa ni kutafuta wanachama, kuingiza wanachama na wawe wanaweza kukubalika kwa wananchi.”

Naibu katibu mkuu bara wa chauma, Rahman Rungwe akitangaza kujiuzulu nafasi hiyo mbele ya Halmashauri Kuu ya chama hicho.
“Nimeachia ngazi kwa sababu ya manufaa ya chama changu ili tuongeze wanachama wengine watakaoleta manufaa kwa wananchi wetu. Sio haramu ni halali kabisa,” amesema.
Rashid alifuatiwa na Naibu Katibu Mkuu Bara, Rahman Rungwe aliyesema anaachia ngazi kwa masilahi ya umma na chama hicho ili wengine waendelee.
“Kwa masilahi ya chama changu na ya umma nichukue nafasi hii kujiuzulu nafasi yangu na kuiachia nafasi hii kwa maendeleo ya chama chetu,” amesema.

Makamu Mwenyekiti Chaumma, Tanzania Bara, Kayungo Mohammed akitangaza kujiuzulu nafasi hiyo mbele ya Halmashauri Kuu ya chama hicho.
Haikuishia hapo, Makamu Mwenyekiti Bara, Kayungo Mohammed alifuata akisema anajiuzulu kwa masilahi ya chama chake cha Chaumma.
“Kwa niaba ya wajumbe wa mkutano mkuu na wanachama naomba leo hii nitamke wazi naachia nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara kwa masilahi ya chama,” amesema.
Amesema siasa ni kama mbio za vijiti na inafika mahala unapaswa kumkabidhi mwingine aendelee kukijenga chama.
Akirejea Katiba ya chama hicho, Mkurugenzi wa Katiba na Sheria, Ali Omar Juma, amesema Katiba imefuatwa katika hatua hiyo ya kujiuzulu kwa viongozi hao.
Amesema kifungu cha 53(R) kinasema ni jukumu la halmashauri kuu kuidhinisha na kuondoa viongozi.
Taarifa hizo zilifuatiwa na kuahirishwa kwa kikao.