Zitto ashtakiwa kwa andiko la IPTL

Dar es Salaam. Mfanyabiashara Harbinder Sethi amemfungulia mashtaka kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, akimtuhumu kumdhalilisha kwa kuchapisha taarifa za uongo, kashfa na zenye madhara dhidi yake.

Shtaka hilo la Sethi katika Mahakama Kuu ya Tanzania limetokana na chapisho la Zitto katika ukurasa wake wa X (zamani Twitter) akifafanua kuhusu sakata la IPTL kwa kurejea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere.

Kwa mujibu wa taarifa ya wito wa mahakama hiyo, Zitto anapaswa kufika mahakamani hapo saa 2:30 asubuhi ya Juni 12, 2025, siku ambayo kesi hiyo namba 8810 ya 2025 itatajwa mbele ya Jaji Philip.

Leo Jumapili, Mei 18, 2025,  Zitto amethibitisha kwa waandishi wa habari kuhusu kupokea wito huo wa mahakama, akisema ni jukwaa zuri la kuweka wazi kila kilichojificha kuhusu sakata la IPTL.

“Nimepokea wito wa mahakama Aprili 29, mwaka huu na kwamba nimefunguliwa kesi na Sethi kuwa nimemkashifu na kumshushia heshima kwa sababu na ameiomba mahakama nimlipe mabilioni ya fedha,” amesema.

Zitto amesema ataitumia kesi hiyo kuweka wazi mambo yote yaliyoonekana kuwa wingu la muda mrefu nchini kuhusu sakata la IPTL lililomhusisha Sethi.

“Sikatai kuandika maneno ambayo Sethi ananituhumu nayo. Niliyaandika na kuyachapisha X, na yanaakisi picha halisi na yenye ukweli wa jambo zima hili la IPTL,” amesema.

Ingawa alichapisha andiko hilo kwa nia njema, amesema kwa kuwa ameshtakiwa, yuko tayari kukutana na Sethi mahakamani kuweka wazi kila kinachostahili.

Zitto, wakati wa sakata hilo, alikuwa Mbunge wa Kigoma Kusini na ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Akiwa na nafasi hizo, alifichua sakata hilo na kuongoza kuchunguza malipo yenye utata kutoka akaunti ya Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania kwenda IPTL.

Ripoti ya kamati yake ilifichua ukiukwaji wa taratibu na madai ya rushwa katika miamala hiyo na matokeo hayo aliyawasilisha bungeni na kuibua mjadala kwa umma.

Katika sakata hilo, kilichokuwemo ni mkataba tata wa kuzalisha umeme kati ya Serikali ya Tanzania (kupitia Shirika la Umeme la Taifa – Tanesco) na kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Mkataba huo ulisainiwa mwaka 1995 lakini ulikumbwa na utata mwingi kutokana na gharama kubwa ya umeme iliyokuwa ikitozwa na IPTL, pamoja na tuhuma za rushwa na ufisadi katika mchakato wake.

Tanesco ilikubali kununua umeme kutoka IPTL kwa bei iliyoonekana kuwa juu sana ikilinganishwa na vyanzo vingine.

Akaunti maalumu (Escrow) iliwekwa Benki Kuu ya Tanzania kwa ajili ya malipo ya IPTL wakati mzozo kuhusu gharama ukiendelea. Baadaye, zaidi ya Sh300 bilioni zilitolewa kutoka akaunti hiyo kwa IPTL kwa utata.

Hata hivyo, umiliki wa IPTL ulibadilika mara kadhaa kwa njia tata, huku kampuni ya Pan African Power Solutions Tanzania Limited (PAP), iliyomilikiwa na Sethi, ikinunua hisa kwa njia iliyoibua maswali mengi.

Chapisho lenyewe

Kupitia ukurasa wake wa X, Aprili 4, 2025, Zitto aliandika…

1. Kampuni ya IPTL iliingia nchini katikati ya miaka ya 90 kwa lengo la kufanya biashara ya kuzalisha na kuuza umeme. Ilimilikiwa na kampuni ya Malaysia ya Mechmar na kampuni ya Kitanzania ya VIP Engineering. Mechmar walifilisika huko kwao na mali zake kununuliwa na Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong.

2. IPTL iliingia mikononi mwa mfanyabiashara Harbinder Singh Sethi mwaka 2013 kupitia hukumu ya Jaji Utamwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania. Hukumu hiyo ilitumika kuchota fedha zilizokuwa Benki Kuu katika akaunti ya Tegeta Escrow. Hata hivyo, hukumu hiyo ilitenguliwa na Mahakama ya Rufani. Hivyo, Mahakama ya Rufani ilimaliza suala la umiliki wa IPTL. Hii ndiyo mahakama ya mwisho kabisa ya nchi yetu.

3. Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong, ambayo inadai kumiliki IPTL, mara kadhaa imeishitaki Serikali ya Tanzania na kushinda kesi zote. Ushindi wao ni kuwa wao ndiyo wanastahili hisa za IPTL na hivyo kuchotwa kwa fedha za Tegeta Escrow Account iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania kulikofanywa na PAP haikuwa halali. Pesa hizo, kwa mujibu wao, kiasi cha Dola milioni 148 za Marekani, zilistahili kulipwa kwao.

4. Harbinder Singh Sethi, baada ya kukaa jela muda mrefu, aliingia plea bargain na DPP ili kuachiwa huru. Sethi ameingia makubaliano halali na Serikali kuwa atalipa kiasi hicho cha pesa, vinginevyo Serikali itawalipa SCBHK na kubaki na mitambo pamoja na mali zote za IPTL.

5. Katika makubaliano hayo na Serikali (settlement agreement), IPTL ilikubali kuwa haina madai yoyote kwenye mkataba wa umeme – PPA (Power Purchase Agreement) wala mkataba wa utekelezaji – Implementation Agreement (IA) kati yake na Tanesco. Hivyo, IPTL haina madai yoyote halali dhidi ya Serikali wala Tanesco. Ilinishangaza sana kusikia kutoka kwa CAG kuwa eti IPTL sasa wanaidai Tanesco. Ni utapeli na wizi unaopangwa. Kila Mtanzania apambane na wizi huu na yeyote anayeupanga azikwe nao.

6. Hivyo basi, kitendo cha Bwana Singh Sethi kuendelea kudai kumiliki IPTL na kuisumbua Serikali na Tanesconi utapeli wa wazi, kwa kuwa hautokani na sheria wala amri yoyote ya mahakama. Kinachofanyika, bwana huyu anakiuka plea bargain na makubaliano halali na Serikali. Anapaswa kushitakiwa criminally.

7. Serikali inapaswa kutekeleza matakwa na vipengele vyote vya settlement agreement iliyoingia kumaliza jambo hili ili suala hili lifike ukomo.

8. Brela wanapaswa kufuta usajili wa kampuni ya IPTL na takataka zingine zote zinazohusiana na IPTL. Mzoga huu sasa uzikwe!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *