
Rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden, amegunduliwa kuwa na saratani ya tezi dume aina kali, ambayo tayari imesambaa hadi kwenye mifupa, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi yake binafsi.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Taarifa hiyo imeeleza kuwa wiki iliyopita, Biden alifanyiwa uchunguzi baada ya kuanza kupata dalili za kuongezeka kwa matatizo ya njia ya mkojo, na madaktari waligundua uvimbe mpya kwenye tezi dume. Kufuatia vipimo vya kina, aligunduliwa kuwa na saratani ya tezi dume yenye alama ya Gleason 9 (Kundi la Daraja 5), hali inayodokeza ukali wa juu wa ugonjwa huo na usambao hadi kwenye mifupa.
Hata hivyo, taarifa hiyo imeongeza kuwa aina ya saratani aliyogundulika nayo bado ni nyeti kwa homoni, jambo linalotoa matumaini ya usimamizi bora wa matibabu. “Ingawa hii ni aina kali ya saratani, inaonesha kuwa nyeti kwa matibabu ya homoni, jambo linalowezesha usimamizi mzuri wa ugonjwa huu,” taarifa hiyo imesema.
Rais wa sasa wa Marekani Donald Trump amesema amehuzunishwa na taarifa hizo na kumtakia kila la heri mke wa Biden, Jill na familia na afueni ya haraka kwa Joe Biden.
Naye Makamu wa rais wa zamani wa Marekani Kamala Harris amesema anahuzunishwa kujua juu ya ugunduzi huo na ana matumaini Joe Biden atapona kikamilifu na kwa haraka, huku akisema Joe ni mpambanaji na anaamini ataikabili changamoto hiyo kwa nguvu, uthabiti na matumaini, mambo ambayo yamekuwa kilelezo cha maisha yake na uongozi wake.