Gugumaji jipya ladhibitiwa Ziwa Victoria

Mwanza. Serikali imefanikiwa kudhibiti gugumaji jipya aina ya salvinia molesta, huku changamoto ikibaki kushamiri kwa gugumaji la asili la lutende.

Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Jumatatu, Mei 19, 2025, alipotembelea eneo la Kigongo – Busisi mkoani Mwanza kujionea hali halisi na uvunaji wa gugumaji la lutende, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Cyprian Luhemeja, amesema tangu Februari hadi Mei 18, 2025, tayari tani 840 za gugumaji jipya zimeopolewa.

Amesema kwa sasa changamoto iliyopo ni gugumaji la lutende ambalo limesambaa ekari 375 kwenye Ziwa Victoria, hata hivyo tayari ekari 65 zimevunwa.

Mkurugenzi wa Tafiti ya Mazingira Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk Menan Jangu, ametaja baadhi ya mbinu zilizotumika kumaliza gugumaji jipya kuwa ni pamoja na kutumia mitumbwi na matenga kuyaopoa na kufanikiwa kutatua changamoto ya usafiri kwa wananchi wanaotumia vivuko eneo la Kigongo – Busisi.

“Ziwa Victoria linakabiliwa na changamoto ya gugumaji. Gugumaji hili limegawanyika katika aina tatu; aina ya kwanza ni gugumaji jipya la salvinia molesta, aina ya pili ni water hyacinth (maji parachichi), na gugumaji la asili aina ya lutende,” amesema Dk Jangu.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Kigongo – Busisi alipotembelea eneo hilo kujionea udhibiti wa magugumaji ndani ya Ziwa Victoria.

Amesema magugumaji hayo yameathiri mfumo wa ikolojia, shughuli za usafiri na usafirishaji na uvuvi katika baadhi ya maeneo ndani ya ziwa hilo.

“Gugumaji aina ya water hyacinth limeshadhibitiwa na Serikali kupitia Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) kwa kushirikiana na taasisi nyingine.

“Kwa sasa hivi, eneo letu la ziwa linakabiliwa na gugumaji la asili aina ya lutende. Pamoja na faida za mimea aina ya lutende katika uhifadhi wa bayoanuwai, mazalia ya samaki na kuchuja maji yanayoingia ziwani, mimea hii inapomeguka na kuacha eneo lake la asili na kuingia ziwani inaathiri shughuli za usafiri na usafirishaji pamoja na shughuli za uvuvi kwa wananchi,” amesema mtafiti huyo.

Amesema kutokana na gugumaji la lutende kuathiri ekari 375 za eneo la Kigongo-Busisi, pia limeathiri shughuli za uchumi zinazotegemewa kwenye ziwa hilo.

“Jumla ya tani 840 zimeondolewa na kufungua njia ya usafirishaji katika eneo la Kigongo-Busisi. Kwa sasa eneo hili halina changamoto ya gugumaji jipya.

“Kwa sasa, juhudi zinaendelea za kushughulikia gugumaji hili la asili aina ya lutende. Jumla ya ekari 65 zimeshughulikiwa katika kipindi cha wiki moja, na lengo ni kumaliza ekari zote kabla ya kufika Juni 10, 2025,” amesema Dk Jangu.

Amesema tayari wamekamilisha mchakato wa ununuzi wa mitambo miwili maalumu ya kuchakata gugumaji salvinia molesta endapo litatokea tena, na mtambo mwingine wa kuondoa gugumaji la lutende unatarajiwa kuingia nchini kabla ya mwishoni mwa Julai, 2025.

Ameeleza, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Kamati Tendaji ya Makatibu Wakuu itaendelea kusimamia mkakati wa kudhibiti gugumaji na kutoa taarifa kila baada ya miezi mitatu, zoezi hilo litahusisha maeneo yote ya Ziwa Victoria mara baada ya mitambo hiyo kuwasili.

Maagizo ya Majaliwa

Naye, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameagiza Bodi ya Bonde la Ziwa hilo pamoja na taasisi nyingine kuhakikisha magugumaji hayo yanaondolewa na ziwa hilo linabaki safi.

“Tunataka tusafishe eneo hilo lote libaki wazi tutakapoanza matumizi ya barabara na daraja letu, huku chini kuwepo na mazingira ya kuvutia,” amesema na  kuongeza;

“Serikali inaendelea kupambana na magugumaji… nyie wenyeji hapa mmeshuhudia kwa muda mrefu uwepo wa magugumaji hayo ambayo yapo ya zamani na mapya ambayo yamefunika sehemu kubwa ya ziwa na kupunguza ukubwa wa ziwa.”

Amesema iwapo magugu hayo yakiachwa na kuendelea kuongezeka, shughuli za uvuvi ambazo zinategemewa na watu wengi zitaathirika.

“Unapopunguza ukubwa wa ziwa, ina maana unapunguza shughuli za kibinadamu, ikiwemo uvuvi. Pia, uwepo wa magugu hayo ulikuwa unaziba njia ya kupita vivuko, na vivuko hivyo vinapopita vinaharibika na kutengeneza tatizo lingine kubwa la usafiri,” amesema Majaliwa.

Amesema jitihada nyingine zinazofanywa na Serikali ni kuwawezesha wataalamu wa ndani kwenda kujifunza nchini Uganda namna ambavyo nchi hiyo inapambana na mimea hiyo vamizi.

“Natumia nafasi hii kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa fedha kwa ajili ya kununua mitambo hiyo ili ibaki ndani ya Ziwa Victoria, na itakwenda popote ndani ya ziwa kuanzia Mkoa wa Mara, Simiyu, Mwanza, Geita na Kagera, itapita mpaka kwenye visiwa vyote kuhakikisha gugumaji kama lipo linaliwa mara moja,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *