Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Kisutu imetoa maelekezo kwa askari wa Jeshi la Magereza kumuacha huru Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu akiwa kizimbani, badala ya kumlinda kwa kumzingira, ili apate nafasi ya kufuatilia kesi yake.
Pia, mahakama hiyo imebadili uamuzi wake wa awali wa kusikiliza kesi ya uhaini inayomkabili Lissu kwa njia ya mtandao (video conference), na badala yake kesi hiyo sasa itaendeshwa katika mahakama ya wazi.
Vilevile, mahakama hiyo imeamuru upande wa mashtaka katika kesi hiyo kutoa mrejesho wa hatima ya upelelezi wakati kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Amri hizo zimetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Franco Kiswaga, anayesikiliza kesi ya uhaini katika hatua ya awali, kutokana na hoja zilizotolewa na jopo la mawakili wanaomtetea Lissu.
Mawakili hao zaidi ya 20 wakiongozwa na Mpale Mpoki (kiongozi wa jopo), Dk Rugemeleza Nshala, Peter Kibatala, Jeremiah Mtobesya na wengine, wameibua hoja hizo leo Jumatatu, Mei 19, 2025, wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa ajili ya kujua kama upelelezi umekamilika.
Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, ameieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na akaomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa.
Baada ya maelezo hayo, ndipo jopo la mawakili hao likaibua hoja kuhusu askari kumlinda Lissu hadi kizimbani.
Hoja ya ulinzi wa Lissu iliibuliwa na Wakili Nshala kutokana na utaratibu uliotumika kumlinda.
Kwa kawaida, mshtakiwa aliye mahabusu akishafikishwa mahakamani hufunguliwa pingu na kuachwa huru, kisha anapanda kizimbani peke yake, huku Askari wa Magereza wakibaki nje ya kizimba, na baada ya kesi kumalizika, humfuata mshtakiwa kwa ajili ya kumrudisha mahabusu.
Hata hivyo, kwa Lissu, leo licha ya askari Magereza, Polisi waliovaa sare na wasio na sare waliokuwepo ndani na nje ya Mahakama, askari wengine sita walipanda kizimbani na kumzingira mshtakiwa wakati wote wa kesi.
Kutokana na hali hiyo, Dk Nshala ameiomba mahakama iamuru askari hao waondoke kizimbani na wasubiri hadi kesi itakapomalizika. Amesema kwa mujibu wa Katiba na sheria, kila mtu anahesabika kuwa hana hatia hadi itakapothibitishwa vinginevyo na mahakama.
Wakili Mpoki ameikumbusha mahakama kuwa Mei 6, 2025 ilitoa amri kwa upande wa mashtaka kuja kueleza hatua iliyofikiwa katika upelelezi, lakini leo hakuna mrejesho uliotolewa.
Wakili Kibatala naye ameikumbusha mahakama kuwa awali iliamua kesi hiyo iendeshwe kwa njia ya mtandao, lakini katika kesi nyingine ya Lissu mahakamani hapo, mahakama iliamua iendeshwe kwa uwazi, na kwamba ndio maana yuko mahakamani hapo.
Kibatala alitaja kifungu cha 192 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na kanuni ya 16(c) ya Kanuni za Uendeshaji Mashauri kwa Njia ya Mtandao za Mwaka 2021, kuwa mahakama ina mamlaka ya kubadili uamuzi wake endapo mazingira yatabadilika.
“Hata katika uamuzi wako wa awali ulisema kuwa uamuzi wa kuendesha kesi kwa mtandao si wa kudumu. Sasa kwa kuwa mazingira yamebadilika, tunaomba mahakama yako iongozwe na busara na iruhusu kesi hii iendelee kwa wazi,” amesema.
Akijibu hoja hizo, Wakili Katuga amesema kuwa upelelezi uko katika hatua za mwisho, lakini hawawezi kueleza ni nini kimezuia kukamilika haraka, huku akidai hakuna sheria inayowalazimisha kufanya hivyo.

Kuhusu ulinzi, amekiri kuwa Katiba inasema mtu anahesabika kuwa hana hatia hadi atakapotiwa hatiani, lakini hakujatajwa namna ya ulinzi wa mshtakiwa aweje. Amesisitiza kuwa ulinzi ni kwa manufaa ya mshtakiwa, mahakama na mawakili, na akaongeza kuwa haijathibitika kuwa uwepo wa askari umezua tatizo.
“Hata wenzetu upande wa utetezi hawajaeleza kuwa askari hao kumlinda kumeathiri nini,” amesema Wakili Katuga na kusisitiza;
“Ni vema hawa wenzetu wa vyombo vya ulinzi waendelee kumlinda mshtakiwa maama na sisi maofisa wa Mahakama. Na kwa mazingira ya shauri hili tena ni vema kama ulinzi ungeongezwa zaidi.”

Kuhusu utaratibu wa uendeshaji kesi hiyo, amesema kuwa kanuni iliyotajwa na Wakili Kibatala iko wazi na kwamba wao wanaiachia mahakama iangalie na kutumia busara kama iendelee kwa mtandao au ibadilishe uamuzi wake wa awali.
Dk Nshala amesisitiza kuwa upelelezi ni haki ya msingi na kwamba upande wa mashtaka ulipaswa kueleza hatua iliyofikiwa. Kuhusu ulinzi wa kizimbani, alisema hawapingi kulindwa bali wanasisitiza heshima ya mahakama na kwamba mshtakiwa awe peke yake kizimbani.
“Waendelee kulinda Mahakama kama wanavyofanya, tunaona hata kuna snipers kila mahali. Rai yetu ni kulinda utukufu wa Mahakama, mshtakiwa awe huru kizimbani,” amesisitiza.
Hakimu Kiswaga, baada ya kusikiliza hoja zote, amesema “Mahakama inasisitiza Jamhuri ikamilishe upelelezi kwa wakati, na tarehe ijayo iwe imeleta mrejesho wa wazi, si kusema tu uko katika hatua za mwisho.

“Kuhusu ulinzi kizimbani, mshtakiwa awe peke yake kizimbani ili afuatilie shauri lake ipasavyo. Vyombo vya ulinzi vitafanya tathmini ya usalama na kama hakuna sababu ya msingi ya kumzingira mshtakiwa, basi aachwe huru kizimbani,” amesema.
Kuhusu uendeshaji wa kesi, amesema mahakama imekubali kubadili uamuzi wa awali, na kuagiza kuwa kuanzia sasa kesi hiyo iendelee kusikilizwa katika mahakama ya wazi.
“Hakuna ubishi hili ni shauri la kosa kubwa la uhaini hivyo hoja ya utetezi kubadili utaratibu iko sahihi…Bila kuathiri hali ya uendeshaji shauri hili Mahakama chini ya kanuni ya 16 (c) inaamuru tarehe ijayo kesi hii itaendelea kwa namna hii hivyo mshtakiwa aletwe mahakamani,” amesema Hakimu Kiswaga.

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akisalimiana na Jaji mstaafu wa Kenya, David Maraga.
Kesi imeahirishwa hadi Juni 2, 2025 itakapotajwa tena.
Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini. Anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025, kwa madai ya kuhamasisha kuzuia Uchaguzi Mkuu 2025.
Alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Aprili 10, 2025, na tangu wakati huo yuko mahabusu kwa kuwa kosa hilo halina dhamana.