Mwakilishi ataka tume ya pamoja ya fedha ivunjwe, Serikali yajibu

Unguja. Wakati mwakilishi akiibua hoja barazani kuhusu kutokuwa na umuhimu wa Tume ya Pamoja ya Fedha kutokana na kulalamikiwa kila mara, Serikali imesema uwepo wa tume hiyo una tija katika kuimarisha uhusiano wa kifedha kati ya Serikali zote mbili.

Tume ya Pamoja ya Fedha ni taasisi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) iliyoundwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 134 na kuanzishwa kwa sheria ya tume hiyo, Sura 140.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu, Mei 19, 2025 katika mkutano wa 19 wa Baraza la Wawakilishi baada ya Mwakilishi wa Wingwi, Kombo Mwinyi Shehe, kuhoji kuna haja gani ya kuendelea na tume hiyo ilhali utendaji kazi wake bado unaendelea kulalamikiwa kila siku.

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Juma Makungu Juma, amesema bado ina tija kubwa na kueleza faida zilizopatikana kupitia tume hiyo.

“Mheshimiwa Spika, jukumu la msingi la Tume ya Pamoja ya Fedha ni kutoa ushauri na mapendekezo kuhusu uhusiano wa kifedha kati ya Serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ),” amesema.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 133 na 134, majukumu ya tume ni kuchambua mapato na matumizi yanayotokana na, au yanayohusu, utekelezaji wa mambo ya Muungano na kutoa mapendekezo kwa Serikali mbili kuhusu mchango na mgawanyo wa kila mojawapo wa Serikali hizo.

Naibu Waziri huyo ametaja majukumu mengine kuwa ni kuchunguza kwa wakati wote mfumo wa shughuli za kifedha wa Jamhuri ya Muungano na pia uhusiano katika mambo ya kifedha kati ya Serikali mbili, na kutekeleza majukumu mengine ambayo Rais ataipatia Tume au kama Rais atakavyoagiza, na kwa mujibu wa sheria itakavyotungwa na Bunge.

Amesema katika kutekeleza jukumu la kutoa ushauri kuhusu uhusiano wa kifedha kati ya SMT na SMZ, Tume ya Pamoja ya Fedha imekuwa ikifanya uchambuzi na tafiti katika masuala yanayohusu uhusiano wa kifedha kwa lengo la kutoa ushauri na mapendekezo.

Kwa mujibu wa waziri huyo, ushauri na mapendekezo yanayotolewa na tume hiyo yamekuwa na faida kwa Serikali zote mbili, ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano katika ukopaji wa nje ya nchi.

“Katika eneo hili, tume ilizishauri Serikali mbili kuzingatia mahitaji na vipaumbele vya kila upande wa Muungano kwa ajili ya ukopaji nje ya nchi,” amesema.

Pia, katika eneo hilo, Naibu Waziri amesema tume ilishauri kuongeza idadi ya wajumbe katika Kamati ya Wataalamu ya Usimamizi wa Madeni na Kamati ya Taifa ya Usimamizi wa Deni la Taifa.

Kabla ya ushauri huo, SMZ ilikuwa ikiwakilishwa na wajumbe wawili (Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, na Mhasibu Mkuu wa SMZ) na SMT ikiwa na wajumbe wanane.

Ushauri huo uliziwezesha Serikali kufanya marekebisho ya Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura 134, na marekebisho hayo yameongeza idadi ya wajumbe katika kamati hizo hadi kufikia wajumbe watano wanaotoka SMZ, hivyo kuongeza uwazi na uwiano mzuri wa ushiriki kwa pande zote mbili za Muungano katika ukopaji wa nje ya nchi.

Amesema katika kuimarisha ushirikiano katika upangaji wa sera za kodi za Muungano, tume ilizishauri Serikali kuweka utaratibu wa kushauriana katika upangaji wa viwango vya utozaji wa kodi za Muungano ili kuweka uwiano mzuri katika kukuza uwekezaji, biashara na kuimarisha uchumi na ustawi wa jamii katika pande zote mbili za Muungano.

Amesema kupitia ushauri huu, Sheria ya Bajeti, Sura 439, imeweka utaratibu wa Serikali mbili kushirikiana katika upangaji wa sera za kodi zinazozingatia maslahi ya pande zote mbili kila mwaka wa fedha.

Kuhusu mfumo wa biashara, katika eneo hili, Serikali mbili zilishauriwa kuondoa vikwazo visivyo vya kodi kwa wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar au kinyume chake.

Lengo lilikuwa ni kuimarisha biashara na uwekezaji katika pande zote mbili na kuongeza uelewa kuhusu uhusiano wa kifedha kati ya SMT na SMZ.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *