
IMEPITA miaka minne sasa bila rekodi ya Aisha Masaka aliyetimkia Brighton & Hove Albion kuvunjwa katika Ligi Kuu Wanawake ya kufunga mabao mengi.
Msimu 2020/21 Masaka aliibuka mfungaji bora wa WPL akiweka kambani mabao 35 akiwa mzawa wa mwisho kufunga mabao hayo.
Tangu hapo msimu uliofuata Mrundi wa Simba Queens, Asha Djafar alifunga mabao 27, msimu 2022/23 akachukua tena Mkenya, Jentrix Shikangwa akifunga mabao 17 na mwaka jana Aisha Mnunka wa Simba akiweka kambani mabao 20.
Ulikuwa msimu wenye ushindani kwa wachezaji wazawa kwani mfungaji bora alijulikana kwenye mechi za mwisho wa msimu.
Hadi mechi za mwisho Opah Clement wakati ule yupo Simba alikuwa na mabao 34 mechi ya mwisho iliamua Masaka akachukua kiatu baada ya kufunga hat-trick.
Hata hivyo, baada ya kuondoka kwa nyota hao waliopata timu nje ya nchi hakukuwa na ushindani kwa wachezaji wazawa jambo linaonyesha kuna pengo kwa washambuliaji hao.
Kwa sasa Stumai anachuana na Shikangwa ambaye ni Mkenya wakitofautiana mabao manne tu kwenye mechi 17 zilizochezwa WPL.
Hadi sasa Stumai amefunga mabao 27 kwenye mechi 17 zilizochezwa huku Shikangwa akiweka kambani 23 tofauti ya mabao manne baina yao.
Imesalia mechi moja kuamua hatma ya vinara wa mabao WPL lakini mambo yanaonekana kuwa magumu kwa Stumai na Shikangwa ambao wako kwenye nafasi nzuri ya kuchukua kiatu.
Rekodi hiyo inaonekana kuwapalia kooni washambuliaji hao na ili wafikie na kuivunja Stumai anapaswa kufunga mabao tisa na Shikangwa aweke kambani 13.
Kiufupi msimu huu pia washambuliaji wameshindwa kuvunja rekodi ya Masaka na anaendelea kushikilia rekodi hiyo akiwa England.