Barcelona, Hispania. Klabu ya Barcelona imefanikiwa kukabidhiwa kombe lake la Ligi Kuu ya Hispania, La Liga, pamoja na kupoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya Villarreal, huku staa wake Lamine Yamal akiweka rekodi mpya.
Huu ulikuwa mchezo wa kwanza Barcelona wanapoteza kuanzia ilipofanya hivyo tena Desemba mwaka jana, lakini bado haikuwazuia kukabidhiwa kombe hilo ambalo ililitwaa baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Espanyol wiki moja iliyopita.

Kocha wa Barcelona Hansi Flick, amesema anaamini kuwa bado wanaweza kufanya vizuri msimu ujao kama wataboresha zaidi kikosi chao.
“Nafikiri Villarreal walicheza vizuri sana, lakini zaidi ya hilo sisi ni mabingwa,” alisema mchezaji wa Barcelona Fermin Lopez, ambaye alifanikiwa kuifungia timu yake bao la pili.
“Ninafuraha kuona nimefunga bao na kuisaidia timu yangu ingawa tumepoteza lakini furaha yetu kwa leo ni kuona kuwa tumefanikiwa kutwaa ubingwa huu, hili ndiyo jambo zuri zaidi kwetu kwa leo, hayo mengine yatafuata baadaye,” alisema Lamine Yamal ambaye aliifungia Barca bao moja.

Lamine Yamal, ameweka rekodi ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa La Liga mara mbili hata kabla hajafikisha umri wa miaka 18, lakini kwa ujumla akiwa ametwaa makombe matano kwenye maisha yake ya soka akiwa amekaa kwenye soka la ushindani kwa kipindi kifupi.
Amefanikiwa kutwaa Kombe la Euro akiwa na Hispania, Copa del Rey, Spanish Super Cup na makombe mawili ya La Liga, ikiwa ni rekodi kwenye maisha yake kwa kuwa hakuna mchezaji hata mmoja wa Ligi Kuu ya Hispania amewahi kufanya hivyo.
Huku msimu ukitarajiwa kufungwa wikiendi ijayo Barcelona ipo kileleni na pointi 85, zikiwa ni nne zaidi ya timu inayoshika nafasi ya pili Real Madrid, huku Atletico ikiwa ya tatu na pointi 73.
Athletic Bilbao, ina pointi 70, na Villarreal, 67 na kukamilisha tano bora kwenye La Liga ambayo itawakilisha nchi hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.