Dar es Salaam. Ukiachana na uwezo wake kiuongozi na hotuba yake iliyoakisi kiu kubwa ya Waafrika, sifa ya Tanzania kidiplomasia barani Afrika ni miongoni mwa mambo yaliyochangia ushindi wa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi.
Kipindi cha kampeni iliyochukua takribani miezi mitatu, Mjumbe Maalum wa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alionekana akizunguka katika nchi kadhaa za Afrika kumnadi Profesa Janabi.
Huu ni mwendelezo kwa Watanzania kadhaa ambao wamefanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali duniani, kutokana na uzalendo wa kuipigania nchi katika medani za siasa za dunia.
Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaalamu ya Mawaziri wa Umoja wa Afrika kutoka Liberia, Dk Louise Mopleh Kpoto, amesema Janabi ameshinda kwa kishindo baada ya nchi 32 kumchagua kati ya 46. Ili ashinde alitakiwa kupata kura 24.
Dk Louise amesema Profesa Janabi atatumikia nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano na miezi minane.
Uchaguzi huo umefanyika leo Jumapili, Mei 18, 2025, mbele ya Bodi ya Utendaji ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kamati ya Kanda ya Afrika katika kikao cha ana kwa ana kilichofanyika jijini Geneva, Uswisi.
Uchaguzi huo umeitishwa kwa mara nyingine baada ya kifo cha aliyekuwa mteule wa nafasi hiyo, Mtanzania Dk Faustine Ndugulile, aliyechaguliwa kushika nafasi hiyo Agosti 27, 2024, na kufariki dunia Novemba 27, 2024, wakati akipatiwa matibabu nchini India.
Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pongezi kwa Profesa Janabi kuchaguliwa katika nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka 2025 hadi 2030.
“Kwa kuwa na uzoefu na ujuzi wa miongo kadhaa katika sekta ya afya, nina imani kubwa kwamba una kila sifa zinazohitajika kulitumikia bara letu na kuliongoza kufikia mafanikio makubwa zaidi.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawashukuru kwa dhati nchi zote wanachama zilizouamini uwezo wako, uzoefu wako na maono yako kwa ajili ya bara letu. Profesa, nakutakia kila la heri na mafanikio tele katika kipindi chako cha uongozi,” ameandika Rais Samia katika kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Akitoa hotuba yake baada ya ushindi, Profesa Janabi ambaye pia ni Mshauri wa Rais wa Tanzania kwenye Masuala ya Afya na Tiba, ametoa shukrani zake za dhati kwa nchi zote barani Afrika kwa kumwamini na kumpa nafasi hiyo, huku akiahidi kutekeleza maono yake kwa ushirikiano na nchi zote 47.
“Niwashukuru wote kwa kuniamini na sitawaangusha. Naamni tutatengeneza Afrika yenye nguvu kubwa katika kufanikisha maono haya. Natarajia kushirikiana nanyi katika kuipeleka Afrika mbele.
“Mambo muhimu kuzingatia ni pamoja na uwekezaji wa fedha katika sekta ya afya, mmesikia vipaumbele vyangu. Natarajia ushirikiano kwa wote ili kufikia haya malengo,” amesema.
Akitoa salamu zake, Waziri wa Afya nchini, Jenista Mhagama amesema kwa niaba ya Rais Samia anatoa shukrani kwa kuiamini Tanzania kushika kijiti hicho na kupokea pole za kifo cha Dk Ndugulile.
“Ushindi huu si kwetu pekee, bali kwa wote wanaoamini katika maono ya Profesa Janabi na huduma bora za afya. Tanzania itaendelea kumpa ushirikiano katika ahadi aliyoiweka na kuahidi kufanya kazi bega kwa bega na mataifa yote kuhakikisha malengo ya WHO Afro yanafikiwa,” amesema Jenista.
Kilichompa ushindi
Hotuba yake iliyoakisi kiu kubwa ya Waafrika katika mapinduzi ya sekta ya afya, elimu na uongozi wake ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa kumpa ushindi wa kishindo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Elibariki Kingu ametoa heshima na shukrani kwa Rais Samia, akisema amekuwa mzalendo wa kuipigania Tanzania katika medani za siasa za dunia.

