
Moshi. Kama binadamu angepewa uwezo wa kutazama kesho yake, huenda Mzee Fredy Mlinga (60) asingekanyaga kabisa ndani ya nyumba aliyojenga kwa mikono yake mwenyewe, iliyogeuka kuwa kaburi la mkewe na mwanaye wa pekee wa kiume.
Usiku wa Mei 6, 2025 katika Kitongoji cha Mndede, Kijiji cha Korini Juu, kata ya Mbokomu, Wilaya ya Moshi, uligeuka kuwa jinamizi kwa Mzee Mlinga baada ya nyumba yake kuangukiwa na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa na kusambaratisha kila kitu ikiwemo maisha ya mkewe Ester na mwanaye wa pekee wa kiume, Emanuel
Mzee Mlinga ambaye aliokolewa akiwa hai kwenye tope zito la maporomoko hayo akiwa hajitambui, amejikuta katikati ya maumivu yasiyoelezeka akitazama kaburi la mkewe na mwanaye kila asubuhi yakimkumbusha kuwa katika dakika chache tu maisha yake yalibadilika, hana tena matumaini ya kesho.
Mei 6, 2025 watu watatu wakiwemo wawili wa familia moja, mama na mwanaye walifariki dunia baada ya nyumba zao kuangukiwa na maporomoko ya udongo usiku wa manane wakiwa wamelala kufuatia mvua zilizonyesha mkoani Kilimanjaro. Watu hao akiwemo mama na mwanaye (mke na mtoto wa mzee Mlinga) walizikwa Mei 10, 2025 katika Kijiji cha Korini juu, huku mmoja akizikwa katika Kijiji cha Tema.
Nyumba yake ilisombwa kabisa na maporomoko hayo, huku mifugo waliokuwa ndani wakifa na mali zote alizojitahidi kuzikusanya kwa miaka mingi zikitoweka kwenye tope lisilo na huruma.
Akisimulia tukio hilo lilivyotokea Mzee Mlinga amesema wakati maporomoko hayo yanatokea ghafla alijikuta yuko nje, huku akiwa katikati ya tope zito ambapo alinasuliwa na majirani.
“Wakati maporomoko yalivyotokea hata mimi sikusikia nilijishtukia tu nipo nje, nikiangalia juu kupo wazi sioni nyumba, kumbe wakati huo nilishasogezwa eneo nililokuwa nalala kama hatua 30 hivi, huku mvua inanyesha na kila nikijaribu kujitingisha siwezi ikabidi nianze kupiga kelele kumbe nilikuwa nimenasa kwenye tope,”anasimulia mzee huyo.
Anasema wakati alivyonasa kwenye tope alitolewa na majirani zake akiwa hajitambui na kuwahishwa hospitali ambapo alipopata fahamu hakujua mke na mtoto wake walipo.
“Hospitali nilifanyiwa vipimo na bahati nzuri sikuwa nimevunjika popote, nilipewa dawa za kutuliza maumivu, nilipokaa sawa nilirudi nyumbani,”anasimulia mzee huyo.
Anasema wakati anarudi nyumbani hakuambiwa chochote kuhusu kifo cha mke wake wala mtoto wake mpaka alipofika nyumbani na kukuta mazingira ya majonzi huku watu wakiwa wamekaa makundi kwa makundi.
“Nilipoona mazingira yalivyokaa nilijua hakuna kitu tena (wenzangu hawapo) nilikaa kinyonge sana, niliumia sana moyoni mwangu, kwa sababu mke wangu nimeshazoeana naye na mtoto wangu, sasa kwa kweli nilishindwa kujua nifanyeje mpaka sasa unavyoniona,”anasimulia mzee huyo
Anasema licha ya kwamba kwa sasa amepata hifadhi kwa ndugu yake, halali usiku wala mchana kutokana na msongo wa mawazo.
“Hapa nilipo sina mke wala mtoto wangu niliyekuwa naishi naye, mawazo yananisumbua bado sijakaa sawa, nipo mpweke sina hili wala lile yaani sijioni sawa, sina nyumba, sina chochote, sasa hivi naishi hapa kwa ndugu yangu amenipa tu hifadhi,”
Anasema, “Maisha haya ya upweke niliyonayo najiona kama vile sijitambui maana hapa nilipo nashindwa nianzie wapi, sina mwanga najiona nipo tu na kila ninachokiwaza naona hakiendi.”
“Upweke unanipa shida zaidi, hapa nilipo ni kwa ndugu naishi, natamani ndugu jamaa na marafiki wanisaidie maana nyumba, mali zote zimesambaratika nimebaki hivi nilivyo mwenyewe na hata hizi nguo nilizovaa ni msaada,”anasimulia mzee huyo.
Victor Mlinga, ambaye ni ndugu wa mzee Fredy na mwathirika wa maporomoko hayo anasema ndugu yake ni kama amekata tamaa na wamekuwa wakijitahidi kumrudisha katika hali ya kawaida inakuwa vigumu kwa sababu kila kukicha makaburi ya wapendwa wake anayaona.
“Wakati mwingine tunakaa pamoja lakini ana mawazo sana, kuna muda nikimuangalia ana mawazo yaliyopitiliza zaidi kutokana na tatizo alilolipata ni pigo kubwa sana amepata huyu mzee, yaani moyo wake unavuja damu,”anasema.
Wadau wawakimbilia
Kufuatia tukio hilo wadau mbalimbali wamejitokeza kuwasaidia waathirika hao ikiwemo misaada ya chakula na fedha.
Akizungumza balozi wa kampuni ya Asasi na kampuni ya utalii ya Zara Tours, Salimu Kikeke amesema tukio hilo limewagusa hivyo wakaamua kuwakimbilia waathirika hao kwa kuwapa misaada mbalimbali.
Kikeke ambaye ni Mkurugenzi wa Crown Media amesema tukio kama hilo linavyotokea jamii inapaswa kushirikiana pamoja kusaidiana na kufarijiana.
“Wenzangu wa Asasi wametupa katoni 50 za maziwa kwa ajili ya kuwasaidia wenzetu waliokumbwa na maafa haya, lakini wenzetu wa Zara tours ambao tunafanya nao kazi kwa muda mrefu wameguswa na hili jambo na wametoa Sh1 milioni,”amesema Kikeke
Mwakilishi wa kampuni ya utalii ya Zara tours, Bearnald Saini amesema tukio hilo limewagusa hivyo akawataka Watanzania kujitokeza kuwasaidia waathirika wa mafuriko hayo.