Yanga yamuuza rasmi Aziz KI, acheza mechi ya mwisho

Kama umemuona kiungo Stephanie Aziz KI uwanjani leo akiichezea Yanga basi umebahatika kumtazama kwa mara ya mwisho kiungo huyo akiwa na jezi ya timu hiyo.

Yanga leo Jumapili imemuaga rasmi kiungo huyo uwanjani na wakati wowote kuanzia sasa atatimka kwenda kujiunga na klabu mpya huko Afrika Kaskazini.

Taarifa ya uhakika ni kwamba, Yanga itamuuza Aziz KI huko Morocco kwa klabu ya Wydad Athletic ambayo imefanikiwa kufikia dau ambalo Yanga ililihitaji.

Wydad na FAR Rabat zote zilikuwa zinamuwania kwa karibu kiungo huyo,  lakini Wydad ikapiga bao kwa dakika mwisho.

Ukiondoa dau la fedha ambalo Wydad itailipa Yanga  lakini Waarabu hao imeyatumia mashindano ya Klabu Bingwa Dunia itakayofanyika mwaka huu kama njia ya kumnasa Mchezaji Bora huyo wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Aziz KI, anatakiwa haraka Morocco kwenda kumaliza kila kitu kuhusu dili hilo ikiwa ni kuwahi maandalizi ya msimu mpya.

Yanga imelazimika kutumia mechi ya leo ya nusu fainali ya Kombe la FA kumuaga Aziz Ki, huku wachezaji wenzake wakimpa heshima ya kuwa nahodha wa mechi hiyo, walioshinda kwa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania, licha ya nahodha msaidizi wa kikosi hicho, Dickson Job kuwepo uwanjani.

Kiungo huyo alicheza kwa dakika 73 pekee kabla ya kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Clatous Chama.

Usiku huu, mara baada ya mechi hiyo wachezaji wa Yanga na viongozi  wanaendelea na hafla fupi ya kumuaga kiungo huyo ambaye atatimka haraka nchini mara baada ya kurejea jijini Dar es Salaam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *