
Mbeya. Watu watatu wakazi wa wilaya za Chunya na Mbarali mkoani Mbeya wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja baada ya kupatikana na makosa ya ubakaji.
Katika tukio la kwanza, Mahakama ya Wilaya ya Mbarali mkoani hapa, imemuhukumu Kulwa Memba (30), mkazi wa Kijiji cha Lukali kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka binti wa miaka (17) mwenye ulemavu wa ngozi.
Imeelezwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo alimbaka binti huyo mara kadhaa na kisha kumtorosha kwenda jijini Dar es Salaam kuishi naye kama mke wake.
Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa Msaidizi wa Polisi, Given Komba alieleza mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kipindi cha Januari mpaka Aprili 2024.
Amesema baadaye mshtakiwa alimtorosha na kwenda kuishi naye eneo la Buguruni Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam kama mke na mume, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Komba amesema ili kukomesha matukio hayo, ameomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa iwe fundisho kwa wengine na kulinda haki za watoto wa kike.
Kufuatia ushahidi uliotolewa, Mei 5, 2025, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbarali, Aliko Mwandumbya alitoa hukumu ya kutumikia kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwa wengine.
Wakati huohuo, mkazi wa Kijiji cha Madibira kilichopo Wilaya ya Mbarali, Amiri Kaduma (20), amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kujaribu kubaka.
Mshtakiwa alitenda kosa hilo katika Kijiji cha Nyamakulu baada ya kuingia chumbani alikokuwa amelala binti mwenye umri wa chini ya miaka 12.
Mwendesha mashtaka wa Serikali, Hannarose Kasambala aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Julai 24, 2024, usiku baada ya kuingia chumbani alikokuwa amelala binti huyo.
Imeelezwa baada ya kuingia chumbani, alimvua nguo za ndani kwa nguvu kwa lengo la kutaka kumbaka, ndipo alipiga kelele za kuomba msaada na mshtakiwa alifanikiwa kukimbia.
Amesema baada ya taarifa kutolewa polisi, msako ulianza na kufanikiwa kumkamata, lakini baada ya upelelezi alifikishwa mahakamani kusomewa mashitaka.
Hata hivyo Aprili 30, 2025 Hakimu Mfawidhi, Emily Mwambapa alimuhukumu kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.
Katika hatua nyingine, mkazi wa kitongoji cha Itumbi kilichopo kata ya Matundasi, Wilaya ya Chunya mkoani hapa, Lutenga Majora (32) amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kumbaka mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 14.
Awali, ilielezwa mahakamani hapo kuwa Mei 14, 2024, Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Chunya (jina limehifadhiwa) alipokea taarifa kwa wasamaria wema kuwa mshtakiwa anaishi kinyumba na binti mdogo.
Baada ya taarifa hizo, walianza ufuatiliaji ambapo Mei 15, 2024, mshtakiwa alikamatwa akiwa anaishi na binti na kufikishwa Kituo cha Polisi Chunya.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mwajabu Tengeneza amesema mtuhumiwa alitiwa hatiani baada ya upelelezi kukamilika ikiwepo ushahidi wa mwathilika wa tukio hilo ambaye aliishi naye kinyumba kwa muda wa siku tisa akimbaka mara kadhaa.
Mei 20, 2024, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Chunya, James Mhanusi alitoa hukumu ya kutumikia kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwa wengine.
Mkazi wa Kata ya Matundasi Wilaya ya Chunya, Ndomba John amesema kumekuwepo kwa matukio mengi ya ubakaji yanayojitokeza katika maeneo ya machimbo ya madini ya dhahabu yanayo husishwa na imani za kishirikina.
“Kuna miezi matukio ya ubakaji yanajirudia sana na changamoto kubwa kuhusishwa na imani za kishirikina, tuombe Serikali na asasi za kiraia kukemea ili kunusuru kundi la watoto wa kike ambao ndio Taifa la kesho,” amesema.