Na Gideon Gregory, Dodoma
Wazi wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana amesema, Wizara hiyo imewezesha ujenzi wa viwanda vya kati na vikubwa vya kuchakata na kuongeza thamani mazao ya nyuki na kufanya idadi ya viwanda hivyo kuongezeka kutoka kiwanda kimoja (1) mwaka 2020 hadi kufikia viwanda nane (8) mwaka 2025.
Balozi Dkt. Chana ameyasema hayo leo Mei 19,2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025/26 ambapo ameongeza kuwa Viwanda hivo vimejengwa katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Singida, Iringa, Katavi na Geita.
“Hadi kufikia Aprili 2025, jumla ya tani 1,321.35 za asali zenye thamani ya shilingi Bilioni 15 zimeuzwa nje ya nchi sawa na asilimia 206.9 ikilinganishwa na kiasi cha tani 430.61 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 5 zilizouzwa nje ya nchi kwa kipindi kama hicho mwaka 2024,”amesema.
Aidha, ameongeza kuwa kwa maendeleo hayo, Shirika la Wafugaji Nyuki Duniani limeiteua Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wafugaji nyuki duniani (APIMONDIA) mwaka 2027, utakaohudhuriwa na watu zaidi ya 4,000 kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
Mbali na hayo amesema Serikali imeendelea kushuhudia kuimarika kwa biashara ya
mazao ya misitu na nyuki nchini ambapo kuimarika kwa biashara hiyo kunatokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi.
“Katika kipindi cha miaka mitano (5), kumekuwa na ongezeko la kiwango cha uzalishaji wa malighafi mbao katika mashamba ya Serikali yanayolimwa
miti kibiashara kutoka mita za ujazo 1,108,791 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 hadi kufikia mita za ujazo 1,264,535 mwaka wa fedha 2024/2025,”amesema.
Sambamba na hilo, amesema thamani ya mauzo ya mazao ya misitu nje ya nchi imeongezeka kufikia Shilingi Bilioni 458 mwaka 2024/2025 sawa na asilimia 333.8 ikilinganishwa na Shilingi Bilioni 105 mwaka 2020/2021.
The post IDADI YA VIWANDA VYA KUONGEZA THAMANI MAZAO YA NYUKI VYAONGEZEKA NCHINI appeared first on Mzalendo.