Kingu amesema ushindi huo ni ishara tosha kwa dunia kuwa Tanzania ina kiongozi shupavu na shujaa.
“Hotuba ya Profesa Janabi imeakisi kiu kubwa ya Waafrika katika mapinduzi ya sekta ya afya, ikizingatia kuhama kwa mlengo wa dunia katika ufadhili wa huduma nyingi za afya barani Afrika.
“Tanzania inakwenda kutoa uongozi katika sekta ya afya Afrika, tunamuombea kwa Mungu afanikiwe na kuipa nchi yetu heshima,” amesema Kingu.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema uwezo wake kitaaluma, kiuongozi, ushawishi wa Tanzania Afrika, rekodi ya ushindi wa Dk Ndugulile, na idadi kubwa ya wagombea kutoka Afrika Magharibi ni miongoni mwa mambo yaliyompa ushindi.
Amesema historia imeandikwa kwa Mtanzania mwingine kushika nafasi hiyo iliyowahi kushindaniwa na Dk Ndugulile na kuwa Mtanzania wa pili kushika nafasi hiyo.
Amesema kuna manufaa mengi ambayo Taifa na Profesa mwenyewe atayapata kwa kuwa mshindi.
“Tanzania ina ushawishi mkubwa Afrika katika medani za siasa, na leo tunadhibitisha kwa kutoa viongozi bora wanaoweza kuliongoza bara letu,” amesema.
Dk Nkoronko amesema amefuatilia hotuba yake ambayo imejaa matumaini makubwa kwa Waafrika, kwa kuwepo kwa mashirikiano ya kikanda.
Amesema Tanzania inasimama kama kinara wa huduma za afya, kwa sababu kwa Afrika ni miongoni mwa nchi 10 bora kupunguza vifo vya kinamama.
Amesema kwa kushika nafasi hiyo, inamaanisha mataifa mengi yatakuja kujifunza kutoka Tanzania.
“Pia tunajenga sura mpya kwa vijana wetu waliopo shule, waliozaliwa na baadaye kuwa katika Taifa letu ambalo liliwahi kuwa na viongozi waliovuka mipaka na kwenda kuongoza nchi zingine duniani, ikiwemo Shirika la Afya Duniani Ukanda wa Afrika,” amesema.
Ametaja faida nyingi ambazo nchi itazipata, ikiwemo fedha za kigeni ambazo Profesa Janabi atalipwa kama mshahara wake na zitaingia katika akaunti za Tanzania.
“MAT inampongeza kwa dhati mwanachama wetu kwa kushinda nafasi hii na tunaipongeza timu ya kampeni chini ya Dk Ntuli, jitihada zote za Serikali na wengine wote waliomtakia mema na walio na mawazo tofauti kuweza kufikia malengo aliyofikia,” amesema.
Ameongeza kuwa wanatamani kuona aliyoainisha yanawezekana, kuongeza ushiriki wa huduma bora za ubingwa bobezi na viwanda vya dawa, kudhibiti milipuko ya magonjwa na mengine.
Mawaziri wa nchi mbalimbali wametoa salamu zao za pongezi kwa nchi ya Tanzania na Profesa Janabi huku wakionyesha imani yao kubwa katika uongozi wake ujao.
Vipaumbele
Upatikanaji wa huduma za afya kwa wote (UHC) unaoendana na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), akibainisha kuwa Afrika imechelewa katika utekelezaji wake.

Ufadhili endelevu- ameeleza kuwa nchi wanachama huchangia asilimia 20 pekee ya bajeti ya WHO. Hali hiyo inazuia uhuru wa shirika hilo, hivyo anaunga mkono kuongeza michango ya lazima na kupanua vyanzo vya fedha kupitia bima ya afya, ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, uwekezaji mseto, ubadilishaji wa madeni kwa afya, na kufutwa kwa madeni ya kimataifa.
Maandalizi ya kukabiliana na dharura za kiafya: kinajumuisha kuimarisha nguvu kazi ya afya, kuboresha ufuatiliaji wa magonjwa, kuimarisha mifumo ya mwitikio wa haraka, na kukuza ushirikiano wa mipakani.
Afya ya mama, mtoto na lishe: amesema Afrika inachangia asilimia 70 ya vifo vya wajawazito na asilimia 56 ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano duniani.
Kupambana na magonjwa ya kuambukiza, yasiyoambukiza na magonjwa yaliyopuuzwa: kwa kutekeleza mikakati thabiti ya kudhibiti magonjwa, kukuza maisha yenye afya, na kutambua uhusiano kati ya binadamu, wanyama, mimea na mazingira.

Kupambana na usugu wa vimelea vya dawa (AMR): tatizo linalosababisha vifo milioni 1.2 kila mwaka, huku asilimia 40 ya mataifa ya Afrika yakikosa takwimu za ufuatiliaji. Ameahidi kuanzisha hifadhidata za kikanda kukabiliana na tatizo hilo.
Kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa ndani wa bidhaa za afya: ikiwemo chanjo, dawa na kuboresha tafiti.