
Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa Wakili Tundu Lissu imeletwa siku ya Jumatatu Mei 19, 2025 kwa ajili ya kutajwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambapo upande wa Jamhuri umeieleza Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Upande wa Jamhuri umeeleza kuwa mpaka sasa shauri hilo linaendelea na uchunguzi chini ya mamlaka za Kipolisi, na kwamba kwa kuwa upelelezi haujakamilika hivyo wanaiomba Mahakama kuhairisha kesi husika kwa siku 14 zaidi, jambo ambalo limeonekana kupingwa vikali na Mawakili wa utetezi.
Jopo la Mawakili wa utetezi likiongozwa na Mawakili waandamizi Mpale Mpoki, Dkt. Rugemeleza Nshala na Peter wameliwasilisha maombi kadhaa mahakamani hapo, ambapo miongoni mwake wameiomba Mahakama ‘kulazimisha’ upande wa Jamhuri ueleze nini hasa kinachokwamisha upelelezi kwa sababu mwanzo ilidaiwa mahakamani kuwa ushahidi wote kuhusiana na shauri hilo upo mtandaoni.
Jambo la pili walilowasilisha Mawakili wa utetezi mahakamani ni kwamba, hawafurahishwi namna ambavyo mteja wao anavyokuwa amezungukwa na maafisa wa Jeshi la Magereza (askari), ambapo wameishawishi mahakama kutoa amri ya kuwaondoa askari wote ‘wanaomlinda’ Lissu ndani ya chumba cha Mahakama, kwa kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 Mahakama haimtambui mtuhumiwa.
Miongoni mwa waliofika kusikiliza kesi hiyo ni Jaji Mkuu Mstaafu wa Kenya David Maraga na Mwanahabari Mkongwe wa Tanzania, Jenerali Ulimwengu. Lissu, akiwa amezingirwa na askari wa usalama aliwasili katika Mahakama hiyo mnamo saa 3 na nusu asubuhi, akiwa ameshikilia begi kubwa lililojaa vitabu.
wa hiyo kesi ya uhaini dhidi ya Lissu imeahirishwa hadi Juni 2 mwaka huu ambapo itasikilizwa kwa njia ya mahakama ya wazi na shauri la uchochezi dhidi ya Lisuu kadhalika bado linaendelea.